Friday, June 19, 2015

India yaipa Tanzania mkopo wa Dola Mil. 268 kwa ajili ya mradi wa maji katika miji ya Tabora, Igunga, Sikonge na Nzega

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete (katikati) akiwa ameshikilia cheti kwa pamoja na Mwenyekiti wa Makampuni ya Kamal, Bw. Gagan Gupta. Bw. Gupta ni mfanyabiashara kutoka India ambaye amewekeza nchini Tanzania alikabidhiwa cheti cha kutambua mchango wake katika kukuza uchumi wa Tanzania. Cheti hicho alikabidhiwa siku ya Alhamisi jijini Delhi.



Na Ally Kondo, Delhi

Serikari za Tanzania na India zimewekeana saini Hati za Makubaliano kwa ajili ya kushirikiana katika kuendeleza sekta za maji, utalii, usafiri na usalama wa bahari pamoja na Chuo cha Takwimu cha Afrika Mashariki.  Uwekaji saini wa hati hizo umefanyika jijini Delhi siku ya Ijumaa na kushuhudiwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa India, Mhe. Narendra Modi. Rais Kikwete yupo nchini India kwa ziara ya kitaifa ya siku nne aliyoianza tarehe 17 Juni 2015.

Kwa mujibu wa Makubaliano katika Sekta ya Maji, Serikali ya India itatoa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 268.35 kwa Serikali ya Tanzania kwa ajili ya mradi wa maji katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega na Sikonge pamoja na  vijiji vitakavyopitiwa na bomba kubwa la maji litakalojengwa kutoka Ziwa Victoria.

Mradi huo utakaojengwa kwa miaka miwili na nusu na kampuni kutoka India utaanza Mwaka ujao wa Fedha 2015/16 na unatokana na ahadi ya Rais Kikwete aliyoitoa kwa wananchi wa maeneo hayo wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.

Kujengwa kwa mradi huo, itakuwa faraja kubwa kwa watu wanaoishi maeneo hayo ambayo kwa Tanzania yanakabiliwa na ukame na kupata mvua chache kwa mwaka ukilinganisha na maeneo mengine ya nchi. Watu takribani milioni 1.5 watafaidika na mradi huo utakapokamilika.

Mradi huo utakapokamilika utawaondolea wananchi adha ya kutembea mwendo mrefu kwa ajili ya kutafuta maji na badala yake watatumia muda mwingi kujishughulisha na shughuli za uzalishaji mali. Aidha, utawapa fursa watoto wa kike kujishughulisha na masomo pamoja na kutoa huduma za maji katika zahanati, vituo vya afya na mashuleni.


Kwa upande wa Makubaliano ya kushirikiana katika sekta ya utalii, inatarajiwa kuwa makubaliano hayo yatasaidia kuongeza idadi ya watalii kutoka India kuja Tanzania. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Balozi wa Tanzania nchini India, Mhandisi John Kijazi, India kila mwaka inatoa watalii milioni 128 kwenda nchi mbalimbali duniani, lakini kati ya hao ni watalii 27,000 tu, ndio wanakuja Tanzania.

Makubaliano yaliyosainiwa kwa ajili ya Chuo cha Takwimu, utakiondolea chuo hicho na uhaba wa wakufunzi na mzigo wa kugharamia wakufunzi kutoka India kwa kuwa, kuanzia sasa India itakuwa ikipeleka wakufunzi kwenye chuo hicho kwa  gharama zao.  




 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.