Na Ally Kondo, Delhi
Rais Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa
licha ya biashara kati ya Tanzania na India kuongezeka katika miaka ya hivi
karibuni, bado kuna nafasi ya kufanya vizuri zaidi endapo fursa zilizopo
zitatumiwa ipasavyo.
Rais Kikwete alisema hayo alipokuwa
anaongea na Watendaji Wakuu wa Makampuni Makubwa ya India jijini Delhi leo
tarehe 18 Juni 2015.
Rais Kikwete yupo nchini India kwa ziara
ya Kitaifa ya siku nne iliyoanzia Siku ya Jumanne tarehe 17 Juni, 2015. Alisema
kuwa lengo la ziara hiyo ni kukuza na kuimarisha mahusiano ya kibiashara kati
ya Tanzania na India, kuaga na kuishukuru India kwa misaada inayotoa tokea
uhuru hadi sasa pamoja na kuisihi nchi hiyo kumpa ushirikiano Rais
atakayechaguliwa mara uongozi wake utakapokamilika baada ya Uchaguzi Mkuu wa
Mwezi Oktoba 2015.
Katika kikao hicho, Rais Kikwete
alibainisha masuala mbalimbali ambayo yanaifanya Tanzania kuwa chaguo la kwanza
kwa Mfanyabiashara anayetaka kuwekeza. Alieleza Serikali imefanyia mabadiliko
makubwa Sera, Sheria na Kanuni mbalimbali ambazo sasa zinaruhusu na kuimarisha
Uchumi wa Soko. Kutokana na mabadiliko hayo, hakuna mwekezaji anayetakiwa kuwa
na khohu ya kutaifishwa vitega uchumi vyake endapo atawekeza nchini Tanzania.
Aliendelea kueleza kuwa Tanzania ni mwanachama wa kituo cha Kimataifa cha
Utatuzi wa Migogoro ya Kibiashara, hivyo, mwekezaji yeyote ana uhuru wa
kufikisha suala lolote katika kituo hicho ili kupata haki yake, endapo atahisi
amedhulumiwa.
Aliwambia Wakuu hao waje kuwekeza
nchini kwa sababu Tanzania ni nchi yenye amani na utulivu wa hali ya juu kwa
muda mrefu na aliwahakikishia kuwa Serikali itaendelea kudumisha amani na
utulivu huo.
Sanjari na amani na utulivu,
Tanzania imejaliwa kuwa na fursa lukuki za uwekezaji katika sekta za kilimo;
viwanda vya uzalishaji; kilimo cha biashara; madini; utalii; uchukuzi na
usafirishaji; miundombinu kama vile reli, barabara na bandari; afya; elimu na
ujenzi wa makazi.
Kwa upande wa kilimo, Rais Kikwete
alisisitiza umuhimu wa kufanya uwekezaji katika pembejeo hususan, matrekta ili
nchi iachane na matumizi ya jembe la mkono. Uzalishaji wa mbolea na dawa za
kuua wadudu wanaoshambulia mazao, uzalishaji wa mbegu za kisasa pamoja na
kujenga viwanda vya kusindika mazao, matunda na nyama.
Aidha, alisema jiografia ya Tanzania
inatoa fursa nyingi za uwekezaji hususan katika uchukuzi na usafirishaji. Hii
inatokana na nchi nyingi zinazopakana na Tanzania kuwa hazina bandari, hivyo bidhaa
zao wanazoagiza au kusafirisha nje ya nchi zinategemea Bandari ya Dar es
Salaam.
Rais aliwambia wafanyabiashara hao
kuwa, atakayekuja kuwekeza Tanzania ana uhakika wa soko kubwa la bidhaa zake
ndani na nje ya nchi. Alisema Tanzania ina fursa ya kuuza bidhaa
zinazozalishwa nchini katika nchi za SADC na EAC bila kulipa ushuru. Nchi hizo
kwa pamoja zinakadiriwa kuwa na soko la watu zaidi ya milioni 300. Aidha, nchi
za EAC, SADC na COMESA zimekubaliana kuanzisha Eneo huru la Biashara ambalo
litakuwa na soko la watu zaidi ya milioni 600.
Kwa upande wao,
wafanyabiashra hao walivutiwa na mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na
walionesha dhamira ya kuwekeza, isipokuwa waliomba kuwepo na ushirikiano mzuri
na serikali ili nia yao hiyo iweze kufanikiwa.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.