Picha na Reginald Philip
=====================================
JAPAN YAAHIDI
KUIMARISHA USHIRIKIANO NA TANZANIA
Serikali ya Japan imeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo baina yake na
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha sekta ya miundombinu
kama barabara, reli na bandari kwa maendeleo ya haraka nchini.
Kauli hiyo
imetolewa na Balozi wa Japan nchini, Mhe. Masaharu Yoshida wakati akizungumza
na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi
Liberata Mulamula kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya nchi hizi
mbili.
Balozi
Yoshida amesema kuwa Serikali yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania
katika kuhakikisha uchumi unakua kwa kasi zaidi kwa kuboresha sekta muhimu
ya miundombinu ambapo Serikali hiyo ipo tayari kuendeleza miradi mbalimbali
ambayo serikali hiyo inashirikiana na Tanzania ikiwemo barabara, reli na
bandari.
Balozi Yoshida
alibainisha kuwa miradi ambayo tayari inaendelea hapa nchini chini ya usimamizi
wa Serikali yake ukiwemo ule wa kuboresha Reli ya Kati na barabara za juu
(fly-over) katika eneo la TAZARA Jijini Dar es Salaam itajadiliwa kwa pamoja na
Serikali ya Tanzania, Ubalozi na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA) ili
kuangalia namna miradi hiyo itakamilishwa.
“Serikali ya
Japan kwa sasa inaondoka katika mfumo wa kutoa misaada na kwenda kwenye
uwekezaji, hivyo Tanzania ni mdau muhimu sana katika kufanikisha azma hiyo ili
kila upande unufaike”, alisema Balozi Yoshida.
Akizungumzia
Bandari, Balozi Yoshida alisema kuwa nchi yake ipo tayari kushirikiana na
Tanzania katika kuboresha Bandari ya Dar es Salaam pamoja na ile ya Kigoma ili
kuimarisha biashara na nchi jirani.
Akitoa taarifa
kuhusu Mkutano wa Sita wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD
VI) ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti 2016 nchini Kenya, Balozi huyo
alisema mkutano huo pamoja na mambo mengine utazungumzia Maendeleo ya
Miundombinu ya Kikanda ikiwemo mradi wa kuimarisha miundombinu ya Nchi za Kanda
ya Kati ambao Japan ipo tayari kushirikiana kikamilifu na nchi za Afrika
Mashariki kwa maendeleo ya nchi hizo.
Kwa upande
wake, Balozi Mulamula alimshukuru Balozi Yoshida kwa niaba ya Serikali ya Japan
kwa kuisadia Tanzania kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo kwa
kiasi kikubwa imechangia kuboresha maisha ya Watanzania.
“Naipongeza Serikali
ya Japan kwa kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi yake ya
maendeleo ambayo imelenga mahitaji halisi ya jamii na kuleta maendeleo ya
haraka kuanzia ngazi za chini” alisisitiza Balozi Mulamula.
Kuhusu Mkutano
wa TICAD VI, Balozi Mulamula aliipongeza Japan kwa kuwezesha mkutano huo kufanyika
Afrika kwa mara ya kwanza na kupongeza agenda za mkutano huo ambazo mojawapo
itahusu Maendeleo ya Miundombinu ya Kikanda ambapo Tanzania itatumia fursa hiyo
kuzungumzia mradi wa kuimarisha Miundombinu ya Nchi za Kanda ya Kati (Central
Corridor) kwa vile Serikali imeweka umuhimu mkubwa kwenye miradi ya aina hiyo.
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.