Safari za Mhe. Rais Jakaya Mrisho Kikwete Nje ya Nchi
Wizara imesikitishwa na taarifa za uongo
zilitolewa katika vyombo vya habari kuwa Mhe. Jakaya Kikwete, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania katika uongozi wake wa miaka 10 ametumia Shilingi
trilioni 4 kwa ajili ya safari za kikazi nje ya nchi, ambazo ni wastani wa
bajeti nzima ya wizara kwa miaka ishirini na tano (25).
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa inapenda kutoa ufafanuzi kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete aingie madarakani mwaka 2005, kiasi
kikubwa kabisa cha bajeti kuwahi kutengwa kwa ajili ya safari za Viongozi Wakuu
yaani Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni shilingi bilioni 50 ambazo
zilitengwa kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015 kwa ajili ya Idara ya Itifaki. Kwa
miaka mingine yote wastani umekuwa ni kati ya shilingi bilioni tano hadi 25
kulingana na mahitaji ya idara hiyo.
Ifahamike kuwa kiasi hicho cha shilingi
bilioni 50 ni bajeti nzima ya Idara ya Itifaki, ambapo kuna fungu maalum kwa
ajili ya ziara za viongozi. Fungu hilo linagharamia makundi makuu matano kama
ifuatavyo:
1.
Kundi la Rais wakiwemo
Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
2.
Kundi la Makamu wa Rais
wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
3.
Kundi la Waziri Mkuu
wakiwemo Wasaidizi, Mawaziri au Wakuu wa Taasisi na Walinzi;
4.
Kundi la Wakuu wa Nchi na
Serikali kutoka nje ya nchi wanapotembelea Tanzania; na
5.
Kundi la Wajumbe Maalum
wanaokuja nchini kuleta taarifa muhimu kwa Rais.
Makundi yote haya hugaramiwa na Serikali
kupitia Wizara ya Mambo ya Nje ndani ya bajeti ya Idara ya Itifaki kifungu cha
Ziara za Viongozi.
Aidha uandaaji wa bajeti ya Wizara chini ya
Idara ya Sera na Mipango unahusisha wadau wengine nje ya Wizara kama vile
Kamati ya Bunge ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na hupitishwa kila mwaka na
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Tunapenda kuwaatahadharisha wananchi juu ya
watu wanaotoa taarifa za uongo kwa madhumuni ya
kujenga chuki dhidi ya Serikali.
Ikumbukwe kuwa ziara za viongozi zinazoratibiwa na Wizara ya Mambo ya
Nje zina mafanikio makubwa kwa nchi na Watanzania kwa ujumla.
Wizara inaandaa taarifa ya ndefu ya
utekelezaji wa majukumu ya Wizara, changamoto na mafanikio yaliyopatikana ndani
ya kipindi cha miaka kumi ya uongozi wa Rais Jakaya Mrisho Kikwete ambayo
itatolewa kwa umma kwa lengo la kutoa elimu zaidi.
MWISHO.
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kwa
Umma,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa,
17 Septemba 2015
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.