Kiongozi wa Mabalozi ambaye pia ni Balozi wa Congo nchini Mhe. Juma Alfan Mpango akizungumza kwenye hafla na Mabalozi wa Afrika nchini. |
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Mulamula akisalimiana na Balozi wa Congo nchini, Mhe. Mpango (Kushoto). |
Umoja wa Mabalozi wa nchi za Kiafrika nchini Tanzania umempongeza Balozi Liberata Mulamula kwa kuteuliwa kuwa Katibu wa Kudumu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Umoja huo ukiongozwa na Balozi wa Angola nchini Prof. Ambrosio Lukoki umesema kuwa uteuzi huo umekidhi vigezo vyote na umelenga katika kuendeleza mahusiano mema yaliyopo baina ya Tanzania na nchi zingine za Afrika ambao umekuwa ukizidi kuimarika kila siku.
"Uteuzi huu una maana kubwa sana kwetu sisi Mabalozi wa nchi za Afrika tuliopo Tanzania kwani tunafahamu utendaji kazi wako hivyo tunaamini kuwa utakuwa pamoja nasi muda wote wa utumishi wako. Tunaahidi kushirikiana nawe bega kwa bega kwani uteuzi wako ni faida kwa Tanzania na Afrika nzima," alisema Prof. Lukoki.
Aidha katika hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Hyatt Regency, Balozi Mulamula alisema kuwa ni heshima kubwa kupata ukaribisho kama huo kutoka kwa Mabalozi wa Kiafrika na jambo hilo linadhihirisha ni kwa namna gani Afrika inaendeleza umoja pasipo kujali mipaka.
"Ni heshima kubwa kwangu na kwa nchi na hata bara lote la Afrika kwani ninyi ni wawakilishi wa wananchi wa nchi mnazotoka. Nitashirikiana nanyi muda wote wa utumishi wangu na pia nawaahidi kuwa muda wowote mkikwama msisite kuwasiliana nami au Wizara ya Mambo ya Nje kwa usaidizi zaidi,"
"Nafarijika sana kupata mapokezi makubwa kama haya, hali hii inaonesha ni kwa namna gani roho ya umoja inazidi kuota mizizi nje na ndani ya bara letu la Afrika. Umoja wetu ni fahari kwa kila mtu kwani tumekuwa tukishirikiana kwa karibu hata tukiwa nje ya bara letu ambalo Umoja na Upendo ndiyo kauli mbiu yetu," alisema Balozi Mulamula.
Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Congo DRC), Juma-Alfani Mpango alisema kuwa uteuzi huo ni wa kufurahisha kwao kama Mabalozi kwani wamekuwa wakishirikiana na Balozi Mulamula hata kipindi alipokuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
"Tumekuwa tukimfahamu Balozi Mulamula toka akiwa kule Marekani na utendaji wake ni mkubwa na hauna shaka. Tanzania inapaswa kujivunia watendaji kama hawa, kama Balozi wa Congo DRC nitashirikiana nawe muda wote wa utumishi wangu hapa Tanzania," alisema Balozi Mpango.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.