Mwakilishi
wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa Balozi Tuvako Manongi
akifurahia jambo na Bi Ikponwosa Ero mwenye Ualibino mara baada ya
mazungumzo yao ambapo walibadilisha mawazo kuhusu pamoja na mambo
mengine, changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino na namna gani
jumuiya ya kimatifa inaweza kushirikiana katika kuzikabili changamoto
hizo. Bi Ikponwosa aliteuliwa mwezi Agosti Mwaka huu na Kamisheni ya
Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kama Mtaalamu huru anayeendesha
kampeni, uhamasishaji, uelimishaji na uwezeshaji kuhusu watu wenye
ualibino na changamoto zinazowakabili watu wenye ualibino. Bi Ero ni
Mzaliwa wa Nigeria mwenye uraia wa Canada.
Na
Mwandishi Maalum, New York
Kutokana
na changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ualibino, Wakilishi za Kudumu
za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Malawi katika Umoja wa Mataifa,
zimewasilisha rasimu ya azimo kuhusu watu wenye ualibino.
Rasimu
ya azimio hilo inalenga katika kuzishawishi na kuzitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea
na juhudi za kutetea haki na ustawi wa watu wenye ualibino ikiwa ni pamoja na kuliwanda.
Azimio
hilo limewasilishwa kupitia Kamati ya Tatu ya Utamaduni, Haki za Binadamu na Jamii ya Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa, na ambalo limekwisha kusambazwa
kwa nchi wanachama na wadau wengine kwa ajili ya kupata maoni na kuungwa mkono.
Azimio
hilo linajielekeza pia katika kusisitiza upatikanaji wa fursa za elimu, huduma za
afya na ajira kwa watu wenye ualibino, maeneo ambayo ni changamoto kubwa kwa watu
hao.
Kupitia
azimio hilo, Tanzania na Malawi,
zinaitaka Jukumuiya ya Kimataifa kuunga
mkono jitihada zinazofanywa na nchi ambazo tayari zimejiwekea sera,
sheria na mipango ya pamoja na mambo
mengine, kuwalinda watu wenye ualbino na kuwapatia fursa mbalimbali za maendeleo
kama raia wengine.
Vile
vile, azimio hilo linamwomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuwasilisha taarifa kuhusu hali za watu wenye
ualibino mkazo ukiwa katika changamoto wanazokabiliana nazo, na juhudi ambazo zimechukuliwa na nchi wanachama
katika kuzikabili.
Taarifa
hiyo ya Katibu Mkuu inaombwa kuwasilishwa wakati wa Mkutano wa 71 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa chini ya
ajenda ya Maendeleo ya Jamii.
Azimio
hilo pia linasisitiza haja na umuhimu wa kutambua juhudi zinazofanywa katika ngazi
ya nchi na Ki- Kanda, na hivyo Katibu Mkuu anaombwa kuwasilisha katika Baraza Kuu
la 71 la Umoja wa Mataifa, mapendekezo ya
namna ya kuimarisha uwezo na juhudi za nchi husika katika kulitafutia ufumbuzi tatizo
la watu wenye ualibino kwa kadri nchi hizo
zitakavyoomba.
Katika
sehemu ya utangulizi wa Azimio, Azimio linatambua juhudi mbalimbali na taarifa za
vyombo vingine kama Vile Baraza la Haki za Binadamu, Kamisheni ya Umoja wa Afrika
kuhusu haki za watu ,kuzuia vitendo viovu na ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino.
Azimio linaeleza hofu
dhidi ya uovu wanaofanyiwa watu wenye ualibino wakiwamo wanawake na watoto.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.