Wednesday, December 23, 2015

Taarifa kwa Vyombo vya Habari




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

ZIARA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI, KIKANDA NA KIMATAIFA, MHE. DKT.AUGUSTINE MAHIGA NCHINI BURUNDI NA UGANDA
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe. Dkt. Augistine Mahiga (Mb), atafanya ziara ya kikazi ya siku mbili katika nchi za Uganda na Burundi kuanzia tarehe 23 Desemba, 2015.

Ziara hiyo ya Mhe. Mahiga inafanyika kufuatia maelekezo ya Mhe. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ya kumtaka kwenda kufuatilia hali nchini humo ili kuiwezesha Jumuiya kushughulikia mgogoro wa kisiasa unaondelea nchini Burundi.

Akiwa Uganda, 2015, Mhe. Mahiga atakutana kwa mazungumzo na Mhe. Crispus Kiyonga, Waziri wa Ulinzi wa Uganda ambaye anaendelea na jukumu  la usuluhishi wa mgogoro wa kisiasa wa Burundi kwa niaba ya Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Uganda.

Aidha, Mhe. Waziri atakutana na Mshauri wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali nchini Burundi, Ndg. Jamal Benomar.

Mhe. Waziri atasafiri siku hiyo hiyo kuelekea Bujumbura, Burundi ambapo atakutana na wadau mbalimbali wa mgogoro huo kabla ya kukutana na Mhe. Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi. Mhe. Waziri atarejea Dar es Salaam tarehe 24 Desemba, 2015 baada ya kukamilika kwa ziara hiyo.



Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,
Dar es Salaam
23 Desemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.