Wednesday, December 9, 2015

Wizara ya Mambo ya Nje na Mfuko wa UTT/PID watiliana saini makubaliano ya kuendeleza viwanja vya Balozi za Tanzania nje

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula (kulia) wakiweka saini Mkataba wa Hati ya Makubaliano (MoU) na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Umoja Unit Trust (UTT/PID),  Dkt. Gration Kamugisha,  Makubaliano hayo yatatoa fursa kwa Mfuko wa UTT/PID kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje katika kuendeleza viwanja na majengo mengine ya Ofisi za Balozi zilizopo nje ya nchi.  
Balozi Mulamula na Dkt. Kamugisha wakibadilisha Mkataba huo mara baada ya kuweka saini 
Viongozi mbalimbali wa Wizara ya Mambo ya Nje nao wakishuhudia zoezi hilo la uwekaji saini Kutoka kulia ni Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. James Lugaganya, Mkurugenzi wa Sera  na Mipango, Balozi Baraka Luvanda, Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria na Bw. Gerald Mbwafu, Afisa Mambo ya Nje.
Ujumbe ulioambatana na Dkt. Kamugisha nao wakishuhudia tukio hilo
Balozi Mulamula akiwa katika picha ya pamoja na Dkt. Kamugisha
Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Balozi Liberata Mulamula na Mtendaji Mkuu Dkt. Kamugisha wakiwa katika picha ya pamoja na Balozi Luvanda (wa tatu kutoka kulia),  Bi. Kasiga (wa kwanza kulia), na Maafisa Mambo ya Nje, Bw. Mbwafu (wa pili kutoka kulia) na Bi. Happy Ruangisa (wa kwanza kushoto) 

Picha na Reginald Philip


========================

TAARIFA YA KATIBU MKUU WA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUSAINIWA KWA HATI YA MAKUBALIANO KATI YA WIZARA NA MFUKO WA UTT/PID

Ndugu wanahabari nimewaita leo ili mshuhudie tukio muhimu la uwekaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Mfuko wa Umoja Unit Trust (UTT/PID). 

Makubaliano haya yatatoa fursa kwa Mfuko wa UTT/PID kwa kushirikiana na Wizara yangu kuendeleza viwanja na majengo mengine ya Ofisi zetu za Balozi zilizopo nje ya nchi.

Kama mnavyofahamu, Serikali ina Balozi 35 katika nchi mbalimbali duniani. Tumefanikiwa kuwa na majengo yetu wenyewe kwa ajili ya ofisi na makazi ya maafisa wetu katika Ofisi za Balozi za baadhi ya nchi. Majengo hayo yamejengwa au kununuliwa kwa kutumia fedha za Bajeti ya Maendeleo za Serikali na imesaidia kupunguza mzigo mkubwa kwa Serikali wa kulipa gharama kubwa za kodi ya pango katika nchi hizo.

Ieleweke kwamba, nia ya Wizara ni kuendeleza viwanja na majengo yote yanayomilikiwa na Ofisi za Balozi nje ya nchi.  Hivyo, Wizara imebuni mkakati wa kushirikiana na wabia mbalimbali kuhakikisha kuwa viwanja au majengo yanayomilikiwa na Balozi nje ya nchi vinaendelezwa.

UTT/PID ni mmoja wa washirika aliyeitikia wito wa mkakati huo wa Wizara ambapo baada ya kusainiwa kwa Makubaliano haya, Wizara katika siku chache zijazo itakabidhi kwa UTT/PID ripoti ya viwanja na majengo mengine inayomiliki nje ya nchi ili waainishe maeneo watakayoanza kuyaendeleza kwa kuzingatia kigezo cha fursa za kiuchumi.

Lengo la Wizara kuviendeleza viwanja hivyo, sio tu kupata ofisi na makazi ya kudumu ya maafisa wa Ubalozi bali pia kwa ajili ya vitega uchumi ambapo ofisi za ziada zitapangishwa kwa ajili ya kuingizia mapato Serikali.

Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Dar es Salaam
08 Desemba, 2015

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.