Rais Mhe. Dkt. Ally Mohamed Shein akivipongeza vikundi vya wacheza ngoma vilivyokuja kumpokea uwanjani hapo. |
Kikundi cha ngoma cha wanawake kikimpokea kwa shangwe Rais wa Zanzibar.
|
Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Kenyata akisalimiana na Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. John Haule mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro. |
Wah. Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha ya pamoja na Wah. Mawaziri wa Jumuiya hiyo.
==============================================================================================
Mkutano wa 17 wa wakuu wa nchi wanachama wa Afrika Mashariki umefanyika Jijini Arusha ambapo Tanzania ilikuwa mwenyeji na muandaaji wa Mkutano huo ambao ulifanyika katika ukumbi wa Victoria katika Hoteli ya Ngurudoto, tarehe 2 Februari 2016.
Burundi pia ilishiriki mkutano huo ambapo Mhe. Rais Pierre Nkurunziza aliwakilishwa na Makamu wa pili wa Rais Mhe. Joseph Butole. Sudan Kusini nayo ilialikwa na ikashiriki katika mkutano huo ambapo Makamu wa Rais Mhe. James Wani Igga alimwakilisha Rais wa Taifa hilo. Aidha mkutano ulihudhuriwa na waalikwa kutoka katika mataifa na jumuiya mbalimbali duniani.
Muongozo wa maadili ya biashara "Code of conduct for business in EAC" pia ulisainiwa na wakuu wa nchi wa jumuiya hiyo, lengo likiwa kuziinua nchi hizo katika hali duni ya umasikini na kuwekeza katika biashara zenye manufaa makubwa kwa mataifa hayo na kuhakikisha kila taifa halikiuki taratibu zilizowekwa. Pia Tanzania chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeombwa kuendelea kuongoza umoja huo kwa mwaka mmoja zaidi. Wakuu hao wa nchi walimuomba Mhe Rais Magufuli kusimamia jumuiya hiyo kwa kutumia kauli mbiu yake ya "hapa kazi tu" kwa vitendo na si kwa maneno. Rais Magufuli alikubali ombi hilo na kuahidi kutowaangusha katika utendaji kazi na kwamba ataanza na kuangalia utendaji wa ofisi ya Jumuiya hiyo akisisitiza asiyeweza kuendana na kasi yake basi hafai kuwepo katika taasisi hiyo. Mhe. Rais Magufuli alieleza pia kwa upande wa usuluhishi wa mgogoro wa Burundi Mhe. Yoweri Museveni alifanyie kazi suala hilo ili kuepuka madhara yatokanayo na migogoro. Wakati huo huo, Rais Mstaafu wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Benjamin W. Mkapa amechaguliwa kuwa msuluhishi katika mgogoro wa Burundi, hivyo ataenda kuongeza nguvu kwa Mhe. Yoweri Museveni na akawasihi wanajumuiya kuwapa ushirikiano wasuluhishi hao. Sambamba na hayo suala la kuanzisha na kukuza viwanda ndani ya jumuiya nalo lilionekana kuwa jambo la msingi kwa mataifa yote ili kuweza kuzalisha bidhaa zenye ubora na zitakazowezesha kukua kwa uchumi, pamoja na lugha ya Kiswahili kutumiwa na wanachama wote ili kurahisisha mawasiliano katika shughuli za kiuchumi. Mwisho wakuu hao wa nchi walimpongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kushinda katika uchaguzi na kupata nafasi ya kuwa Rais na pia walimpa pongezi kwa kuweza kuandaa Mkutano uliofanyika katika hali ya amani na utulivu na kuwezesha kufanikisha mambo muhimu yaliyoweza kutekelezwa katika mkutano huo. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.