Tuesday, March 29, 2016

Waziri Mahiga aeleza msimamo wa Serikali juu ya uamuzi wa Bodi ya MCC

 Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Mhe.Balozi  Dkt. Augustine Mahiga(Mb) akiwa katika Mkutano na waandishi wa  habari uliofanyika katika ukumbi wa ofisi ya Wizara ambapo alieleza msimamo wa  Serikali ya Tanzania juu ya kusitishwa kwa fedha za Mpango wa kukabiliana na changamoto za Milenia ambao umekuwa ukitolewa na Shirika la Millenium Challenge Corporation (MCC) la nchini Marekani.
Sehemu ya waandishi wa Habari wakifuatilia Mkutano huo.
Waziri akifafanua jambo kwa waandishi wa habari ambao hawapo pichani. Wengine katika picha ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika, Balozi Joseph Sokoine (kushoto) na Bi. Mindi Kasiga, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali. 
=======================================================
Serikali ya Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa Serikali ya Marekani wa kutoipatia fedha za awamu ya pili ya Mpango wa ushirikiano wa kushughulikia Changamoto za Milenia (Millenium Challenge Corporation MCC-2) kiasi cha Dola za Marekani milioni 472 kwa ajili ya kukamilisha miradi ya umeme vijijini na kuitaka nchi hiyo kutafakari upya uamuzi huo.


Hayo yalisemwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Dkt. Augustine Mahiga alipozungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam kuelezea msimamo wa Serikali kufuatia uamuzi huo.

Mhe. Mahiga alisema kuwa uamuzi huo ambao haukuishirikisha Tanzania kwa namna yoyote umetolewa na Bodi ya MCC ambayo imekutana Jijini Washington DC hivi karibuni.

Katika maelezo yake, Waziri Mahiga alisema kuwa, Awamu ya Kwanza ya mpango huo ilitolewa na Marekani baada ya Tanzania kukidhi vigezo ambavyo ni pamoja na kufuata misingi ya demokrasia, kupambana na rushwa, utawala bora na kuheshimu haki za binadamu. 
Hata hivyo alieleza kushangazwa kwake na uamuzi wa sasa wa nchi hiyo wa kuahirisha kuipatia Tanzania  fedha za awamu ya pili ya mpango huo kwa madai kuwa haikukidhi vigezo hususan kwa kufuta uchaguzi wa Zanzibar na kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Mitandao ambayo wamedai inawanyima wananchi uhuru wa kujieleza.

“Tanzania imesikitishwa na uamuzi wa Marekani wa kuinyima fedha za MCC kwa madai kuwa hatujakidhi vigezo ambavyo ni vigezo hivyo hivyo walivitumia kutupatia awamu ya kwanza ya fedha hizo. Ni matumaini yangu kuwa watatafakari upya uamuzi wao” alisema Balozi Mahiga. 

Kuhusu, Zanzibar Balozi Mahiga alifafanua kuwa ni nchi huru ambayo inaendesha mambo yake kwa uhuru hususan masuala ya uchaguzi ambayo si ya muungano. Hivyo uamuzi wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ya kufuta uchaguzi uliofanyika mwezi Oktoba 2015 baada ya kutokea kasoro huko Pemba, ulikuwa ni uamuzi wa Tume na unatakiwa kuheshimiwa.

Aidha, kuhusu Sheria ya Makosa ya Mitandao ya Mwaka 2015 (Cyber Crime Act), Balozi Mahiga alieleza kuwa nayo kwa kiasi kikubwa ilianzishwa ili kukabiliana na vitendo vya kigaidi na uhalifu mwingine wowote unaofanyika kupitia mitandao. 

“Kwa mantiki hiyo, Tanzania haikupaswa kuadhibiwa kwa kuangalia masuala hayo pekee wakati kwa muda mrefu Tanzania imejijengea sifa ulimwenguni kote ya kufuata misingi ya demokrasia na utawala bora,” alisisitiza Balozi Mahiga.

Akizungumzia uhusiano kati ya Tanzania na Marekani, Waziri Mahiga alisema kuwa unaendelea kama kawaida kwani MCC ni kipengele kimoja tu katika masuala mengine mengi ya ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.

“Marekani imekuwa ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kila mwaka huipatia nchi yetu msaada wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 700 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya. Hivyo MCC ambayo ni mpango mwingine wa msaada kutoka nchi hiyo ni sehemu ya mambo kadhaa tunayoshirikiana na Marekani” alifafanua Dkt. Mahiga.

Akielezea athari zitakazotokana na kukosekana kwa fedha hizo za Awamu ya Pili ya MCC, Mhe. Mahiga alisema kuwa kwa kiasi fulani Tanzania itaathirika hususan katika eneo la usambazaji wa Nishati ya Umeme Vijijini. Hivyo alisisitiza umuhimu wa Marekani kutafakari upya uamuzi wao huo.

“Marekani inazitaka nchi zipambane na kuondokana na umaskini. Umoja wa Mataifa nao umeanzisha Malengo ya Maendeleo Endelevu ambayo yanalenga kupambana na umaskini. Hata hivyo nasikitika kuwa kuondolewa kwa MCC Tanzania hakutaiwezesha kufikia malengo ya milenia wala dhamira njema ya Marekani ya kuzitaka nchi zinazoendelea kuondokana na umaskini. Kwa maana nyingine nasema ni Malengo ya Milenia na MCC dhidi ya Tanzania”, alieleza Dkt. Mahiga.

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizonufaika na Mpango wa kukabiliana na Changamoto za Milenia (MCC) ambapo katika awamu ya kwanza ya mpango huo, Tanzania ilipatiwa kiasi cha Dola za Marekani Milioni 698. 

Fedha hizo zilikuwa ni kwa ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo katika uboreshaji wa maeneo ya miundombinu ya barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga. 

Pia zilitumika kujenga mfumo wa maji kwa miji ya Dar es Salaam na Morogoro. Vile vile fedha hizo zilitumika kutandaza njia ya kusafirisha umeme chini ya Bahari ya Hindi kati ya Bara na Tanzania Visiwani na pia kujenga barabara zote kuu za Kisiwa cha Pemba na baadhi ya barabra za Unguja kwa kiwango cha lami.

-Mwisho-
 


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.