TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkutano wa Kimataifa kujadili Utawala wa Sheria kufanyika nchini
Mkutano wa Kimataifa kujadili masuala ya Utawala wa Sheria kama chachu ya Maendeleo Endelevu unatarajiwa kufanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam tarehe 1 na 2 Juni, 2016.
Mkutano huo ambao utafanyika katika ngazi ya Mawaziri kutoka nchi mbalimbali za Afrika utafunguliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Harison Mwakyembe (Mb.) na kuhudhuriwa na Mawaziri kutoka nchi za Afrika, Maafisa Waandamizi wa Serikali na Wakuu wa Taasisi mbalimbali za Kimataifa.
Mkutano huo unaolenga kuweka sera, mikakati thabiti, pamoja na kubadilishana uzoefu, weledi na ujuzi miongoni mwa washiriki ili kuwawezesha kutekeleza malengo mapya ya dunia chini ya dira mpya ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo ya Dunia ijulikanayo kama “Agenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030” yenye jumla ya Malengo 17. Malengo hayo yanarithi Malengo ya Milenia yaliyomaliza muda wake mwaka 2015.
Ikumbukwe kuwa, mwezi Septemba 2015 Jumuiya ya Kimataifa ilifikia makubaliano ya kihistoria kwa kupitisha Agenda mpya ya Maendeleo Endelevu wakati wa Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa uliofanyika Mjini New York, Marekani. Katika mkutano huo, Wakuu wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa walikubaliana kuwa na Dira Mpya ya Maendeleo ya Dunia ikilenga katika kutokomeza umaskini; kulinda mazingira; kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kushirikisha makundi yote kwenye jamii katika masuala ya maendeleo.
Mkutano huo wa siku mbili umeandaliwa na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Sheria (International Development Law Organisation-IDLO) yenye Makao yake makuu mjini Roma, Italia kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mkutano huo unatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki takriban 70 kutoka ndani na nje ya Tanzania na umejikita zaidi kwenye lengo Namba 16 linalohimiza haki, amani na jamii shirikishi.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Mei 2016.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.