Thursday, June 2, 2016

Bunge lapitisha Bajeti ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (Mb.) akipongezwa na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini mara baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2016/2017. Mhe. Mahiga aliwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara Bungeni tarehe 31 Mei, 2016.
Mhe. Mahiga katika picha  na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi (mwenye miwani) na Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mhe. Mchungaji Peter Msigwa (wa nne kulia) pamoja na wajumbe wengine mara baada ya Bajeti ya Wizara kupitishwa na Bunge
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Susan Kolimba (Mb.) naye akipongezwa na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nhini mara baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2016/2017.


 ===================================================================


 HOTUBA YA MHESHIMIWA BALOZI DKT. AUGUSTINE PHILIP MAHIGA (MB), WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI AKIWASILISHA MAKADIRIO YA BAJETI YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA
MWAKA WA FEDHA 2016/2017





UTANGULIZI


1. Mheshimiwa Spika, kutokana na Taarifa iliyowasilishwa leo Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kujadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

2.      Mheshimiwa Spika, awali ya yote nakushukuru kwa fursa hii adhimu ya kuwasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu kwa mara ya kwanza Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Aidha, naomba nitumie nafasi hii adhimu kumpongeza kwa dhati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba, 2015.  

3.      Mheshimiwa Spika, naungana na walionitangulia kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa uongozi wake madhubuti na makini unaoakisi kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’. Sisi sote ni mashahidi wa namna uongozi wake ulivyogusa si tu wananchi wa Tanzania bali pia ulivyopokelewa na kuwa mfano wa kuigwa katika nchi za bara la Afrika na duniani kwa ujumla. Sifa zake zinasikika kila pembe ya dunia na kutufanya tutembee kifua mbele. Nampongeza sana kwa kumteua Mheshimiwa Samia Suluhu kuwa Mgombea Mwenza na baadae kuchaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya nchi yetu. Kuchaguliwa kwake kumeidhihirishia dunia hatua kubwa ambayo nchi yetu imepiga katika kumpa fursa sawa mwanamke.

4.      Mheshimiwa Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kipindi cha pili katika uchaguzi ulioendeshwa kwa amani na usalama. Kadhalika, nampongeza Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), kwa kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wizara yangu imefaidika sana na uongozi wao na miongozo mbalimbali wanayoitoa katika utekelezaji wa majukumu yetu.

5.   Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu walionitangulia kuwashukuru na kuwapongeza watoa hoja waliozungumza kabla yangu wakiongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango (Mb), Waziri wa Fedha na Mipango ambao hotuba zao zimeweka msingi mzuri kwa kuainisha dira na masuala muhimu ya kitaifa na kimataifa ambayo baadhi yake yanaangukia katika majukumu ya Wizara yangu.  Kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais kujenga ‘Tanzania ya Viwanda’ na kama ilivyotafsiriwa katika Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2016/2017 hadi 2020/2021, Wizara yangu nayo imejielekeza katika kutekeleza ‘Azma ya Serikali ya kujenga Uchumi wa Viwanda’.

6.      Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu, Wizara hii ni mpya baada ya kuunganishwa kwa zilizokuwa Wizara mbili za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Kwa ajili hiyo, namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa kwanza wa Wizara hii. Napenda kumuahidi mbele ya Bunge lako Tukufu kuwa nitatumia ujuzi na uzoefu mkubwa niliouvuna katika nyanja za diplomasia ya kikanda na kimataifa kuendelea kuipaisha diplomasia ya Tanzania.

7.      Mheshimiwa Spika, kazi yangu imefanywa kuwa nyepesi zaidi kutokana na ushirikiano mzuri na ushauri tunaoupata mara kwa mara kutoka kwenye Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi wa Mheshimiwa Balozi Adadi Mohammed Rajab (Mb), na Makamu wake Mheshimiwa Kanali Mstaafu Masoud Ali Khamis (Mb) pamoja na Wajumbe wote wa Kamati hiyo. Wamekuwa wa msaada mkubwa sana kwa Wizara yangu katika utekelezaji wa majukumu.

8.      Mheshimiwa Spika, ukiniona nasimama mbele ya Bunge lako Tukufu kwa kujiamini ni kwa sababu ninao nyuma yangu viongozi wenzangu, watendaji na wafanyakazi wanaonisaidia kutekeleza majukumu yangu kwa ufanisi mkubwa. Napenda kumshukuru Mheshimiwa Dkt. Susan Alphonce Kolimba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Aziz Ponary Mlima, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Mabalozi, Maafisa na Wafanyakazi walioko Makao Makuu, Balozini na Ofisi ya Zanzibar kwa msaada mkubwa wanaonipatia.  Uzalendo wao, ari yao na imani yao kwangu, vinanipa kila sababu ya kuamini kuwa malengo tuliyojiwekea katika Bajeti hii tutayatekeleza kwa ufanisi mkubwa.

9.      Mheshimiwa Spika, mwisho lakini si mwisho kwa umuhimu,  namshukuru kwa dhati mke wangu mpendwa Mama Elizabeth Mahiga, Watoto na familia yangu yote kwa ujumla kwa kunivumilia, kuniunga mkono na kunipa utulivu wa kutosha kuniwezesha kuyakabili  majukumu niliyopewa na Mheshimiwa Rais kutimiza matarajio ya Watanzania.



10.     Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa, naungana na Wafanyakazi wa Wizara yangu kutoa salamu za pole na rambirambi kwa familia za Watumishi wenzetu watatu, Marehemu Manfred Ngatunga, Marehemu Apolonia Mbogo Mwangosi na Marehemu Ezekiel Makonda, ambao walifikwa na mauti wakati wakiendelea kuitumikia Wizara na Taifa kwa ujumla. Tuendelee kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awapumzishe kwa amani. Amina.



11.     Mheshimiwa Spika, hotuba hii imejumuisha shughuli zilizokuwa zikifanywa na iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Hivyo, nitatoa taarifa ya mapato na matumizi ya Wizara hizo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na kuwasilisha Mpango na Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.

TATHMINI YA HALI YA DUNIA


Hali ya Uchumi, Siasa na Usalama Duniani

12.     Mheshimiwa Spika, hali ya dunia imeendelea kuwa ya mchanganyiko wa matumaini na mashaka. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita dunia imepiga hatua kwenye masuala kadhaa ya msingi kwa ustawi na mustakabali wa dunia. Katika kipindi hiki tumeshuhudia kusainiwa kwa Mkataba wa Paris kuhusu Tabianchi mwezi Desemba, 2015 ambao umesubiriwa kwa muda mrefu. Kusainiwa kwa Mkataba huu kunatoa matumaini kwa nchi za Afrika na zile zinazoendelea kwa kuwepo kwa uhakika katika Kudhibiti  na Kukabili athari na changamoto za tabianchi. Hii ni kutokana na ukweli kuwa nchi zetu zinaathirika zaidi na athari za tabianchi wakati ni wachangiaji wadogo sana wa tatizo hilo. Kusainiwa kwa Mkataba huu kunatoa fursa kwa nchi maskini kufidiwa na kujengewa uwezo katika kukabiliana na changamoto hizo. Hili ni jambo ambalo nchi yetu imekuwa mstari wa mbele kulipigania na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliongoza jitihada hizi akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Wakuu wa Nchi wa Umoja wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi.

13.     Mheshimiwa Spika,  jambo lingine la kutia matumaini ni kusainiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu  ambayo yanachukua nafasi ya Malengo ya Milenia  ya mwaka 2000 - 2015  ambayo utekelezaji wake ulifikia tamati mwezi Septemba, 2015. Majadiliano kati ya nchi zetu yaliyofikia malengo haya yalizingatia uzoefu katika utekelezaji wa Malengo ya Milenia, haja ya kumalizia viporo vya Malengo ya Milenia na umuhimu wa kuhakikisha kuwa malengo mapya yanazingatia mahitaji ya leo na kesho kwa kuhakikisha kuwa ni endelevu. Malengo ya Maendeleo Endelevu ndio mwongozo wa agenda ya maendeleo duniani kote na ndiyo yatakayokuwa rejea ya majadiliano na makubaliano mengine duniani. Sisi tumejipanga vyema kutekeleza malengo hayo na bahati nzuri yanashabihiana kwa kiwango kikubwa na Dira yetu ya Taifa ya 2025 na Mpango wa Pili wa Maendeleo 2016/2017 – 2020/2021.

14.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita kumekuwa pia na matukio ambayo yana mwelekeo mzuri kwa ustawi wa amani na usalama duniani. Kwa kuwa yako mengi, niruhusu niyataje mawili makubwa. Kwanza, ni hatua ya nchi za Marekani na Cuba kuamua kurejesha urafiki wao baada ya kuwepo kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba kwa zaidi ya miaka 50. Hatua hii ni muhimu na tunaungana na wapenda amani kote duniani kumpongeza Rais Barack Obama wa Marekani na Rais Raul Castro wa Cuba. Ikumbukwe kuwa Marekani na Cuba ni rafiki wa Tanzania, na Tanzania imekuwa mstari wa mbele kupinga vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba. Ni faraja kuwa uhasama huo umekwisha, kwani kuondolewa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya Cuba kutawezesha Cuba kushiriki kikamilifu katika uchumi wa Dunia, na hali kadhalika itaimarisha ushirikiano mzuri wa kiuchumi tulionao kati yetu na Cuba. Makubaliano hayo yamemaliza mabaki ya misuguano ya vita baridi ya miongo ya nyuma na kuendeleza amani duniani.

15.     Mheshimiwa Spika, tukio la pili, ni kuondolewa kwa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran kuhusu Mpango wa Iran wa Nyuklia tarehe 16 Januari, 2016, kufuatia Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki kuthibitisha kuwa Iran imekamilisha hatua zote ilizopewa na Wanachama wa Kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Ujerumani. Hatua hii nayo ni muhimu sana kwa kuwa inaondoa hali ya mashaka iliyokuwa imetanda katika eneo la Mashariki ya Kati kuhusu nchi ya Iran kutengeneza silaha za nyuklia. Mashaka hayo ndiyo ambayo yamekuwa yakiyumbisha sana dunia kiuchumi kwa kuathiri bei za mafuta. Iran ni nchi rafiki ambayo tunashirikiana nayo kiuchumi. Hivyo, kuondolewa kwa vikwazo hivyo kunatoa fursa ya kukua kwa ushirikiano wa kiuchumi kati ya nchi hizi mbili katika mazingira ya amani.

16.     Mheshimiwa Spika,  pamoja na matumaini hayo, yako matukio na mambo ambayo yanaiweka dunia katika hali ya tahadhari. Hali ya uchumi duniani haijaimarika sana na inapitia katika mashaka makubwa. Hii inatokana na sababu kadhaa zikiwemo kupungua kwa kasi ya ukuaji wa uchumi mkubwa wa China kutoka asilimia 6.9 hadi asilimia 6.3; kushuka kwa bei ya bidhaa duniani kama dhahabu, mafuta, shaba na bidhaa nyingine muhimu; na kupungua kwa mitaji na uwekezaji. Kuteremka kwa bei ya mafuta hakujaleta unafuu sana kwetu kwa sababu bei ya bidhaa zetu muhimu kwenye soko la dunia nazo zimeporomoka na thamani ya fedha imepungua. Aidha, riba ya mikopo na mitaji imepanda.  Hali hii si afya kwa uchumi wa nchi masikini na zinazoendelea kwa kuwa kushuka kwa bei ya bidhaa kunaathiri sana uchumi wa nchi zetu zenye uwezo mdogo wa kuhimili misukosuko ya uchumi wa dunia.

17.     Mheshimiwa Spika, hali ya usalama duniani nayo imeendelea kutoridhisha. Kumekuwepo na kuongezeka kwa wasiwasi wa kiusalama kati ya Ulaya Magharibi na Urusi, Korea Kaskazini na nchi za Asia hasa Korea Kusini inayosaidiwa na Marekani, Syria na nchi za Mashariki ya Kati na kupanuka kwa shughuli na dhana ya himaya ya Islamic State  katika eneo lote la ukanda huo.  Dhana hiyo inayosimamiwa katika eneo lote na kundi la  Islamic State of Syria (ISS) imeanza kujipenyeza Afrika Mashariki, Magharibi na Kaskazini hasa Lybia.  Dhana ya himaya hiyo au Caliphate ni kali zaidi kuliko mlengo wa Al - Qaeda.  Dunia inaelekea tena kwenye ushindani mkali wa mataifa makubwa hasa kati ya Marekani, Urusi na China.  Kwa muktadha huo, Tanzania itaendelea kufuata siasa isiyofungamana na upande wowote. Yote haya kwa pamoja yanaiweka dunia katika hali ya tahadhari kubwa na hivyo kuilazimu dunia kuelekeza fedha na muda wake mwingi katika ushindani na kutafuta ufumbuzi badala ya kuelekeza muda na rasilimali hizo kujenga uchumi na kuinua hali ya maisha ya watu. Tanzania imeendelea kutoa mchango wake wa moja kwa moja na kwa kushirikiana na nchi nyingine katika kutatua migogoro ya Kanda na kudumisha amani duniani. Kwa mantiki hiyo, Mheshimiwa Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete aliteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Umoja wa Afrika katika Mgogoro wa Libya na Mheshimiwa Rais Mstaafu Benjamin William Mkapa aliteuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki kuwa Msuluhishi wa Mgogoro wa Burundi. Uteuzi wa Viongozi wetu Wastaafu wa Kitaifa ni ushahidi kuwa kauli ya Tanzania inasikilizwa na kuheshimika kwenye majukwaa ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

18.     Mheshimiwa Spika, Macho na masikio ya dunia yameelekezwa huko Asia-Pacific kutokana na fukuto la mgogoro wa umiliki wa eneo la Bahari ya Kusini mwa China unaohusisha nchi za China, Brunei, Vietnam, Malaysia na Ufilipino. Pamoja na kuwa kijiografia eneo hili laweza kuonekana ni mbali sana na nchi yetu, athari za mgogoro huo zitagusa kila pembe ya dunia kama hautamalizika kwa njia za amani. Eneo hilo ndio penye kitovu kikubwa cha ukuaji wa uchumi, uzalishaji na biashara katika kipindi hiki ambacho uchumi wa dunia kiujumla unasuasua. Tanzania inaamini kuwa njia ya uhakika ya kumaliza mgogoro wa Bahari ya Kusini mwa China ni kupitia mazungumzo baina ya nchi na nchi na kanda. Kwa sababu hiyo, tunaunga mkono juhudi za utatuzi wa mgogoro huo kwa njia ya mazungumzo na mashauriano. Tunaitaka Jumuiya ya Kimataifa na vyombo vyake kuzingatia Azimio Na. 298 la mwaka 1982 la Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria ya Bahari.

MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016

ILIYOKUWA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA


19.     Mheshimiwa Spika, kabla ya kueleza utekelezaji wa Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa fedha 2015/2016, naomba uniruhusu niainishe kwa ufupi majukumu ya iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kama ifuatavyo:-

             i.        Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Nchi ya Mambo ya Nje;
           ii.        Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa;
          iii.        Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali, Ushirikiano wa Kimataifa, Bara la Afrika na Kikanda;
          iv.        Kulinda na kuendeleza Maslahi ya Taifa ya Kiuchumi na Mengineyo nje ya nchi;
            v.        Kusimamia masuala yanayohusu Kinga na Haki za Kibalozi kwa Wanadiplomasia waliopo nchini kulingana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961;
          vi.        Kusimamia na kuratibu masuala ya Itifaki na Uwakilishi;
        vii.        Kuanzisha na Kusimamia Huduma za Kikonseli;
       viii.        Kuratibu shughuli za Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano; na
          ix.        Kusimamia utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu.

20.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza majukumu hayo kwa mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara ilitengewa kiasi cha Shilingi 170,367,129,238.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 162,367,129,238.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo. Katika fedha zilizotengwa kwa Matumizi ya Kawaida, shilingi 153,698,142,238.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na  Shilingi 8,668,987,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi.

21.   Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara na Balozi zake ilitarajia kukusanya maduhuli ya kiasi cha shilingi 20,036,019,000.00. Hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2016, Wizara imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 16,296,907,020.00 ikiwa ni sawa na asilimia 81.3 ya makisio ya makusanyo yote ya maduhuli kwa mwaka  wa fedha 2015/2016.

22.   Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili, 2016 Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 126,407,697,224.00 sawa na asilimia 77.8 ya bajeti iliyopitishwa na Bunge. Kati ya fedha hizo Shilingi 117,783,609,614.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 8,624,087,610.00 ni kwa ajili ya mishahara ya Watumishi. Hadi hivi sasa, Wizara bado haijapokea mgao wowote wa fedha za bajeti ya maendeleo.

23.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, Wizara imetekeleza majukumu yake kama ifuatavyo:-

 Kubuni na Kusimamia Utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje

24.   Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Balozi zake, Taasisi nyingine za Serikali na sekta binafsi imeendelea kubuni na kusimamia utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje yenye lengo la kukuza uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya uchumi iliyo endelevu. Aidha, jukumu hili limepewa uzito zaidi na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati alipozindua Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo aliziagiza Balozi zetu kushiriki Mikutano inayofanyika nje kwa niaba ya Wizara, Idara na Taasisi nyingine za Serikali. Jukumu hili kubwa limetekelezwa ipasavyo na Balozi zetu na hivyo kupunguza gharama kubwa za safari ambazo zingefanywa na Watumishi wa Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

25.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kufanikisha ziara za Viongozi Wakuu wa Kitaifa hapa nchini kutoka nchi za Vietnam na Msumbiji. Wizara pia iliratibu ziara za viongozi mbalimbali kutoka nchi za Saudi Arabia, Oman, Qatar, Ujerumani, Norway, Umoja wa Falme za Kiarabu, Sweden, Finland, Ireland, Czech, Italia, na Urusi. Pamoja na mambo mengine ziara hizo zililenga kuimarisha, mahusiano ya biashara na uwekezaji kati ya nchi yetu na nchi hizo. Aidha, baadhi ya nchi hizo tayari zina mikataba ya Ushirikiano na Tanzania na nyingine zimeanzisha ushirikiano kwa mara ya kwanza.

26.   Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilifanikisha kufanyika makongamano na maonesho ya biashara na uwekezaji yaliyolenga kutangaza fursa za biashara na uwekezaji zilizopo hapa nchini. Makongamano hayo yalijumuisha wafanyabiashara na wawekezaji wa Tanzania na nchi za Oman, Urusi, Rwanda, Ujerumani, China, India, Czech, Comoro, Misri na Singapore.

27.   Mheshimiwa Spika, kutokana na makongamano hayo, Tanzania iliweza  kutangaza fursa zake mbalimbali katika biashara na uwekezaji na kufanikisha yafuatayo:-

(a)  Kusainiwa kwa mkataba wa makubaliano ya ushirikiano baina ya Chama cha Wafanyabiashara, wenye Viwanda na Wakulima Tanzania na Chama cha Wafanyabiashara wa Oman wa kuanzisha Kampuni ya Uwekezaji kati ya Tanzania na Oman. Kampuni hiyo imeanzishwa kwa lengo la kutafuta fursa za uwekezaji Tanzania na Oman na imeazimia kuanza na mtaji wa Dola za Marekani milioni 25 ambazo zitatumika kutoa mikopo kwa wawekezaji. Mkataba huo ulisainiwa mwezi Aprili 2016, Dar es Salaam wakati wa Kongamano la Biashara na Uwekezaji baina ya Tanzania na Oman;

(b) Serikali ya Oman pia imeanza mazungumzo na kiwanda cha sukari Kagera kwa nia ya kuingia makubaliano yatakayowezesha Serikali ya Oman kuwekeza katika kiwanda hicho. Hatua hii inalenga kukiwezesha kiwanda kuzalisha tani laki nne za sukari ambazo zitauzwa hapa nchini na hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa sukari. Ongezeko hili la uzalishaji  pia litawezesha kuzalisha hamira, spiriti na umeme. Hamira itauzwa Oman na sehemu nyingine wakati umeme utaingizwa katika gridi ya taifa; na  

(c)  Kuanzishwa kwa Kiwanda cha utengenezaji wa pikipiki katika eneo la Ukanda Maalum wa Kiuchumi wa Bagamoyo kupitia Kampuni ya Guanghzhou Fekon Motorcycle Co. Ltd. ya China. Aidha, Kampuni hiyo imeahidi kufungua Chuo maalum kwa ajili ya mafunzo ya ufundi wa pikipiki na makenika. Vilevile, mwekezaji huyo ameahidi kutoa nafasi kwa ajili ya vijana wa Tanzania kwenda China kupata ujuzi wa masuala hayo katika kiwanda mama kilichopo China. Makubaliano hayo yalifanyika wakati wa kongamano la biashara na uwekezaji baina ya Afrika na China lililofanyika mwezi Agosti 2015 mjini Guangzhou China.

28.   Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje imefanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta za miundombinu, nishati, viwanda,  kilimo na  mifugo. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2015/2016 ni pamoja na:-
(a)  Mradi wa barabara ya Ndundu-Somanga yenye urefu wa kilomita 60 uliozinduliwa mwezi Agosti, 2015. Barabara hiyo imejengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait kwa kushirikiana na Mfuko wa Umoja wa Nchi zinazozalisha Mafuta Duniani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
(b) Mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kidahwe-Uvinza yenye urefu wa kilomita 76.6 uliozinduliwa mwezi Septemba, 2015. Barabara hiyo imejegwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kupitia Mfuko wa Maendeleo wa Abu Dhabi kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 57 pamoja na mchango wa fedha za ndani;
(c)  Mradi wa Daraja la Kikwete kwenye mto Malagarasi mkoani Kigoma lililozinduliwa mwezi Septemba, 2015. Daraja hilo limejengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Uchumi wa Jamhuri ya Korea;
(d) Mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ukamanda na Unadhimu cha Tengeru, Arusha kilichozinduliwa mwezi Agosti 2015 ambao ulitekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu; na
(e)  Mradi wa ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo na Eneo Huru la Kiuchumi uliozinduliwa Oktoba 2015. Mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano baina ya Serikali ya Tanzania, China na Oman.

29.   Mheshimiwa Spika, katika hatua nyingine Wizara imeendelea kuzungumza na kuwashawishi wadau mbalimbali wa maendeleo ili kusaidia jitihada  za Serikali katika kukabiliana na changamoto ya ujangili hapa nchini, hususan upatikanaji wa vifaa kwa ajili ya kufanyia doria kwenye Mbuga na Hifadhi za Taifa. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika kipindi hiki, Serikali ya Ujerumani imeipatia Tanzania ndege mbili ndogo kwa ajili ya kupambana na ujangili. Tunaamini kuwa ndege hizo zitaongeza ari na ufanisi kwa askari wetu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kuendesha doria katika Hifadhi za Taifa na Mapori ya Akiba yaliyopo nchini. Vilevile, nchi nyingi za Ulaya, Marekani na Mashirika ya Kimataifa kama vile World Wildlife Fund, Frankfurt Zoological Society zimeonyesha utayari wa kuisaidia Tanzania kwa hali na mali katika kulinda hifadhi za wanyamapori.

30.   Mheshimiwa Spika, Kadhalika, Wizara kwa kushirikiana na wadau wengine, imefanikisha majadiliano na Serikali ya Ufaransa kwa ajili ya kusaidia mpango wa maboresho ya jengo la abiria (Terminal II) katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo imekubali kuipatia Serikali ya Tanzania kiasi cha Euro Milioni 65 kwa ajili ya ukarabati na uboreshaji wa uwanja huo.

31.    Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu  na Mafunzo ya Ufundi imeendelea kutafuta fursa za masomo nje ya nchi ili kuliwezesha Taifa kuwa na hazina kubwa ya wataalam katika sekta mbalimbali. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa nchi rafiki za Algeria, Malaysia, Indonesia, Pakistan, Iran, Malta, Misri, Sri Lanka, Brunei Darussalam, Canada, Ujerumani, Uingereza, Marekani, Uholanzi, Ubelgiji, Oman, Urusi, Australia, Japan, China, Cuba, Ufaransa, Thailand, Uswisi na Korea pia zimeendelea kushirikiana nasi katika kuwajengea uwezo Watanzania kupitia ufadhili wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika fani mbalimbali.

32.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kufanikisha upatikanaji wa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 20 kutoka Serikali ya Italia, kupitia Shirika la Maendeleo la nchi hiyo. Mkopo huo utatumika kutekeleza mradi wa Technical and Labour Market Support Programme unaolenga kuimarisha na kukuza elimu ya Ufundi kwa kuvijengea uwezo vyuo vya ufundi ili kutoa mafunzo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira. Vyuo vitakavyonufaika na mradi huo ni pamoja na Chuo cha Ufundi Dar es Salaam, Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya.

33.   Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea na juhudi za kuwatafutia fursa za ajira na kuwaandalia mazingira mazuri watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi. Kufuatia Mkataba wa ajira baina ya Tanzania na Qatar, Watanzania wapatao 250 wamekwenda Qatar kufanya kazi kuanzia mwezi Desemba, 2015. Timu za pande zote mbili zinaendelea na uratibu wa kuwapata Watanzania watakaoweza kunufaika na fursa hiyo. Aidha, Wizara pia inaendelea kuwasaidia Watanzania kupata kazi katika makampuni mbalimbali nje ya nchi mathalani katika Mashirika ya Ndege yanayofanya safari zake hapa nchini. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Watanzania 18 walipata kazi katika Shirika la Ndege la Emirates na jitihada kama hizo zinaendelea kufanyika kwa mashirika mengine. Nichukue fursa hii kutoa wito kwa vijana wa Tanzania kujitokeza na kuomba kazi katika Mashirika ya Kimataifa.

34.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kufanikisha makubaliano kati ya Tanzania na Poland yaliyofanyika mwezi Oktoba 2015, ambapo Poland ilikubali kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 110. Makubaliano hayo yatawekwa saini baina ya Shirika la Maendeleo la Taifa kwa upande wa Tanzania na kampuni ya URSUS ya Poland.  Kati ya fedha hizo, kiasi cha Dola za Marekani milioni 55 zitatumika kwa ajili ya uanzishaji kiwanda cha kuunganisha matrekta hapa nchini yanayotengenezwa na kampuni hiyo. Chini ya makubaliano hayo kampuni hiyo itafundisha vijana wetu kuunganisha na kutengeneza matrekta. Aidha, kiasi cha Dola za Marekani Milioni 55 kitatumika kwa ajili ya ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mazao. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa utekelezaji wa miradi hii miwili utaanza hivi karibuni.

35.   Mheshimiwa Spika, katika suala zima la utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo katika Diplomasia ya Uchumi, Tanzania itaendelea kujenga mahusiano ya karibu na mashirika mbalimbali ya kimataifa kama vile Benki ya Dunia; mashirika yasiyo ya kiserikali yenye nguvu za kiuchumi na kisiasa; na makampuni ya kimataifa ya mafuta, nishati, mawasiliano na miundombinu ili kupata mitaji na teknolojia inayohitajika nchini kwetu.

Kusimamia Mikataba na Makubaliano ya Kimataifa

36.   Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara iliratibu na kusimamia uwekwaji saini wa mikataba ifuatayo:-

(a)      Hati za Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali za Sri – Lanka,  Serbia, Ghana, Malta, Qatar, Kuwait na Morocco kuhusu masuala ya Usafiri wa Anga yaliyotiwa saini mwezi Oktoba, 2015;
(b)      Hati ya Makubaliano kati ya Wizara na Taasisi ya Maendeleo ya Miundombinu kuhusu kuendeleza viwanja na nyumba zinazomilikiwa na Serikali nje ya nchi, uliowekwa saini tarehe 08 Desemba, 2015 – Dar es Salaam;

(c)      Mkataba wa Uenyeji kati ya Tanzania na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kuhusu Makao Makuu ya Kamisheni ya Kiswahili ya Jumuiya ya Afrika ya Mashariki yaliyoko Zanzibar. Mkataba huo uliwekwa saini tarehe 28 Desemba, 2015; na


(d)      Mkataba wa Ushirikiano kati ya Tanzania na Ufalme wa Saudi Arabia katika nyanja za uchumi, biashara, uwekezaji, michezo na vijana uliosainiwa tarehe 24 Machi, 2016.


37.     Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kufuatilia utekelezaji wa mikataba hiyo ili kusimamia maslahi ya nchi.

Kuratibu Masuala ya Uhusiano baina ya Tanzania na nchi mbalimbali, Ushirikiano wa Kimataifa, Bara la Afrika na Kikanda


Ushirikiano wa Kimataifa

Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030
38.   Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 utakumbukwa sana na Jumuiya ya Kimataifa kutokana na makubaliano na maamuzi muhimu ya kimataifa yaliyofikiwa. Miongoni mwa makubaliano hayo ni kupitishwa kwa Ajenda Mpya ya Maendeleo  kwenye Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika New York, Marekani mwezi Septemba, 2015. Katika Mkutano huo, viongozi hao walikubaliana kuwa na dira mpya ya maendeleo ya dunia ijulikanayo kama Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya mwaka 2030 yenye jumla ya Malengo 17 na shabaha 169. Ajenda hii mpya ya maendeleo endelevu inarithi Malengo ya Maendeleo ya Milenia ya miaka 15 yaliyomalizika mwaka 2015.

39.   Mheshimiwa Spika, malengo hayo yamejikita katika kutokomeza umaskini; kuhifadhi mazingira; kupambana na mabadiliko ya tabianchi; na kushirikisha makundi yote kwenye jamii katika masuala ya maendeleo. Ninajivunia kuwa Tanzania ilitoa mchango mkubwa sana katika ngazi mbalimbali kipindi chote cha majadiliano yaliyopelekea kupatikana kwa malengo hayo na hivyo kuhakikisha kuwa vipaumbele vya nchi vinakuwepo kwenye Ajenda hiyo mpya ya Maendeleo. Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi 30 zilizounda Kikundi Kazi kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu ambacho ndicho kilichopendekeza malengo hayo.

40.   Mheshimiwa Spika, utekelezaji wa Malengo hayo umeanza rasmi mwezi Januari mwaka huu na napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa malengo hayo yameshaingizwa kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi ili kuendana na vipaumbele vyetu hasa Mpango wa Pili wa  Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/2017 - 2020/2021) uliowasilishwa kwenye Bunge lako Mwezi Aprili 2016 na Waziri wa Fedha na Mipango.

41.   Mheshimiwa Spika,  inazidi kubainika katika Jumuiya ya Kimataifa kuwa moja ya vikwazo vikubwa vya maendeleo ni rushwa na ufisadi.  Uongozi wa Awamu ya Tano umezidi kutambulika duniani na kusifiwa kwa ujasiri wa kupambana na janga la rushwa.  Tanzania ilikuwa moja ya nchi na mashirika makubwa 40 duniani yaliyokaribishwa na Mheshimiwa David Cameroon, Waziri Mkuu wa Uingereza kushiriki Mkutano uliojadili juu ya mkakati mpya wa pamoja duniani wa kupambana na rushwa. Mkutano huo ulifanyika London, Uingereza mwezi Mei, 2016 ambapo Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alimwakilisha Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.  Katika Mkutano huo, Mheshimiwa Majaliwa alipata nafasi ya kufafanua hatua mbalimbali za kisiasa, kisheria na utawala ambazo Serikali ya Tanzania inachukua katika kupambana na tatizo hilo sugu la rushwa na pia kuonyesha ushirikiano wa kitaifa katika kuimarisha juhudi hizo.

Usimamizi wa Amani Duniani

42.   Mheshimiwa Spika, miongoni mwa masuala yanayoiletea heshima kubwa nchi yetu ni suala la ulinzi na utetezi wa amani na usalama kwenye ukanda wetu na sehemu mbalimbali duniani. Hadi sasa Tanzania imepeleka askari, wanawake kwa wanaume zaidi ya 2,328 kwenye misheni saba tofauti za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na bado tunaendelea kufanya hivyo. Tunayafanya yote haya kwa kuwa tunaamini amani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa binadamu. Pia, tunatimiza wajibu wetu kama sehemu ya Jumuiya ya Kimataifa katika kuhakikisha kuwa dunia inakuwa sehemu nzuri na salama ya kuishi.

43.   Mheshimiwa Spika, Taifa linajivunia sana Askari wetu wanaofanya kazi hizo za kulinda amani kwani pamoja na kushambuliwa mara kadhaa, wamekuwa wakiifanya kazi hiyo kwa umahiri, kujitoa, bidii na weledi mkubwa. Ndiyo maana haishangazi kuona Watanzania mbalimbali wakiwa wanateuliwa kushika nyadhifa za juu kwenye misheni hizo za kulinda amani. Ninatoa pongezi za pekee kwa askari wetu wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Polisi na raia walioshiriki kwa vipindi mbalimbali katika vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika.

44.   Mheshimiwa Spika, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na askari hawa wazalendo, hivi karibuni tumepokea tuhuma kwamba baadhi ya askari wetu wamehusika kudhalilisha kijinsia wanawake huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Tanzania ilizichukulia tuhuma hizi kwa uzito mkubwa sana na iliunda timu ya uchunguzi kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania ndani ya siku tano badala ya siku kumi zinazotakiwa na Umoja wa Mataifa baada ya Nchi husika kupokea taarifa za tuhuma. Tuhuma hizi zimeisikitisha sana Serikali na endapo zitathibitika hatua kali za kinidhamu dhidi ya wale wote waliohusika zitachukuliwa. Ili kuhakikisha kuwa vitendo kama hivyo vinaepukwa siku zijazo, Tanzania itajiunga na kusimamia kikamilifu “Kigali Principles” ambazo ni mwongozo wa jumla kwa nchi zinazopeleka askari wa kulinda amani kwenye vikosi vya Umoja wa Mataifa.

45.   Mheshimiwa Spika, maendeleo ya kisayansi na teknolojia yamesababisha kuongezeka kwa hali ya uhatarishi kutokana na mbinu za kiuhalifu zinazotumiwa na wahalifu wenye mitandao ya kimataifa. Mathalan, tumeshuhudia ongezeko la tishio la ugaidi Afrika Mashariki, biashara haramu ya dawa za kulevya, uvuvi haramu katika Bahari ya Hindi na mzunguko wa silaha ndogondogo. Wizara yangu kupitia Jumuiya za Kikanda na Kimataifa na ushirikiano tulionao na nchi zilizondelea, tunaratibu jitihada za kitaifa za kukabiliana na uhalifu wa kimataifa. Kwa mfano, kupitia Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi Wanachama wa SADC uliofanyika Gaborone, Botswana mwezi Agosti, 2015 Nchi Wanachama zilikubaliana kuandaa Mkakati wa SADC wa kukabiliana na Ugaidi, Mkakati wa SADC wa kukabiliana na ujangili na Mkakati wa SADC wa kukabiliana na uzagaaji wa silaha ndogondogo.

46.   Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza jitihada za kupambana na uharamia baharini, Wizara iliratibu ushiriki wa Serikali katika Mkutano wa Tatu wa Majadiliano ya Bahari ya Hindi uliofanyika mwezi Machi, 2016 nchini Indonesia. Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo ulijadili changamoto zinazoukabili Ukanda huo ikiwemo vitendo vya uharamia, uhalifu wa kutumia silaha, usafirishaji haramu na ugaidi wa majini ambavyo vinaathiri maendeleo ya uchumi. Kutokana na kuwepo kwa changamoto hizo, Mkutano ulifikia Makubaliano yajulikanayo kama Padang Consensus yanayozitaka Nchi Wanachama kuandaa mikakati mbalimbali kwa kutumia sheria za kimataifa zilizopo katika kupambana na vitendo hivyo haramu. Tanzania imejipanga kutekeleza makubaliano hayo kupitia Kamati ya Kitaifa ya Usalama Majini iliyo chini ya Uenyekiti wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu.


47.   Mheshimiwa Spika, Tanzania ni mhanga wa biashara haramu ya silaha ndogondogo kutokana na kuzungukwa na nchi zenye machafuko hasa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu. Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikichukua hatua madhubuti za kukabiliana na changamoto hiyo ikiwemo kutunga sheria na kanuni za kudhibiti biashara hiyo haramu; kuweka alama silaha zinapoingizwa nchini na kuzisajili; na kuchoma silaha haramu. Jitihada hizi pia zinafanyika kimataifa ikiwemo kusaini mikataba mbalimbali kama vile Mkataba wa Kimataifa wa Kudhibiti Biashara ya Silaha. Aidha, jitihada hizi zinapewa nguvu zaidi na lengo la 16 la Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu ambalo linazitaka nchi kupunguza ufadhili na usambazaji haramu wa silaha ndogondogo ifikapo mwaka 2030.

Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi wa Paris

48.      Mheshimiwa Spika, katika miaka ya hivi karibuni tumekuwa mashuhuda wa athari za mabadiliko ya Tabianchi yanayosababisha kuwepo kwa ongezeko la ukame; mvua nyingi zinazoleta mafuriko; kuzama kwa baadhi ya visiwa; vimbunga na tufani kubwa; kupotea kwa baadhi ya mimea na wanyama na kuongezeka kwa kina cha bahari. Hali hii sio tu inapoteza maisha ya binadamu wengi na mali zao, bali pia inaturudisha nyuma kwenye jitihada zetu za maendeleo na kutokomeza umaskini. Ni kwa msingi huo, Tanzania kama ilivyo nchi nyingi zinazoendelea imeunga mkono kupatikana kwa Mkataba mpya unaolenga kudhibiti mabadiliko ya tabianchi. Mkataba huo ulikubaliwa wakati wa Mkutano wa 21 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Paris, Ufaransa mwishoni mwa mwaka 2015. Mkataba huo tofauti na mingine iliyopita una mamlaka ya kisheria kuzibana nchi zilizoendelea na zenye viwanda vingi kupunguza gesijoto.

49.      Mheshimiwa Spika, Mkataba huo uliokubaliwa na nchi zote, ulitiwa saini tarehe 22 Aprili, 2016 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York na nchi 175 zikiwemo zile kubwa ambazo zilikuwa zikipinga Mikataba iliyopita. Tanzania ilikuwa ni miongoni mwa nchi zilizotia saini Mkataba huo. Naomba nichukue fursa hii kuzisihi nchi zote hasa zile zilizoendelea na zinazotoa gesijoto kwa wingi kuheshimu makubaliano hayo ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuitunza dunia yetu kwa manufaaa ya vizazi vya sasa na vijavyo. Aidha, ninawaasa Watanzania wote kulinda misitu yetu, uoto asilia na wanyamapori wetu kwa manufaa ya Taifa letu.

50.      Mheshimiwa Spika, sitaweza kuhitimisha hoja hii ya Mkataba wa Paris bila  kumpongeza binti wa Kitanzania, Getrude Clement, mwenye umri wa miaka 16 ambaye alipata nafasi ya kulihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa niaba ya vijana duniani wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba huo. Ninaona fahari kuwa nafasi hiyo alipewa mtoto wa Kitanzania miongoni mwa vijana wengi duniani kutokana na uwezo mkubwa alionao. Binti huyo ameliletea heshima Taifa na napenda kutumia nafasi hii kuwasihi watoto na vijana wengine hapa nchini kuweka jitihada kwenye masomo na shughuli zao wanazozifanya ili siku moja nao wapate nafasi kama hizi na kupeperusha vizuri bendera ya Taifa. Mtoto huyu awe mfano kwa kizazi kipya cha Watanzania ambao watakuwa makini katika kulinda urithi wa mazingira yetu.
Uteuzi wa Watanzania kwenye Mashirika na Taasisi za Kimataifa

51.  Mheshimiwa Spika, kutokana na mahusiano mazuri tuliyonayo na nchi nyingine, Watanzania wameendelea kupewa nafasi muhimu kwenye mashirika na taasisi za kimataifa. Suala linalozidi kuipa sifa nchi yetu na kuthibitisha imani iliyowekwa na Jumuiya ya Kimataifa kwa nchi hii na watu wake.

52.   Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa mwezi Februari 2016, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa na Bw. Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuwa mmoja wa wajumbe wa Jopo la Ngazi za juu la kumshauri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Masuala ya Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi. Aidha, mwezi Januari 2016, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Umoja wa Afrika kwenye utatuzi wa mgogoro wa Libya. Uteuzi wa Mhe. Kikwete unalenga kusaidia juhudi za Umoja wa Afrika katika kurejesha amani na utulivu nchini Libya kwa kutumia uzoefu wake. Pia katika mwezi huo wa Januari, Mhe. Kikwete, alichaguliwa kuwa Mwenyekiti mwenza wa Jopo la Watu Mashuhuri la Umoja wa Mataifa lenye jukumu la kutoa mwongozo wa agenda ya kina mama na watoto wakati huu wa mpito kutoka Malengo ya Milenia kwenda Malengo ya Maendeleo Endelevu.

53. Mheshimiwa Spika, uteuzi haukuishia tu kwa viongozi hawa wa Kitaifa, Watanzania wengine pia wameendelea kuchaguliwa na kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali kubwa kwenye Mashirika na Taasisi za Kimataifa. Hawa ni pamoja na Dkt. Agnes Kijazi, Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani; Bw. Gabriel Rugalema ambaye ameteuliwa kuwa Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani nchini Sierra Leone; Profesa Kennedy Gastorn ambaye ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Kitivo cha Sheria, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Mashauriano ya Masuala ya Kisheria katika nchi za Asia na Afrika nafasi ambayo ataanza kuitumikia mwezi Agosti 2016; na Balozi Wilfred Ngirwa alichaguliwa kuendelea na nafasi yake ya Mwenyekiti Huru wa Baraza la Shirika la Chakula na Kilimo Duniani. Pia, Bw. Donatius Kamamba, alichaguliwa kuwa Mjumbe kwenye Kamati ya Urithi wa Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni na Dk. Frannie Leautier alichaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Kuratibu Masuala ya Ushirikiano Barani Afrika

Umoja wa Afrika

54.   Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Ubalozi wetu wa Addis Ababa, Ethiopia, imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania katika shughuli mbalimbali za Umoja wa Afrika. Mwezi Januari 2016, Tanzania ilishiriki kwenye Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo. Kaulimbiu ya mkutano huo ilikuwa ni “Mwaka wa Haki za Binadamu Afrika, hususan Haki za Wanawake”. Wakati wa uzinduzi wa kaulimbiu hiyo, Nchi Wanachama zilihimizwa kuridhia na kutekeleza Itifaki na sera mbalimbali zilizoundwa na Umoja huo kwa lengo la kulinda, kukuza na kutekeleza haki za wanawake Afrika. Itifaki hizo ni pamoja na Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu na Sera ya Umoja wa Afrika kuhusu Masuala ya Jinsia. Mkutano huo pamoja na masuala mengine pia ulijadili ripoti ya Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu hali ya amani na usalama Barani Afrika.

55.   Mheshimiwa Spika, mwezi Novemba, 2015 Tanzania iliteuliwa na Umoja wa Afrika kusimamia uzinduzi wa Jeshi la Pamoja la Afrika la Kulinda Amani Barani Afrika.  Mimi mwenyewe nilisimamia uzinduzi huo. Tanzania vilevile iliendelea kutoa mchango wake katika kutafuta suluhu ya migogoro barani Afrika. Tanzania ikiwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ilieleza hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kutatua mgogoro wa Burundi. Mchango wa Tanzania katika Umoja wa Afrika kuhusu mgogoro wa Burundi kwa kiasi kikubwa uliweza kusaidia Umoja huo kuwa na taswira mpya ya namna ya kutafuta suluhu ya kudumu ikiwemo kutoa kipaumbele katika mazungumzo yanayohusisha pande zinazohasimiana nchini Burundi chini ya usimamizi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki badala ya uamuzi wa awali wa kupeleka majeshi ya Umoja huo nchini Burundi.

56.   Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Tanzania ilichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kwa vipindi viwili mfululizo kuanzia mwaka 2012 hadi mwezi Januari, 2016. Hii inatokana na mchango wake mkubwa katika kusuluhisha migogoro barani Afrika. Katika uchaguzi wa wajumbe wapya wa Baraza hilo uliofanyika mwezi Januari 2016, Kenya, Rwanda na Uganda zilichaguliwa kuwakilisha ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano kati ya Afrika na India

57.   Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu ushiriki wa Tanzania kwenye Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano kati ya Afrika na India, uliofanyika New Delhi, India mwezi Oktoba, 2015. Katika Mkutano huo, pamoja na masuala mengine, India iliahidi kuisaidia Afrika katika kuendeleza miundombinu; umwagiliaji; kuongeza thamani ya rasilimali; kuanzisha viwanda; na teknolojia ya habari na mawasiliano. Aidha, Serikali ya India iliahidi kutoa mkopo wenye masharti nafuu wa Dola za Marekani bilioni 10, ruzuku ya misaada ya Dola za Marekani milioni 600 na kuchangia Dola za Marekani milioni 100 kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo. Vilevile, India iliahidi kutoa nafasi 50,000 za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Afrika nchini India kwa miaka mitano ijayo. Ili kunufaika na fursa hizi, nchi za Afrika zinatakiwa kuwasilisha andiko la miradi mbalimbali ya vipaumbele kwa Serikali ya India.


58.   Mheshimiwa Spika,  napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba kufuatia mkutano huo, tayari Serikali imeandaa na kuwasilisha miradi ya kipaumbele ikiwemo miradi 17 ya maji pamoja na Mradi wa Serikali Mtandao. Aidha, miradi mingine itakayowasilishwa ni pamoja na mradi wa ujenzi wa atamizi kwa ajili ya viwanda vidogo na  vya kati katika kila mkoa; mradi wa ujenzi wa reli itakayotumika kusafirisha abiria katika Jiji la Dar es Salaam; na mradi wa kilimo cha umwagiliaji – Zanzibar.

Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika 

59.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki Mkutano wa Sita wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwezi Desemba 2015, Jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Katika mkutano huo Serikali ya China ilitangaza mpango mpya wa miaka mitatu kuanzia 2016 hadi 2018 wa ushirikiano kati ya China na Afrika ambao umeweka kipaumbele katika kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika. Tanzania ni miongoni mwa nchi nne za mfano zilizochaguliwa na China kwa ajili ya kujenga viwanda vya mfano. Nchi nyingine zilizomo kwenye mpango huo ni Afrika Kusini, Ethiopia na Kenya.

60.   Mheshimiwa Spika, kupitia Mpango huo, Serikali ya China imetangaza kutenga Dola za Marekani bilioni 10 kwa ajili ya kuendeleza sekta ya viwanda barani Afrika. Aidha, China itatoa nafasi 40,000 za mafunzo ya kuwajengea waafrika stadi za ufundi nchini China na nafasi  200,000 kwenye nchi zao; kutuma wataalam wa China katika nchi za Afrika kwa ajili ya kutoa ushauri wa namna ya kutekeleza programu ya viwanda; na kujenga vyuo vya ufundi vya kikanda kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa wafanyakazi wa viwandani.

61.   Mheshimiwa Spika,  ili kunufaika na Mpango huo, Serikali ya Tanzania imebainisha na kuwasilisha miradi ya kipaumbele ambayo ni Ujenzi wa Reli ya Kati katika kiwango cha kimataifa; ujenzi wa miundombinu wezeshi ya reli, barabara, kina cha bandari, umeme, gesi na maji katika Ukanda Maalum wa Uchumi wa Bagamoyo; Ujenzi wa mtandao wa kusambaza gesi katika mikoa ya Dar es Salaam, Mtwara, Lindi na Pwani (Bagamoyo na Mkuranga); Upanuzi wa Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume – Zanzibar; na Ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri – Zanzibar.

Kuratibu Masuala ya Ushirikiano wa Kikanda

Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu 

Mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu.

62.   Mheshimiwa Spika,  katika kipindi hiki Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Mawaziri wa Sheria wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu uliofanyika Livingstone, Zambia mwezi Agosti, 2015. Mkutano huo ulipokea taarifa kutoka Nchi Wanachama kuhusu hatua zilizofikiwa katika kuridhia na kutekeleza Itifaki za Jumuiya ya nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu hususan Itifaki nne zinazopewa kipaumbele katika utekelezaji wake kwa sasa. Itifaki hizo ni; Itifaki ya Ushirikiano wa Kiulinzi; Itifaki ya Ushirikiano wa Kimahakama; Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu wa Maliasili na Itifaki ya Kuzuia Unyanyasaji wa Kijinsia dhidi ya Wanawake na Watoto. Mkutano huo ulibaini itifaki hizo hazijatekelezwa kikamilifu na nchi zote wananchama. Hivyo, nchi wanachama zilikubaliana kutekeleza itifaki hizo kikamilifu.

63.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Itifaki hizo Serikali imechukua hatua mbalimbali zikiwemo kutunga Sheria ya kudhibiti uhalifu wa njia ya mawasiliano; Sheria ya kurudishiana wahalifu waliokimbilia nchi nyingine; kuanzisha vitengo maalum katika viwanja vya ndege vya Kimataifa nchini ili kudhibiti usafirishaji holela wa Maliasili; kuanzisha Mpango wa Mataifa wa kuwalinda wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji wa kujinsia na kuanzisha kitengo maalum katika vituo vya polisi Wilaya zote nchini kushughulikia kesi za uonevu wa kijinsia.

64.   Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu ushiriki wa wataalamu wa Tanzania katika Mkutano wa Jumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu uliofanyika Luanda, Angola mwezi Januari, 2016. Miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa katika Mkutano huo  ni kutathmini  hali ya ulinzi  na usalama katika  nchi za  eneo la Ukanda wa Maziwa Makuu  hususan katika nchi za Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Sudan Kusini. Pamoja na mambo mengine Jumuiya hiyo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Taasisi za Kikanda katika kuratibu shughuli za kutatua migogoro. Kwa mfano, mgogoro wa Burundi kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki, mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kushirikiana na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika pamoja na  mgogoro wa Sudan Kusini kwa kushirikiana na Jumuiya ya Ushirikiano wa Maendeleo ya Nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika.

65.   Mheshimiwa Spika, Jumuiya hiyo ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu ambayo Tanzania ni mwanachama inatambua uhusiano mkubwa uliopo kati ya uvunaji haramu wa rasilimali na kushamiri kwa migogoro. Hivyo, nchi wanachama zimesaini Itifaki ya Ulinzi, Usalama na Maendeleo pamoja na Itifaki ya Kupinga Uvunaji Haramu wa Rasilimali ambazo kwa pamoja zinazitaka nchi zote 12 wanachama kutii taratibu zinazotambulika kikanda za uvunaji rasilimali ambapo Cheti ya Kikanda cha kuthibitisha uvunaji huo hutolewa. Hii kwa kiasi kikubwa imesaidia kudhibiti makundi ya waasi kujipatia fedha kwa njia za uvunaji haramu wa rasilimali kwa lengo la kufadhili shughuli zao.

66.    Mheshimiwa Spika, jitihada hizo za pamoja zimepelekea kutengamaa kwa hali ya ulinzi na usalama katika nchi za maziwa makuu. Kwa mfano, idadi ya wakimbizi wanaoingia nchini imepungua kutoka kati ya wakimbizi 200 hadi 300 kwa siku kwa mwezi Novemba, 2015 hadi kufikia wakimbizi kati ya 100 hadi 120 kwa siku kwa mwezi Mei, 2016. Hadi sasa Tanzania inahifadhi jumla ya wakimbizi 136,000 kutoka Burundi na wengine 2,360 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Bado idadi hii ni kubwa na Serikali inaendelea kushirikiana na wadau wengine katika jitihada za kutatua migogoro katika ukanda wetu wa Maziwa Makuu ili hatimaye wakimbizi hao waweze kurejea nchini mwao.

Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika

Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika

67.  Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika uliofanyika mwezi Agosti 2015 Gaborone, Botswana. Mkutano huo ulijadili masuala ya siasa, uchumi, uwekezaji, kijamii, ulinzi na usalama katika Kanda.

68.  Mheshimiwa Spika, pamoja na Mkutano huo kuiteua Tanzania kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya hiyo, Nchi Wanachama  ziliazimia  yafuatayo:-

             i.        Serikali ya Lesotho pamoja na washirika wengine wa kisiasa nchini humo kuandaa mapema iwezekanavyo mpango wa utekelezaji wa mabadiliko ya Katiba na Sekta ya Ulinzi;

           ii.        Kuhakikisha kuwa kunakuwepo na ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika nafasi mbalimbali za maamuzi ya juu Serikalini na sekta binafsi;

          iii.        Kutekeleza kikamilifu Sera ya Kilimo ya Kanda na Itifaki zingine ili kusaidia kuongeza kasi ya uzalishaji, biashara na ushindani katika sekta ya kilimo; na

          iv.        Sekretariati kufuatilia kwa karibu kwa kushirikiana na Nchi Wanachama kuhakikisha UKIMWI na magonjwa mengine ya kuambukiza hayaendelei kuwa tishio kwenye Sekta ya Afya katika Kanda.

69.   Mheshimiwa Spika, kutokana na nchi yetu kujijengea sifa ya umahiri na weledi katika masuala ya siasa, ulinzi na usalama barani Afrika na katika Kanda, katika mkutano huo, Tanzania iliteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Asasi ya SADC ya Siasa, Ulinzi na Usalama kwa kipindi cha mwaka 2015/2016. Kutokana na uteuzi huo, Tanzania kwa mara nyingine itakuwa Mwenyekiti wa Asasi hiyo katika kipindi cha Agosti 2016 hadi Agosti 2017 ikiwa ni mara ya tatu kupewa wadhifa huo. Uteuzi huu unaonyesha imani ya wanachama wa SADC waliyonayo kwa Tanzania katika kutatua migogoro na kusimamia amani katika kanda hiyo na unaendelea kuijengea nchi yetu heshima kubwa na kuiweka juu katika medani za Kikanda na Kimataifa.

Mkutano wa dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wanaosimamia Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama

70.     Mheshimiwa Spika, Tanzania ilishiriki kwenye Mkutano wa Dharura wa Viongozi Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wanaosimamia Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama uliofanyika Gaborone, Botswana tarehe 18 Januari, 2016 kwa ajili ya kujadili hali ya kisiasa nchini Lesotho. Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huo uliongozwa na Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pamoja na mambo mengine, Mkutano huo uliielekeza Serikali ya Jamhuri ya Lesotho kuitoa kwa umma ripoti ya Tume Huru ya Uchunguzi ya SADC na kuhakikisha kuwa inatekeleza kwa uadilifu mapendekezo yaliyomo katika taarifa hiyo ili kuboresha hali ya siasa, ulinzi na usalama nchini humo. Vilevile, Viongozi Wakuu walisisitiza umuhimu wa kusimamia kwa dhati utekelezaji wa Mikataba yote mitatu ya amani iliyosainiwa kwa ajili ya kurejesha amani nchini humo. Taarifa ya utekelezaji wa mapendekezo yaliyomo katika ripoti hiyo itawasilishwa kwenye Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliopangwa kufanyika mwezi Agosti, 2016 Mbabane, Swaziland.

Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika

71.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ambao ulifanyika Gaborone, Botswana mwezi Machi, 2016. Pamoja na masuala mengine, Mkutano huo ulijadili hatua ya utekelezaji ya Mpango wa Kikanda wa Maendeleo 2015 - 2020; hatua ya utekelezaji wa Mpango wa Kikanda wa Maendeleo ya Viwanda; na Mtangamano wa Utatu wa Eneo Huru la Biashara la COMESA-EAC-SADC. Mkutano huo pia ulipokea taarifa ya utekelezaji wa maamuzi ya vikao vya Baraza la Mawaziri ambayo ilihusisha jumla ya maeneo kumi. Taarifa hiyo inaonyesha kuwa utekelezaji wa maeneo hayo unaendelea vizuri.

72.   Mheshimiwa Spika, Mkutano huo pia, ulipokea maombi ya Serikali ya Visiwa vya Comoro na Serikali ya Burundi ya kutaka kujiunga na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika. Hivi sasa Sekretarieti inaendelea na zoezi la kutathmini maombi ya nchi hizo kulingana na taratibu, kanuni na sheria za Jumuiya za kuwa mwanachama. Taarifa ya tathmini hiyo itatolewa kwenye Mkutano wa 36 wa Wakuu wa Nchi ambao umepangwa kufanyika mwezi Agosti, 2016, Mbabane, Swaziland.

Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi

73.   Mheshimiwa Spika, Tanzania imeendelea kuwa mwanachama wa mstari wa mbele katika kuimarisha ushirikiano wa nchi zilizo katika mwambao wa Bahari ya Hindi kupitia Jumuiya ya Nchi hizo.
Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri kuhusu ‘Blue Economy’
74.   Mheshimiwa Spika, Wizara ilishiriki katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi kuhusu Blue Economy uliofanyika mwezi Septemba, 2015 nchini Mauritius. Mkutano huo ulijadili maeneo manne ya kipaumbele kuhusu matumizi endelevu ya rasilimali zitokanazo na bahari.  Maeneo hayo ni Fisheries and Aquaculture; Renewable Ocean Energy; Seaport and Shipping; na Seabed Exploration and Minerals. Mkutano huo pia ulidhamiria kuunda mifumo madhubuti yenye Sera, Sheria na Mikakati ya Matumizi Endelevu ya Rasilimali za Bahari na kusimamia Dhana ya Uchumi wa Bahari ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo endelevu kwa Nchi Wanachama.

75.   Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza maazimio ya mkutano huo, Mamlaka ya Kusimamia Uvuvi wa Bahari Kuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania inaendelea kufanya utafiti wa kutambua maeneo yenye samaki wengi hususan aina ya Jodari pamoja na majaribio ya kuweka vifaa vya kuvutia samaki katika Bahari ya Hindi. Utafiti huu unaohusisha maeneo ya Mafia, Zanzibar na Bagamoyo unalenga kuwapunguzia wavuvi muda wa kutafuta samaki, kupunguza gharama za mafuta na kuwaongezea kipato. Vilevile, taarifa za utafiti huo zitatolewa kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi ili waje kuwekeza katika uvuvi wa Bahari Kuu ya Tanzania.

Kulinda na kuendeleza Maslahi ya Taifa ya Kiuchumi na Mengineyo nje ya nchi

Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
76.     Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa 70 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika New York, Marekani, mwezi Septemba, 2015 ambapo Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipata nafasi ya kulihutubia Baraza hilo na kueleza msimamo wa nchi kwenye masuala mbalimbali duniani, yakiwemo ya kiuchumi na maendeleo, amani na usalama, pamoja na mahusiano yetu na nchi nyingine. Aidha, Mheshimiwa Kikwete alifanya mazungumzo na nchi marafiki na washirika wetu wa maendeleo na kukubaliana masuala mbalimbali yenye manufaa kwa nchi ikiwemo ufadhili wa miradi ya maendeleo.

Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola
77.     Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola uliofanyika Malta mwezi Novemba, 2015. Tanzania ilishiriki kikamilifu kwenye majadiliano mbalimbali yaliyofanyika na hivyo tamko la mwisho ya mkutano liliakisi maslahi ya nchi hususan kwenye masuala ya amani na usalama; haki za binadamu na utawala bora; maendeleo endelevu; mabadiliko ya tabianchi; biashara na usawa wa kijinsia na kumwezesha Mwanamke.

78.     Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza baada ya miaka 66, Jumuiya ya Madola ilimchagua mwanamke mwenye asili ya Afrika, Mheshimiwa Baroness Patricia Scotland mzaliwa wa Dominica na mwenye uraia pacha wa Dominica na Uingereza kuwa Katibu Mkuu wa sita wa Jumuiya hiyo ambapo alianza kazi tarehe 1 Aprili, 2016. Vipaumbele alivyoainisha Mheshimiwa Scotland ni pamoja na kushughulikia unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto wa kike; athari za mabadiliko ya Tabianchi; biashara na utawala bora; na kuanzisha majadiliano na nchi wanachama kuhusu kutokufanya suala la mahusiano/mapenzi ya jinsia moja kuwa kosa la jinai.  Alisisitiza kuwa nchi haziwezi kulazimishwa kufuata suala hili lakini ataanzisha majadiliano na lazima pawepo na makubalino ya pande zote. Wizara itaendelea kufuatilia kwa makini ajenda zake ili kuhakikisha masuala ambayo yanapingana na sheria, mila na desturi za nchi yetu hayawi sehemu ya majadilino ya Jumuiya.

Mkutano wa 10 wa Nchi Wanachama wa Shirika la Biashara Duniani
79.     Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu na kushiriki kwenye Mkutano wa 10 wa Mawaziri wa Nchi Wanachama wa Shirika la Biashara Duniani uliofanyika mwezi Desemba 2015, Nairobi, Kenya. Katika Mkutano huo Tanzania ilitetea maslahi yake hasa kuhusu masuala ya biashara ya kilimo na mazao yake ikiwemo pamba kwa kushirikiana na makundi ya Afrika; Nchi Masikini zaidi Duniani; Kundi la 77 na China; na Kundi la Afrika, Karibiani na Pasifiki, hivyo kuwa na ushawishi kwenye matokeo ya Mkutano huo yanayojulikana kama Nairobi Package. Makubaliano yaliyofikiwa kwenye Mkutano huo ni pamoja na nchi zilizoendelea kusitisha ruzuku ya kuuza nje mazao ya kilimo na kuimarisha soko kwa nchi zinazoendelea. Makubaliano haya ni muhimu zaidi kuwahi kufanyika ndani ya miaka 20 ya uhai wa Shirika hilo.

Ushiriki wa Watanzania waishio Ughaibuni katika Maendeleo ya Nchi
80.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea na juhudi za kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora wa Tanzania waishio maeneo mbalimbali duniani katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu. Jitihada hizo zimeleta mafanikio katika nyanja za uwekezaji, biashara na kubadilishana uzoefu, elimu na ujuzi. Diaspora waliopo katika nchi mbalimbali kama vile, Australia, Botswana, Marekani, Oman na Thailand wamekuwa mstari wa mbele katika kutafuta fursa za biashara, elimu pamoja kuutangaza utalii wa nchi yetu. Kwa mujibu wa takwimu zilizokusanywa kupitia Balozi zetu, Watanzania waishio nje ya nchi wanakadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja kote duniani. Kitaaluma wapo Wahandisi, Madaktari, Wachumi, Wahadhiri na Wakufunzi katika nyanja mbalimbali na pia wafanyabishara; ambao wote hawa wametawanyika sehemu mbalimbali duniani.

81.     Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika Kongamano la Pili la Diaspora lililofanyika Jijini Dar es Salaam mwezi Agosti, 2015. Lengo la Kongamano hilo lilikuwa ni kuhamasisha Diaspora kushiriki katika kukuza sekta ya biashara ndogondogo na za kati na kuboresha mahusiano kati ya Diaspora na Wajasiriamali waliopo nchini. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu makongamano mengine ya kibiashara na uwekezaji yanayofanyika nje ya nchi kama yale yanayoandaliwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Marekani.

82.     Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara ya kitabibu ya Madaktari Watanzania kwa kushirikiana na madaktari wenzao wa kiafrika waishio nchini Marekani mwezi Julai 2015. Madaktari hao walitoa huduma za matibabu na ushauri katika hospitali za Mwananyamala (Dar es Salaam) na Mnazi Mmoja (Zanzibar) kwa magonjwa ya moyo, saratani na kinywa. Aidha, walitoa msaada wa madawa na vifaa tiba vyenye thamani ya Dola za Marekani 300,000 kwenye hospitali hizo na kukabidhi mashine ya kupima saratani ya matiti yenye thamani ya Dola za Marekani 200,000 katika Hospitali ya Lugalo.

83.     Mheshimiwa Spika, naomba kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru madaktari hao kwa moyo wao wa dhati wa kujitolea. Aidha, ningependa kuwahamasisha Diaspora wengine kuiga mifano hiyo. Wizara yangu iko tayari kushirikiana nao wakati wote.

84.     Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kuitikia wito wa kuchangia maendeleo ya nchi yetu, uwekezaji wa Diaspora katika Benki ya CRDB, Mfuko wa Pensheni wa PSPF na Mfuko wa Mitaji wa UTT umefikia Shilingi Bilioni 26 mwaka 2015.  Aidha, uwekezaji wa Diaspora katika mifuko mingine ya hifadhi za jamii, sekta za afya, viwanda na utalii umeongezeka. 

85.     Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kwamba tunaweka mazingira wezeshi kwa Diaspora, Wizara yangu imekamilisha hatua za awali za kutengeneza Sera ya Diaspora kwa ushirikiano na Mfuko wa Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki. Sera hii itatoa mwongozo kwa wadau na kuleta uelewa wa pamoja kuhusu mikakati bora ya kuwatambua Diaspora na kuwawezesha kuchangia maendeleo ya nchi. Rasimu ya Sera hiyo itawasilishwa kwa wadau kwa ajili ya maoni na ushauri. Ni matarajio ya Serikali kuwa ushirikishwaji wa Diaspora kama moja ya wadau wa maendeleo utawawezesha kuchangia katika maendeleo ya nchi yetu kwa kuleta teknolojia mpya; na kuongeza uwekezaji kwenye sekta mbalimbali kama vile viwanda, masoko ya mitaji, kilimo na utalii. Ushirikishwaji huo wa Diaspora utaiwezesha nchi kufikia malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

86.     Mheshimiwa Spika, Wizara kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania na wadau wengine inaandaa  mfumo sahihi wa kutambua na kurahisisha uingiaji wa fedha kutoka kwa Diaspora ili kuwa na takwimu sahihi za mchango wa Diaspora kwenye kuongeza Pato la Taifa.

Kusimamia masuala yanayohusu Kinga na Haki za Kibalozi kwa Wanadiplomasia waliopo nchini kulingana na Mkataba wa Vienna wa mwaka 1961

87.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kushirikiana na mamlaka mbalimbali nchini ili kuhakikisha kuwa, jamii ya wanadiplomasia waliopo nchini wanapata haki zao kama ilivyoainishwa katika Mkataba wa Vienna Kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia wa mwaka 1961. Wizara inasimamia kikamilifu utekelezaji wa Mkataba huo kwenye vipengele muhimu  vya kinga na haki za kibalozi na wategemezi wao. Pamoja na jamii ya kibalozi kuwa na kinga na upendeleo maalum, Wizara inahakikisha kuwa jamii hizi zinaheshimu na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi yetu.


88.   Mheshimiwa Spika, mara baada ya kuundwa kwa Serikali ya Awamu ya Tano, nilikutana na Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa waliopo nchini. Kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, nilitumia fursa hiyo kuwapatia taarifa ya masuala mbalimbali yanayohusu umuhimu wa ushirikiano wa Tanzania na nchi nyingine na kutoa Dira ya Serikali ya Awamu ya Tano. Wizara yangu itaendelea kuwa na vikao vya mara kwa mara na wanadiplomasia hawa kwa lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano.

89.   Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Nne nje ya nchi ambao ni  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Makamu wa pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Baadhi ya ziara za Viongozi hao zilifanywa katika nchi za Uswisi, Australia, Marekani, Misri, India, Kenya, Uganda, Botswana, Vietnam, Uingereza na Italia. Vilevile, Wizara iliratibu ziara za Viongozi wa Kitaifa wa Awamu ya Tano nje ya nchi zilizofanyika katika nchi za Afrika Kusini, Botswana, Ethiopia, Rwanda, Uganda, Uingereza Zambia, Comoro na Papua New Guinea.

90.   Mheshimiwa Spika, ziara hizo zimekuwa na mafanikio ikiwa ni pamoja na kukuza na kuimarisha mahusiano kati ya nchi yetu na nchi hizo, zimetangaza fursa za uwekezaji, biashara, utalii na kuwahamasisha Diaspora kuwekeza nyumbani. Pia zinaimarisha uhusiano kati ya sekta binafsi za hapa nchini  na taasisi mbalimbali za nje.

91.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu na kufanikisha uwasilishaji wa hati za utambulisho za Mabalozi kutoka nchi mbalimbali. Katika kipindi hiki Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho ni pamoja na Qutar, Argentina, India, Denmark, Uswisi, Uturuki, Finland, Sweeden, Ubelgiji, Hispania, Msumbiji, Uganda, Misri, Israeli, Ufilipino, Jamhuri ya Korea, Umoja wa Ulaya, Palestina, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Jamhuri ya Namibia, Brazil, Jamhuri ya Czech na Jamhuri ya Sudan Kusini.

Kuanzisha na Kusimamia Huduma za Kikonseli

92.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwa kurahisisha upatikanaji wa viza kwa maafisa na watendaji wa Serikali, Vyama vya Siasa na Taasisi nyingine zinazostahili huduma hiyo. Aidha, Wizara imeendelea kuratibu matumizi ya Ukumbi wa Watu Mashuhuri wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, kwa watu wanaostahili wakiwemo Mabalozi na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa, viongozi wa Serikali na baadhi ya Wafanyabiashara hapa nchini. Vilevile, Balozi zetu nje zimeendelea kutoa Viza kwa raia wa nje wanaoitembelea Tanzania na kushirikiana na mamlaka nyingine kutafuta ufumbuzi wa matatizo mbalimbali yanayowakabili Watanzania waishio nje ya nchi.

93.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kulinda maslahi ya Watanzania wanaofanya kazi kwenye Balozi mbalimbali na Mashirika ya Kimataifa hapa nchini. Katika kutekeleza jukumu hilo, Wizara yangu imebaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali ikiwemo baadhi ya Watanzania wanaofanya kazi katika Balozi na mashirika hayo kutokuwa na mikataba ya ajira. Hivyo, natoa rai kwa ofisi za Kibalozi na Mashirika ya Kimataifa yaliyopo hapa nchini kutoa mikataba kwa waajiriwa wao ili kukidhi matakwa ya kisheria. Vilevile, nawaasa Watanzania wanaofanya kazi katika Balozi na Mashirika ya Kimataifa wahakikishe wana mikataba ya ajira ili kulinda maslahi yao.

94.   Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutoa huduma za kikonseli kwa Watanzania waliopo nje ya nchi. Naomba  kutumia fursa hii kuwasihi Watanzania hao kuhakikisha wanajisajili katika Balozi zetu na Konseli, na pale ambapo hatuna ofisi za ubalozi wajisajili katika ofisi za ubalozi wa Uingereza kama ilivyoainishwa kwenye hati za kusafiria.

95.   Mheshimiwa Spika, niruhusu nitumie fursa hii kuliarifu Bunge lako Tukufu na Watanzania kwa ujumla kwamba miaka ya karibuni pamejitokeza wimbi la Watanzania wanaokwenda nje ya nchi kwa ahadi za kupatiwa ajira. Kwa upande wa India, Thailand, Malaysia na China, ahadi hizo za ajira zimekuwa zikitolewa na watu wasio waaminifu ambao wana mtandao wa biashara ya kusafirisha binadamu. Mtandao huo unahusisha raia wa Tanzania waliopo ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na raia wa kigeni waliopo kwenye nchi hizo.  Watu hao wanachofanya ni pamoja na kuwatafuta wasichana wenye umri kati ya miaka 18 na 24, kuwatafutia vibali vya safari na kuwalipia nauli za kuwafikisha kwenye nchi husika kwa kuwalaghai kuwa wanakwenda kufanya kazi katika hoteli, migahawa, maduka makubwa au kazi za nyumbani. Matokeo yake, wanapofika kwenye nchi hizo wasichana hao wanakuta kuwa ahadi walizo ahidiwa sio za kweli na badala yake wanalazimishwa kukubali kufanya kazi za ukahaba ili kurejesha fedha walizogharimiwa kufika huko. Kwa taarifa tulizonazo, mtandao huo wa biashara ya ukahaba huwataka wasichana hao kurejesha kiasi cha Dola za Marekani kati ya 5,000 hadi 6,000 kiasi ambacho sio rahisi kupata kwa kazi hizo ikizingatiwa kwamba mapatano na malipo ya kazi hiyo hayafanywi na wahusika bali madalali wa mtandao huo. Madalali waliowapeleka vijana hao kwenye nchi hizo huwanyang’anya hati zao za kusafiiria ili kuwadhibiti wasitoroke hadi kipatikane kiasi cha fedha walizogharimwa.   Kwa kuwa hawana fedha na namna nyingine ya kuishi wasichana hao wamelazimika kukubali kufanya biashara hiyo.

96.     Mheshimiwa Spika, baadhi ya vijana hao, waliweza kuwatoroka madalali hao, na kukimbilia kwenye ofisi zetu za Ubalozi kutafuta msaada.  Kwa bahati mbaya Mheshimiwa Spika, Balozi zetu hazina fungu la kuhudumia Watanzania wanaopata shida ughaibuni na matokeo yake maafisa wa Ubalozi kwa moyo wa kibinadamu wamekuwa wakitoa fedha zao wenyewe kusaidia kununua tiketi za kuwarejesha Watanzania waliofanikiwa kuchomoka kwenye makucha ya makuadi wa ukahaba. Katika jitihada za kukabiliana na tatizo hilo, Wizara imeanzisha mazungumzo na Shirika la Kimataifa la Uhamaji ili wasaidie kuwarudisha nyumbani vijana hao.

97.       Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba vitendo hivyo ni vya kinyama na vinakiuka haki ya binadamu. Ifahamike pia kwamba usafirishaji wa binadamu ni uhalifu kwa mujibu wa makosa ya kupangwa ya Azimio la Umoja wa Mataifa NA. 55/25 la mwaka 2003 la kuzuia, kukomesha na kuadhibu usafirishaji wa binadamu hasa kwa wanawake na watoto chini ya Itifaki yake.

98.       Mheshimiwa Spika, Kutokana na ushirikiano kutoka kwa Jumuiya za Watanzania waishio nchini Thailand na India, pamoja na baadhi ya wahanga wa biashara hiyo haramu, Serikali imepata majina ya baadhi ya wahusika  wa mtandao huo na tayari mawasiliano na Serikali za nchi hizo yamefanyika ili kuwakamata wahusika wote na kuwafikisha katika mkondo wa sheria.  Kwa hapa nyumbani, uchunguzi unaendelea kwa kushirikiana na Balozi za nchi ambazo wasichana wetu wanapelekwa ili kubaini watu wote walio sehemu ya mtandao huo hususan wale wanaowezesha upatikanaji wa vibali vya kusafiria kwenye Balozi hizo ili kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria. Pia tumeziomba Balozi hizo ziwe makini zaidi kudhibiti uombaji wa vibali vya kusafiria kwa shughuli mbalimbali na kuwataka wahusika kuthibitisha uwezo wa kifedha zitakazo wawezesha kutalii, kufanya shughuli ama kuishi katika nchi wanazokwenda ili kuudhibiti mtandao wa biashara ya watu.

99.       Mheshimiwa Spika, Vilevile, kupitia Bunge hili, ninatoa wito kwa Watanzania wote, tuwe makini pale tunapopata fursa za kazi nje ya nchi.  Kama nilivyosema hapo awali, ni muhimu kuzingatia na kujiridhisha na masuala  yote ya msingi yanayohusiana na ajira za nje, ikiwa ni pamoja na; kuwepo  na mkataba rasmi wa ajira unaotambuliwa na Mamlaka husika zilizopo nchini na za Nchi unayotaka kwenda, kujisajili kweye ofisi za Ubalozi wa Tanzania uliopo katika nchi hizo na kutokubali kuweka hati yako ya kusafiria kama rehani.
100.    Mheshimiwa Spika, nasikitika kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa bado kuna Watanzania kadhaa wanatumikia vifungo na wengine kati yao wanakabiliwa na adhabu ya kifo katika magereza ya nchi mbalimbali duniani baada ya kukutwa na hatia ya makosa ya kujihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya. Idadi yao ni kama ifuatavyo: Brazil (41), China (266), Iran (68), India (9), Nepal (4), Oman (3), Thailand (14) na Umoja wa Falme za Kiarabu (3). Naomba kuchukua nafasi hii kuwasihi Watanzania kujiepusha na biashara hiyo kwa kuwa hasara zake ni kubwa kwa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Kuratibu shughuli za Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano

101.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu Mikutano ya Tume za Pamoja za Kudumu za Ushirikiano ambazo kimsingi hutoa fursa kwa nchi zetu kujadiliana kwa kina kuhusu masuala muhimu katika nyanja zote za mahusiano na kuweka mikakati ya pamoja ya maendeleo.

102.     Mheshimiwa Spika, mwezi Februari 2016, Wizara ilifanya kikao cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia kilichofanyika hapa nchini. Katika kikao hicho, pande zote mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano katika masuala ya Ulinzi na Usalama Mipakani; kuanzisha Mashauriano ya Kidiplomasia; Kupunguza Msongamano wa magari katika mpaka wa Tunduma/Nakonde; na kuanzisha majadiliano ya kutotoza kodi mara mbili kwenye bidhaa zinazotoka na kuingia katika nchi hizo.

103.     Mheshimiwa Spika, Vilevile, mwezi Aprili 2016, Wizara iliratibu na kushiriki kwenye Kikao kingine cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyika Mjini Gisenyi, Rwanda. Katika kikao hicho nchi hizi zimekubaliana kushirikiana katika kukamilisha mapema ujenzi wa miundombinu ya ushoroba wa kati kama vile ujenzi wa reli ya kati katika kiwango cha kimataifa kwa kushirikiana na wadau, kukuza ushirikiano katika sekta ya anga hususan baina ya Shirika la Ndege la Rwanda na Shirika la Ndege la Tanzania, kuimarisha ushirikiano katika sekta za sayansi na teknolojia, afya, kilimo, ufugaji, utalii na elimu. Mkutano huo umezidi kuimarisha urafiki na ushirikiano kati ya Tanzania na Rwanda kufuatia ziara ya kirafiki ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Rwanda mwezi Aprili, 2016.

104.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeratibu na kushiriki vikao vya Ujirani Mwema kati ya Tanzania na nchi za Msumbiji, Uganda na Zambia. Vikao hivyo ni muhimu katika kukuza mahusiano katika sekta mbalimbali kati ya Tanzania na nchi husika. Aidha, Vikao hivyo vinasaidia kutatua matatizo mengi ya mpakani na kurasimisha biashara baina ya nchi yetu na nchi tunazoshirikiana nazo.  

Kusimamia utawala na Maendeleo ya Utumishi Wizarani na kwenye Balozi zetu

105.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Wizara iliajiri watumishi 42, ambapo maafisa 30 kati ya hao walipelekwa katika mafunzo maalum ya Jeshi la Kujenga Taifa yenye lengo la kuwajengea uwezo, uadilifu na uzalendo katika kazi; mtumishi mmoja alibadilishwa kada; iliwapandisha vyeo watumishi 59; na iliwathibitisha kazini watumishi 15. Aidha, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa, katika kipindi hiki ulifanyika uteuzi wa mabalozi kuiwakilisha nchi yetu katika nchi za Uholanzi, Malawi, Kuwait, Japan, Uingereza na Zimbabwe. Vilevile, Wizara imejaza nafasi za Wakurugenzi zilizokuwa wazi.
106.    Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza mpango wa mafunzo wa miaka mitatu 2013/2014 - 2015/2016.  Katika kipindi hiki jumla ya watumishi 43 walihudhuria mafunzo ndani na nje ya nchi. Kati ya hao, Watumishi 24 walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi 19 walihudhuria mafunzo ya muda mfupi. Wizara imeshaanza kuandaa mpango mwingine wa mafunzo wa miaka mitatu ambao utaanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai 2016 baada ya mpango wa sasa kuisha muda wake mwezi Juni 2016.

107.    Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Wizara imewarejesha nyumbani Mabalozi watano na watumishi tisa baada ya kustaafu na wengine kumaliza muda wao wa kufanya kazi Ubalozini. Aidha, Wizara iliwapeleka vituoni Naibu Mabalozi watatu na watumishi thelathini. Zoezi la kuwarudisha Mabalozi na watumishi wanaostaafu na wanaomaliza muda wao na kupeleka mbadala wao ni endelevu na Wizara itaendelea kulitekeleza kadri inavyopata fedha.

TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA


108.     Mheshimiwa Spika, Wizara yangu inasimamia taasisi tatu ambazo ni Chuo cha Diplomasia kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam, Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika na Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha, ambacho pia kinasimamia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam.

Chuo cha Diplomasia


109.     Mheshimiwa Spika, Chuo kimeendelea kutekeleza majukumu yake ya kutoa mafunzo, kufanya tafiti, kutoa ushauri wa kitaaluma na kendesha kozi fupi kwenye nyanja za diplomasia na uhusiano wa kimataifa. Katika kutekeleza jukumu hilo, Chuo kimejizatiti katika kutimiza na kutekeleza viwango vilivyowekwa na Baraza la Taifa la Ithibati la Mafunzo ya Ufundi linalosimamia elimu ya mafunzo na ufundi kama vile kuwa na wanataaluma wenye vigezo vinavyotambulika, kuboresha shughuli za kitaaluma, kuboresha majengo na miundombinu ya kitaaluma pamoja na matumizi ya teknolojia katika taaluma na utawala.

Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha


110.     Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha unaoishia Juni 2015, Kituo kiliweza kuwa mwenyeji wa mikutano 150 ya kitaifa na 57 ya kimataifa iliyoingiza nchini wageni wanaokadiriwa kufikia 35,288. Aidha, hadi kufikia tarehe 31 Machi, 2016 kituo kimeweza kuwa mwenyeji wa Mikutano 82 ambapo 10 ni ya Kimataifa na 72 ya kitaifa.

111.     Mheshimiwa Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kwa mara nyingine tena, Kituo kimeendelea kupata hati safi ya hesabu zake zilizoandaliwa na kukaguliwa kwa wakati kwa kipindi kilichoishia tarehe 30 Juni, 2015.

112.     Mheshimiwa Spika, Katika mwaka wa fedha 2016/2017, Kituo kimepanga kuingiza mapato ya shilingi 15,778,162,803.00 kutokana na vyanzo vyake mbalimbali vya mapato ikiwemo Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kilichopo Dar es Salaam ambacho kinatarajiwa kukusanya mapato ya Shilingi 3,051,000,000.00.

113.     Mheshimiwa Spika, Kituo kinategemea kukopa shilingi bilioni 2.4 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ujenzi wa jengo la maonesho na upanuzi wa Hospitali. Miradi yote inayotekelezwa imeombewa kibali cha Msajili wa Hazina.

114.     Mheshimiwa Spika, Kituo kinaendelea kufanya taratibu za kuwezesha kujengwa kituo mahsusi cha mikutano kitakachoitwa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mlima Kilimanjaro. Taarifa ya upembuzi yakinifu ya mradi wa ujenzi wa Kituo hicho iliandaliwa na Wataalamu Washauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.  Taarifa hiyo ilionyesha kwamba mradi huo ni muhimu na wenye manufaa kiuchumi na kijamii kwa taifa. Aidha, makadirio ya awali ya ujenzi wa kituo hicho ni Dola za marekani milioni 248. Kwa hivi sasa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha kinaendelea na mazungumzo na mifuko ya hifadhi ya jamii iliyopo nchini ili iweze kushiriki katika kutekeleza mradi huo. Ni matarajio ya Wizara kuwa kuwepo kwa Kituo hicho kutakuwa suluhisho sahihi la mahitaji ya mikutano ya kimataifa na maonesho hapa nchini.

Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika


115.     Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania wenye lengo la kuzisaidia nchi za Kiafrika kuhakikisha kuwa changamoto zinageuzwa kuwa fursa za maendeleo na mambo mazuri ya kuendelezwa kwa faida ya nchi yenyewe na hata kuwa mfano wa kuigwa na nchi nyingine. Mpango huo unaratibiwa kwa mujibu wa miongozo ya Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Afrika.

116.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwaka wa fedha 2015/2016, Taasisi ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania imeendelea kutekeleza shughuli zifuatazo:-

        i.        Kusimamia utekelezaji wa Mpango kazi wa kuondoa changamoto za utawala bora zilizobainishwa kwenye ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania. Taasisi imeendelea kupokea na kuchambua taarifa mbalimbali za utekelezaji kutoka Wizara, Idara na Wakala wa Serikali zilizoguswa na Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania;

      ii.        Kuandaa taarifa ya utekelezaji ya mwaka kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kutatua changamoto zilizojitokeza kwenye ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania. Taarifa hiyo inatarajiwa kuwasilishwa kwenye vikao vya Wakuu wa Nchi za Kiafrika wanaoshiriki kwenye mchakato wa Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika;

    iii.        Kuendelea kutoa taarifa kwa wananchi juu ya matokeo ya tathmini ya utawala bora kwa nchi yetu kupitia vyombo mbalimbali vya habari na majukwaa mengineyo; na

     iv.        Kutafsiri ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Barani Afrika kwa upande wa Tanzania katika lugha ya Kiswahili na kuandaa chapisho la muhtasari.

ILIYOKUWA WIZARA YA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI


117.      Mheshimiwa Spika, baada ya kuelezea utekelezaji wa majukumu ya iliyokuwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, naomba sasa nilieleze Bunge lako Tukufu utekelezaji wa majukumu ya iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Wizara hiyo ilikuwa na majukumu yafuatayo:-

        i.        Kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Itifaki zake;
      ii.        Kuratibu, kushiriki na kusimamia utekelezaji wa Mtangamano wa Afrika Mashariki hususan majadiliano na utekelezaji wa hatua za Mtangamano ambazo ni Umoja wa Forodha; Soko la Pamoja; Umoja wa Fedha; na Shirikisho la Kisiasa;
    iii.        Kutoa elimu ya Mtangamano wa Afrika Mashariki ili Wananchi waweze kuelewa na kutumia fursa za Mtangamano huo; na
     iv.        Kuimarisha utendaji na kujenga uwezo wa Wizara.

118.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016 Wizara hiyo iliidhinishiwa Shilingi 26,666,436,300.00. Kati ya fedha hizo, Shilingi 24,047,468,300.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na Shilingi 2,618,968,000.00 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi. Kiasi kilichotengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo  kimejumuisha mchango wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki wa kiasi cha Shilingi 18,570,055,300.00.

119.      Mheshimiwa Spika, hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2016, Wizara ilipokea jumla ya Shilingi 19,003,440,860.00, sawa na asilimia 71.26 ya fedha zote zilizotengwa. Kati ya fedha hizo Shilingi 15,506,375,000 zilitumika kulipa mchango wa Tanzania kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki, Shilingi 1,689,936,160.00 zilitumika kulipa mishahara ya watumishi na Shilingi 1,807,129,700.00 zilitumika kutekeleza shughuli za Wizara.


120.  Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepiga hatua kubwa ambapo Nchi wanachama wa Jumuiya zimefikia makubaliano na kuendelea kuyatekeleza makubaliano hayo kwenye nyanja zote za kiuchumu, kijamii, kiutamaduni na kwa kiasi fulani kisiasa pia na hivyo kutufanya tusilale na kutakiwa kuwa makini katika kila hatua tunazopiga. Itakumbukwa kuwa Jumuiya yetu ilianzishwa rasmi Julai 2000 baada ya Nchi Wanachama kukamilisha kuridhia Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliotiwa saini na Wakuu wa Nchi Wanachama tarehe 30 Novemba, 1999. Aidha, hivi sasa Nchi zote Wanachama zinatekeleza Mkataba huu na Itifaki zake kubwa tatu (3) na zile mbalimbali za kisekta. Maeneo yaliyobaki ambayo tunaendelea na majadiliano ni Umoja wa Fedha na Shirikisho la Kisiasa.

121.  Mheshimiwa Spika,  juhudi hizi sasa zinamaanisha kuwa eneo lote la nchi sita (6) za Jumuiya ya Afrika Mashariki kimsingi limeungana katika nyanja mbalimbali na hivyo kutoa motisha ya ushindani mkubwa wa ndani ya Jumuiya kiuchumi na kimaendeleo. Kwa kutambua kuwa Tanzania ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kupitia Wizara yangu ameelekeza Wimbo na Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki zitumike hapa nchini.

122.  Mheshimiwa Spika,  napenda kuchukua nafasi hii kupitia Bunge lako Tukufu kutoa wito wa kuongezwa kwa matumizi ya Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwenye  Ofisi zote za Umma nchini zikiwemo za Serikali Kuu, Serikali za Mitaa na Taasisi za Umma (tukiwemo sisi Waheshimiwa Wabunge kwenye Magari yetu na ofisi zetu Majimboni) na zile za sekta binafsi sambamba na Bendera ya Taifa letu Tukufu. Aidha, natoa rai kwa Taasisi za Serikali na vyombo vya habari viweze kuutumia Wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pale ambapo Wimbo wa Taifa letu Tukufu unapigwa.

123.  Mheshimiwa Spika,  ni imani yangu kuwa hatua hii itasaidia kuwajengea Watanzania uelewa, kuifahamu vyema Jumuiya yetu na hatimae waweze kujiandaa, kushiriki na kupata manufaa yanayoendana na fursa zilizopo kibiashara, kiuchumi, kiuzalishaji, kijamii na kiutamaduni kwa kuzingatia uwepo wa Soko kubwa la Afrika Mashariki na fursa zinginezo.

124.  Mheshimiwa Spika,  wito huu ni moja ya utekelezaji wa Mkakati wetu wa mawasiliano wa Wizara ambao unalenga kuwapa fursa Wananchi wetu ya kujiandaa, kuiendesha, kuitumia Jumuiya yao na kutimiza matakwa ya Ibara ya 7(a) ya Mkataba wa Uanzishaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo inasisitiza kuwa “Jumuiya yetu hii imejengwa katika Wananchi na ushirikiano wa kimasoko”. Aidha, hatua hizi zinalenga katika kuendeleza juhudi za Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kuhakikisha kuwa Jumuiya hii inakuwa kweli ni Jumuiya ya Wananchi wetu, kutambua uwepo wake na wanufaike nayo katika kubadilisha maisha yao.

Mkutano wa 17 wa Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama na Mikutano ya 32 na 33 ya Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki

125.     Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki Wizara iliratibu na kushiriki katika Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Machi 2016 Jijini Arusha, Tanzania. Katika Mkutano huo Tanzania iliteuliwa kwa mara ya pili mfululizo kuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hadi mwezi Novemba 2016. Aidha, Mkutano huo uliridhia Jamhuri ya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo tarehe 15 Aprili, 2016 nchi hiyo ilisaini Mkataba wa Kujiunga na Jumuiya hiyo.

126.     Mheshimiwa Spika, kadhalika, katika mkutano huo Wakuu wa Nchi walizindua rasmi Pasi mpya ya kielektroniki ya Kusafiria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kuelekeza matumizi ya hati hii mpya kuanza rasmi tarehe 1 Januari, 2017. Pasi hii inaipandisha hadhi Pasi ya sasa ya Afrika Mashariki kutumika kusafiria nje ya Afrika Mashariki. Nchi Wanachama zimekubaliana kuziondoa hati za kusafiria zilizopo sasa katika kipindi cha miezi 24 kuanzia tarehe 1 Januari, 2017 hadi tarehe 31 Desemba, 2018. Hati hizo zitakuwa na alama za jumla za kiusalama na kila Nchi Mwanachama imeruhusiwa kuongeza alama zake za kiusalama katika Pasi hizo. Idara za Uhamiaji katika nchi wanachama zitaendelea na jukumu la utoaji wa hati hizo kwa raia wa nchi zao.

127.      Mheshimiwa Spika, Mkutano wa 32 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki ulifanyika tarehe 14 Agosti, 2015 na kufikia maamuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuidhinisha ajira kwa Mwanasheria Mkuu wa Jumuiya, Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usalama wa Anga na Mkurugenzi wa Mipango katika Jumuiya.

Umoja wa Forodha

128.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa hatua ya kwanza ya Mtangamano ambayo ni Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki kama ifuatavyo:

Kanuni Mpya za Utambuzi wa Uasili wa Bidhaa
129.      Mheshimiwa Spika, katika kuziwezesha Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kunufaika zaidi na hatua hii ya Umoja wa Forodha, mabadiliko yamefanywa katika kanuni za utambuzi wa uasili wa bidhaa. Katika mabadiliko hayo, Nchi Wanachama zimeacha kutumia vigezo sawa kwa bidhaa zote,  na sasa zitatumia vigezo tofauti kulingana na bidhaa husika. Mabadiliko haya ni fursa kubwa kwa viwanda vya Tanzania ambavyo vingi bado ni vidogo na vilikuwa haviwezi kufikia vigezo vya uasili wa bidhaa. Aidha, katika kipindi hiki, nchi Wanachama wa Jumuiya zilikamilisha mwongozo wa kutumika katika kurahisisha utekelezaji wa kanuni hizo.

Uondoaji wa  Vikwazo Visivyo vya Kiforodha
130.      Mheshimiwa Spika, katika kuweka mazingira wezeshi ya biashara katika Jumuiya, Wizara imeendelea kuratibu uondoaji wa Vikwazo Visivyo vya Kiforodha kupitia Kamati ya Kitaifa na  Kikanda ya uondoaji wa vikwazo hivyo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 vikwazo 16 viliripotiwa vimeondolewa, kati ya hivyo vinne (4) viliihusu Tanzania. Vikwazo hivyo ni tozo ya Dola za Marekani 200 kwa kila kontena la kemikali; kutopewa upendeleo wa ushuru wa forodha kwa chumvi na bidhaa za plastiki kutoka Kenya; na upimaji wa malori matupu.

131.      Mheshimiwa Spika, ili kuharakisha uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha, Wizara imekuwa na utaratibu wa kuitisha mikutano ya pande mbili husika. Katika kipindi hiki Wizara ilifanya mikutano na Kenya na Burundi ambayo ilichangia kuharakisha uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha vikiwemo vile vilivyotajwa hapo juu. Vilevile, tumekubaliana na Kenya kufanya utafiti juu ya tozo zinazotozwa na mamlaka za Serikali za mitaa za nchi zetu zinazoathiri biashara baina yetu kwa lengo la kurazinisha tozo hizo.

Mwenendo wa Biashara ya Bidhaa kati ya Tanzania na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

132.      Mheshimiwa Spika, nafasi ya Tanzania katika Soko la Jumuiya imeendelea kupanda kutoka asilimia 18 mwaka 2010 hadi asilimia 26 mwaka 2014 na tunategemea kufanya vizuri zaidi kutokana na juhudi zinazoendelea za kudhibiti ulanguzi wa mazao na bidhaa mipakani, utekelezaji wa sheria mpya ya uasili wa bidhaa, kuondoa vikwazo visivyo vya kiforodha na kuimarisha uzalishaji viwandani. Kwa mujibu wa Taarifa ya Biashara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya mwaka 2014, biashara ndani ya Jumuiya imekua na kufikia Dola za Marekani bilioni 5.63 kwa mwaka 2014 ikilinganishwa na Dola za Marekani bilioni 3.72 kwa mwaka 2010. Aidha, biashara baina ya Tanzania na Nchi Wanachama imeendelea kuimarika na kuongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 0.69 mwaka 2010 na kufikia Dola za Marekani bilioni 1.49 mwaka 2014. Kwa mwaka 2013 kiwango cha biashara kiliongezeka zaidi kulingana na hali ya mahitaji ya soko na kupanda kwa uzalishaji kwenye sekta mbalimbali. Tanzania imeendelea kuwa na urari chanya wa biashara katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kama inavyoonekana katika Kiambatisho Na. 1.

133.      Mheshimiwa Spika, wafanyabiashara wa Tanzania wamendelea kuchangamkia fursa zitokanazo na Umoja wa Forodha wa Afrika Mashariki. Wafanyabiashara hao wamefanikiwa kuuza kwa wingi katika Soko la Afrika Mashariki bidhaa za viwandani kama vile transfoma, waya za umeme, vyandarua, saruji na magunia; na bidhaa za kilimo kama vile mahindi, mchele, katani, mbogamboga, asali na chakula cha mifugo. Hii inaashiria kuendelea kuimarika kwa biashara ya bidhaa za viwandani na mazao ya kilimo.

134.      Mheshimiwa Spika, bidhaa zilizonunuliwa kwa wingi kutoka Nchi Wanachama ni pamoja na kemikali kwa ajili ya viwanda vya nguo, vipodozi na sabuni; dawa za binadamu na mifugo; vipuri vya magari; vifuniko vya chupa za vinywaji; sabuni; vifaa vya kufanyia usafi; vifungashio; mabanda maalum ya kilimo cha mbogamboga na maua (green house); na vyumba vya baridi kwa ajili ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali.

 Umoja wa Fedha

135.      Mheshimiwa Spika, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeendelea kutekeleza Mpangokazi wa Miaka Kumi wa Kuelekea katika Eneo la Sarafu Moja ulioanza kutekelezwa mwaka 2014 na utakaokamilika mwaka 2024. Katika kutekeleza Mpangokazi huo, Nchi Wanachama zimekamilisha majadiliano ya Muswada wa Sheria ya uanzishwaji wa Taasisi ya Fedha ya Afrika Mashariki na Taasisi ya Takwimu ya Afrika Mashariki. Maandalizi ya majadiliano ya muswada wa Kamisheni ya Ufuatiliaji na Usimamizi ya Afrika Mashariki yataanza katika kipindi hiki cha mwaka wa fedha.

136.      Mheshimiwa Spika, matarajio ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ni kuifikia hatua hii muhimu ya kuanzisha matumizi ya sarafu moja kwenye eneo la Jumuiya ifikapo mwaka 2024. Hatua hii itafikiwa mara baada ya Nchi Wanachama angalau watatu (3) kufikia vigezo vya kiuchumi vilivyoainishwa kwenye Itifaki ya Umoja wa Fedha. Aidha, hatua hiyo itatanguliwa na uanzishwaji wa Benki Kuu ya Afrika Mashariki ambayo pamoja na majukumu mengine itakuwa na majukumu ya kuchapisha na kusambaza sarafu hiyo ya Afrika Mashariki.

Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki
137.      Mheshimiwa Spika, Shirikisho la Kisiasa ni hatua ya nne na ya mwisho katika mtangamano wa Afrika Mashariki ambayo inategemea sana misingi imara itokanayo na utekelezaji wa hatua za mwanzo za mtangamano. Katika kipindi cha mwaka fedha 2015/2016, Nchi Wanachama ziliendelea na majadiliano ya modeli ya shirikisho ambayo itatumika katika kuandaa Rasimu ya Katiba ya Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.

138.      Mheshimiwa Spika, rasimu hiyo, inatarajiwa kutumika katika kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa Afrika Mashariki kuhusu aina ya Shirikisho linalotarajiwa kuundwa ili kuleta uelewa wa pamoja na uungwaji mkono wa hatua hiyo wakati ukifika. Aidha, kwa kuwa Shirikisho la Kisiasa ni mchakato, Nchi Wanachama zimeendelea na utekelezaji wa shughuli zinazounda msingi wa Shirikisho hilo ikiwemo masuala ya utawala bora, uimarishaji wa demokrasia na utawala wa sheria.

Ushirikiano na Kanda nyingine za Kiuchumi

Majadiliano ya Kuanzisha Eneo Huru la Biashara la Utatu wa Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika

139.     Mheshimiwa Spika, juhudi za kuziunganisha Jumuiya za COMESA, EAC na SADC ili kuwa eneo moja huru la kibiashara zimefika hatua nzuri. Mkutano wa Tatu wa Wakuu wa Nchi za COMESA, EAC na SADC uliofanyika tarehe 10 Juni, 2015 Jijini Sharm El Sheikh, Misri ulihitimishwa kwa Wakuu wa Nchi na Serikali kutia saini Azimio la Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara; na Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara.

140.    Mheshimiwa Spika, kufuatia kusainiwa kwa mkataba huo, Viongozi Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya hizo walikubaliana kukamilisha majadiliano ya maeneo yaliyosalia katika kipindi cha miezi 6 hadi 12 baada ya uzinduzi rasmi wa eneo huru la biashara. Maeneo hayo ni uondoshwaji wa kodi kwenye bidhaa, utambuzi wa uasili wa bidhaa, usuluhishi wa migogoro ya kibiashara na kupunguziana ushuru.

Majadiliano ya Uhuru wa Wafanyabiashara kusafiri katika Eneo la Utatu

141.      Mheshimiwa Spika, ili kurahisisha na kuwezesha wafanyabiashara kusafiri katika Eneo hilo la Utatu, Nchi Wanachama zimeendelea na majadiliano ya kuandaa Mkataba wa Uhuru wa Wafanyabiashara kusafiri kwenye eneo hilo. Mkataba huo unatarajiwa kuidhinishwa ifikapo Desemba, 2016.

Majadiliano ya Uendelezaji wa Viwanda katika Eneo la Utatu
142.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika kukamilisha Rasimu ya Mpango wa Maeneo ya Ushirikiano katika Maendeleo ya Viwanda; na Mpangokazi kwa ajili ya Utekelezaji wa utaratibu wa Ushirikiano katika eneo la Utatu. Maeneo yaliyoboreshwa ni Sera na Mikakati kutoka Kanda zote tatu; Uzingatiaji wa uendelezaji wa viwanda unaojali utunzaji wa mazingira; na Utambuaji Kisheria na Umiliki wa Haki zinazotokana na Uvumbuzi na Ubunifu katika maendeleo ya Viwanda. Aidha, Nchi Wanachama zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya uratibu na uhamasishaji wa pamoja wa sera ya maendeleo ya viwanda na uongezaji thamani bidhaa baina ya nchi Wanachama; na Uendelezaji wa Viwanda Vidogo na vya Kati  na kujenga uwezo  wa utaalam katika kuendeleza Viwanda.

Ubia wa Kiuchumi kati ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya

143.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu majadiliano ya Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya. Malengo ya ubia huu ni kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuleta maendeleo endelevu na kuziwezesha  nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki kupata misaada ya kimaendeleo ili kukabiliana na changamoto za uzalishaji na kuweka muda wa kuondoa vikwazo vya biashara.
144.      Mheshimiwa Spika, nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya zilikamilisha mapitio ya kisheria ya Mkataba wa Ubia wa Kiuchumi baina ya nchi hizo. Hatua inayoendelea ni Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki kutafsiri mkataba huo katika lugha ya Kiswahili wakati Umoja wa Ulaya unatafsiri mkataba huo katika lugha 21 zinazotumiwa na Jumuiya ya Ulaya. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kufanya tafsiri, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Umoja wa Ulaya zitasaini Mkataba huo, pamoja na kuuridhia ili utekelezaji wake uanze.

145.      Mheshimiwa Spika, ili kuweka mazingira wezeshi ya kukuza na kuendeleza viwanda vya nguo na ngozi ndani ya Jumuiya, Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi Wanachama ulielekeza  Nchi Wanachama kuhakikisha zinapunguza uingizaji wa nguo na viatu vilivyotumika  kutoka nje ya Jumuiya na kusitisha uagizaji  wake katika  kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu wa fedha. Aidha, Wakuu wa Nchi walielekeza Nchi wanachama kupiga marufuku utaratibu wa kuuza ngozi na bidhaa za ngozi ghafi nje ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kujengea uwezo na upatikanaji wa masoko kwa Wajasiriamali wadogo
146.      Mheshimiwa Spika, Maonesho ya 16 ya Juakali/Nguvukazi  yaliyofanyika  tarehe 30 Novemba hadi 6 Disemba 2015  katika Viwanja vya  Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam  katika maonesho hayo   jumla ya wajasiriamali 734 kutoka Nchi zote wanachama walishiriki. Kati ya hao, wajasiriamali 395 walikuwa ni washiriki kutoka Tanzania. Lengo la maonesho hayo ni kujenga uwezo wa wafanyabiashara wadogo kupata masoko ya bidhaa zao katika Nchi Wanachama. Napenda kutoa rai kwa wajasiriamali wa Tanzania kushiriki katika Maonesho ya 17 ya Juakali/Nguvukazi yaliyopangwa kufanyika mwezi Novemba 2016 nchini Kenya.

Uendelezaji wa Miundombinu ya  Kiuchumi

147.         Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu utekelezaji wa programu na miradi ya kitaifa yenye sura ya Kikanda  iliyoainishwa katika Mipango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Uendelezaji wa Miundombinu ya Kiuchumi. Hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa programu na miradi hiyo ni kama ifuatavyo:

Ujenzi wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani

148.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu ujenzi wa vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani. Hadi sasa vituo viwili (2) kati ya saba (7) vinavyojengwa kwa uratibu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki vimekamilika na kuzinduliwa. Vituo hivyo ni kituo cha Holili/Taveta mpakani mwa Tanzania na Kenya; na kituo cha Rusumo mpakani mwa Tanzania na Rwanda.

149.      Mheshimiwa Spika, vilevile, Wizara iliratibu ukamilishaji wa Kanuni za Utekelezaji wa Sheria ya Jumuiya ya Kusimamia Uendeshaji wa Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani. Kanuni hizo zimepitishwa na Mkutano wa 33 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika mwezi Februari, 2016. Ili kupata uelewa wa pamoja kuhusu Vituo vya Kutoa Huduma kwa Pamoja Mipakani, Wizara iliratibu na kushiriki katika mafunzo kwa maafisa wa Serikali, sekta binafsi na wawakilishi wa jamii kwa Vituo vya Horohoro na Sirari. Taarifa kuhusu vituo vingine na hatua zilizofikiwa ili kuwezesha kuanza kutoa huduma stahiki ni kama inavyoonesha katika Kiambatisho Na. 2.
  
150.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuratibu ukamilishaji wa ujenzi wa Daraja la Kimataifa la Rusumo ikiwa ni sehemu ya kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na kuimarisha vituo vya kutoa huduma za pamoja mipakani katika ushoroba wa kati. Daraja hilo lenye uwezo wa kupitisha magari manne kwa wakati mmoja yenye uzito wa tani 56 kila moja lilizinduliwa rasmi na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Paul Kagame, Rais wa Jamhuri ya Rwanda tarehe 6 Aprili, 2016.

Uendelezaji wa Mtandao wa Barabara

151.    Mheshimiwa Spika, hatua zilizofikiwa katika uendelezaji wa mtandao wa barabara za Kikanda katika mwaka 2015/2016 ni kama ifuatavyo:

Mradi wa Barabara ya Arusha – Holili/Taveta – Voi

152.      Mheshimiwa Spika, mradi huu unahusu uendelezaji wa mtandao wa barabara unaoziunganisha nchi za Tanzania na Kenya kupitia mpaka wa Holili/Taveta yenye urefu wa kilomita 234.3. Kwa upande wa Tanzania, awamu ya kwanza ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami unahusisha upanuzi wa sehemu ya kutoka Arusha hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1 kuwa njia nne na barabara ya  mzunguko wa kusini mwa Jiji la Arusha yenye urefu wa kilometa 42.41. Aidha, kwa upande wa Kenya mradi unahusisha ujenzi wa barabara mpya  ya lami yenye urefu wa kilomita 100 kutoka Taveta hadi Mwatate. Gharama za mradi kwa upande wa Tanzania ni takriban Shilingi  bilioni 209.61 ambapo kati ya hizo Benki ya Maendeleo ya Afrika itatoa Shilingi bilioni 190.21 na Serikali ya Tanzania itatoa Shilingi bilioni 19.4.

153.      Mheshimiwa Spika, Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Barabara hiyo liliwekwa mwezi Machi, 2016 na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya.

Uwianishaji wa Uzito wa Magari Katika Barabara

154.    Mheshimiwa Spika, Sheria ya Udhibiti wa Uzito wa Magari ya Mwaka 2013 iliyopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki imeridhiwa na Nchi zote Wanachama. Nchi Wanachama zimekamilisha majadiliano ya kuandaa Kanuni za kuwezesha utekelezaji wa Sheria hizo ambazo zilipitishwa  katika Mkutano wa 33 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya uliofanyika Jijini Arusha mwezi Februari, 2016.

Mkakati wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi

155.      Mheshimiwa Spika, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimeidhinisha utekelezaji wa Mkakati wa Kuwezesha Sekta ya Uchukuzi.  Mkakati huo unazitaka Nchi Wanachama pamoja na masuala mengine kuwianisha mitaala ya mafunzo ya udereva wa magari ya biashara; usajili wa vyombo vya moto; na madaraja ya leseni. Nchi Wanachama zimekamilisha rasimu za mitaala ya mafunzo ya udereva wa magari ya biashara.

Sekta ya Mawasiliano

156.         Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kuratibu utekelezaji wa Mpango wa Kutatua Changamoto ya Gharama Kubwa za Maunganisho ya Simu za Mkononi katika Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama ulivyoridhiwa na Wakuu wa Nchi wa Jumuiya hiyo mwezi Februari, 2015. Katika kutekeleza mpango huo, yamefanyika mapitio ya Kanuni zinazotumika katika mfumo wa kuongoza sekta ya mawasiliano nchini. Wizara ya kisekta inafanya tathmini ya  changamoto zilizoibuliwa na wadau kuhusu mpango huo.

Sekta ya Hali ya Hewa

157.      Mheshimiwa Spika, Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Ushirikiano katika Huduma za Hali ya Hewa ilisainiwa na Mawaziri wanaosimamia masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoka Nchi Wanachama katika Mkutano wa 33 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Februari, 2016. Itifaki hiyo inatoa mwongozo wa ushirikiano wa Nchi Wanachama katika kubadilishana taarifa na ujuzi katika masuala ya hali ya hewa. Nchi Wanachama zimekubaliana kuridhia Itifaki hiyo kabla ya mwezi Julai, 2016.

Sekta ya Bandari na Usafiri Majini

158.      Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kurahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi Wanachama zinaendelea na maandalizi ya Mkakati wa Usafiri wa Majini wa Afrika Mashariki.  Katika kutekeleza azma hiyo, Utafiti wa Awali wa Hali ya Usafiri wa Majini na Sekta ya Bandari umekamilika. Ripoti ya Utafiti huo, pamoja na mambo mengine, imebainisha changamoto katika utekelezaji wa miradi ya kuendeleza Bandari katika mwambao wa Bahari ya Hindi, Maziwa na Uanzishaji wa Bandari Kavu. Changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa rasilimali fedha zinazohitajika katika kutekeleza Miradi iliyoainishwa katika Mipango Mikuu  ya kuendeleza Bandari za Nchi Wanachama na haja ya kuwianisha Mifumo ya Kitaasisi na Udhibiti katika Sekta ya Usafiri wa Majini miongoni mwa Nchi Wanachama ili kuwa na viwango vinavyofanana katika udhibiti wa vyombo vya majini. Maoni ya Ripoti hiyo yatasaidia katika maandalizi ya Mkakati wa Afrika Mashariki wa Usafiri wa Majini.

Sekta ya Nishati

159.      Mheshimiwa Spika, wakati wa Mkutano wa Kilele wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Machi 2016, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Jamhuri ya Uganda walifanya Kikao cha pamoja kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na  ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda mpaka bandari ya Tanga litakalokuwa na urefu wa kilometa 1,410.

160.      Mheshimiwa Spika, kufuatia Kikao hicho  cha Marais wawili, wataalam wa pande zote mbili waliendelea na majadiliano yaliyopelekea Serikali ya Uganda kutoa tamko rasmi kwenye Mkutano wa 13 wa Ushoroba wa Kaskazini uliofanyika mwezi Aprili, 2016 Jijini Kampala kuwa bomba hilo litajengwa kupitia Tanzania. Mradi huo utagharimu Dola za Marekani bilioni nne na kukamilika baada ya miaka mitatu hadi minne. Mradi huo unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja takriban 1,500 na ajira zisizo za moja kwa moja 20,000. Aidha, Benki ya Maendeleo ya Afrika imeidhinisha msaada wa kiasi cha Dola za Marekani 1,691,130 kwa ajili ya upembuzi yakinifu wa ujenzi wa Mradi mwingine wa Bomba la Mafuta la  Mbarara - Mwanza - Isaka - Dar es Salaam. Fedha za nyongeza Dola za Marekani 95,600 zinahitajika ili kukamilisha upembuzi yakinifu huo. Hivyo, kila Nchi Mwanachama imetakiwa kuchangia kiasi cha Dola za Marekani 19,120 kabla ya mwisho wa mwezi Juni, 2016 ili kukamilisha upembuzi yakinifu wa Mradi huo.


Ushirikiano Katika Sekta za Huduma  za Jamii
Sekta ya Elimu, Utamaduni na Michezo

Urazinishaji wa Mitaala

161.      Mheshimiwa Spika, Wizara  imeendelea  na uratibu wa zoezi la urazinishaji wa Mitaala kwa ngazi zote za Elimu pamoja na mafunzo ya ualimu kwa shule za  awali,  msingi na sekondari. 

Shindano la Insha la Jumuiya

162.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika shindano la uandishi wa Insha la Jumuiya ya Afrika Mashariki lililoshirikisha wanafunzi wa shule za sekondari kutoka nchi tano (5) Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Nafurahi kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa kijana Mtanzania Simon Mollel Sabaya kutoka Shule ya Sekondari ya Mzumbe aliibuka mshindi wa kwanza katika shindano hilo. Huu ni ushahidi kuwa vijana wetu wanaweza na wanauelewa wa Jumuiya yetu. Naomba nitumie fursa hii kutoa pongezi kwa kijana huyu na kuwatia moyo vijana wengine waendelee kushiriki kwenye mashindano haya ili waweze kuliletea sifa Taifa letu.  Natoa wito kwa walimu na wazazi kuwahamasisha wanafunzi kushiriki katika shindano hilo ili kukuza uelewa wao katika masuala ya Jumuiya. Wizara yangu kwa kushirikiana na Jumuiya ya Afrika Mashariki; Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia; na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo itaanzisha kampeni ya kuongeza uelewa wa Jumuiya katika shule na vyuo.

Mdahalo wa Nne wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu
163.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu ushiriki wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Tanzania katika mdahalo wa Nne (4) wa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika mwezi Desemba 2015, Kampala, Uganda. Lengo la mdahalo huo ni kupata washindi wawili kutoka kila Nchi Mwanachama wa Jumuiya ambao watakuwa Mabalozi wa Nchi zao katika masuala ya Jumuiya. Kwa upande wa Tanzania, washindi wa mwaka 2015 ni Raphael Kambamwene wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Lucy Peter Funja wa Chuo Kikuu cha Ardhi. Aidha, Wizara inaendelea na jukumu la kuwapatia taarifa Mabalozi hao zitakazowawezesha kutoa elimu kwa umma hususan kwa vijana wenzao.

 

Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki

164.    Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba Kamisheni ya Kiswahili ya Afrika Mashariki imeshahamia rasmi katika Makao Makuu yake yaliyopo Zanzibar. Hii ni kufuatia kusainiwa kwa Mkataba wa Uenyeji baina ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki tarehe 28 Desemba, 2015.

Mradi wa Hifadhi ya Mazingira Katika Bonde la Ziwa Victoria Awamu ya Pili

165.      Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na athari za mazingira zinazotokana na shughuli za binadamu katika Bonde la Ziwa Victoria zilizosababisha pamoja na mambo mengine kupungua kwa kina cha maji na samaki katika ziwa, Wizara imeendelea na uratibu wa utekelezaji wa shughuli za Mradi wa Usimamizi wa Mazingira katika Bonde la Ziwa Victoria. Katika kipindi hiki, Benki ya Dunia iliongeza muda wa miaka miwili na nusu kuanzia mwezi Juni 2015 hadi mwezi Desemba 2017 na mkopo wa Dola za Marekani milioni 10 ambazo zitatumika kukamilisha miradi ambayo ilikuwa haijakamilika katika Awamu ya Pili ya Mradi iliyofikia ukomo wake mwezi Juni 2015 na kuandaa Awamu ya Tatu. Vilevile, udhibiti wa magugumaji katika Ziwa Victoria umeendelea ambapo magugumaji yamepungua Ziwani kutoka hekta 520 mwezi Septemba, 2009 hadi hekta 104 mwezi Novemba, 2015. Mradi umeendelea na shughuli za udhibiti wa utupaji taka na uhamasishaji wa uzalishaji bora viwandani ambapo Jumla ya viwanda 118 sawa na asilimia 86 vimepata mafunzo ya uzalishaji bora viwandani.

Programu ya Hifadhi ya Mazingira kwa Kuboresha Sera, Mabadiliko ya Tabianchi, Utafiti na Maendeleo ya Kiuchumi

166.      Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kunakuwa na matumizi endelevu ya rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara, Wizara yangu imefanikisha utiaji saini wa Hati ya Makubaliano ya Usimamizi wa pamoja wa rasilimali maji katika Bonde la Mto Mara kati ya Tanzania na Kenya. Makubaliano hayo yatasaidia kupunguza athari za mazingira zinazosababishwa na shughuli za binadamu katika bonde hilo.

Mradi wa Idadi ya Watu, Afya na Mazingira wa Jumuiya

167.      Mheshimiwa Spika, ili kujenga uelewa wa pamoja kwa wananchi katika masuala ya idadi ya watu, afya na mazingira kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu, Wizara imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania katika maandalizi ya Mpango Mkakati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Masuala ya Idadi ya Watu, Afya na Mazingira. Mpango huo utakapokamilika utatoa mwongozo wa kuzingatia masuala ya idadi ya watu, afya na mazingira katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Nchi Wanachama.
Sekta ya Jinsia na Maendeleo ya Jamii

168.      Mheshimiwa Spika, nafasi ya wanawake, watoto na vijana imeendelea kupewa kipaumbele katika Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kwa muktadha huo, Wizara imeendelea kuratibu programu na miradi inayolenga kuyajengea uwezo makundi hayo ili kunufaika na fursa mbalimbali zinatokanazo na Mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Aidha, progamu hizi zimetoa fursa kwa makundi  hayo kutoa maoni yao ya namna bora ya kuendeleza mtangamano. Vilevile, Jumuiya ya Afrika Mashariki inakamilisha Sera ya Watoto ya Jumuiya.


Ushirikiano katika Siasa, Ulinzi na Usalama

169.      Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepata Katibu Mkuu mpya Balozi Liberat Mfumukeko kutoka Jamhuri ya Burundi atakeyeiongoza Jumuiya kwa Kipindi cha miaka mitano ijayo. Aidha, naomba kumshukuru Balozi Dkt. Richard Sezibera kutoka Jamhuri ya Rwanda kwa mchango wake mkubwa katika kuiendesha Jumuiya kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Ushirikiano katika Siasa
170.      Mheshimiwa Spika, katika kipindi hiki tumeendelea kushuhudia kushamiri kwa demokrasia katika Nchi Wanachama wa Jumuiya. Kwa kuzingatia kwamba demokrasia ni moja ya misingi mikuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Wizara yangu  imeendelea kuratibu ushiriki wa Tanzania  katika timu ya waangalizi wa uchaguzi mkuu kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi mkuu katika Nchi Wanachama. Katika kipindi hiki, Nchi tatu Wanachama wa Jumuiya zilifanya uchaguzi mkuu wa Rais na Wabunge. Nchi hizo ni Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Uganda. Jamhuri ya Burundi ilifanya Uchaguzi wake mwezi Julai, 2015 ambapo Rais Pierre Nkurunziza aliibuka mshindi wa Uchaguzi huo. Aidha, kwa upande wa Uchaguzi Mkuu wa Tanzania, Wizara iliratibu ushiriki wa waangalizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki waliokuja kufanya uangalizi ambapo Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli alipata ushindi katika uchaguzi huo.

171.      Mheshimiwa Spika, Wizara pia iliratibu ushiriki wa Tanzania katika timu ya waangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya kwenye uchaguzi mkuu wa Uganda uliofanyika mwezi Februari, 2016. Katika uchaguzi huo, Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili alipewa heshima ya kuwa Kiongozi wa timu hiyo kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni aliibuka mshindi.

172.      Mheshimiwa Spika, katika kuwashirikisha zaidi wananchi wa Afrika Mashariki kuchangia maoni yao katika maamuzi mbalimbali ya uendeshaji wa Jumuiya, Wizara yangu iliwawezesha Wananchi wa Tanzania kupitia asasi zao kushiriki katika Mkutano wa Katibu Mkuu wa Jumuiya na Asasi Zisizo za Kiserikali na Sekta Binafsi uliofanyika mwezi Machi, 2016 Dar es Salaam, Tanzania. Maazimio ya Mkutano huo yalikuwa  ni pamoja na kuliomba Baraza la Mawaziri la Jumuiya kuharakisha matumizi ya vituo vya utoaji wa huduma kwa pamoja mipakani, utekelezaji wa himaya moja ya forodha; na kushirikisha sekta binafsi katika ngazi zote za mchakato wa uchaguzi ili kuweka mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao.

Bunge la Afrika Mashariki

173.         Mheshimiwa spika, Wizara iliratibu na kushiriki katika mikutano ya Bunge la Afrika Mashariki, ambapo Bunge hilo lilijadili na kupitisha Miswada ya Sheria za Jumuiya, Maazimio na Taarifa mbalimbali. Miswada iliyopitishwa ni pamoja na Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kupunguza na Kukabiliana na Majanga wa mwaka 2012; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Miamala ya Kielektroniki wa mwaka 2014; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Tasnia ya Ubunifu na Utamaduni wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2015; na  Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu wa mwaka 2015. 

174.         Mheshimiwa spika, aidha, Miswada iliyosomwa Bungeni kwa mara ya kwanza ni: Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Usawa wa Jinsia na Maendeleo wa mwaka 2016; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Kulinda Watoa Taarifa wa mwaka 2016; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Mafao ya Kustaafu kwa baadhi ya Wakuu wa Taasisi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi wa Forodha ya Afrika Mashariki wa mwaka 2016; na Muswada wa Sheria ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wa Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu wa mwaka 2016.

175.         Mheshimiwa spika, Vilevile, Bunge lilitoa Maazimio kwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kusisitiza Kuridhia Itifaki ya Umoja wa Afrika ya kuanzisha Bunge la Afrika; Kuridhia Itifaki ya Sheria ya Ushauri ya Umoja wa Afrika inayohusiana na Bunge la Afrika; Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushindi wake katika uchaguzi Mkuu pamoja na wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kudumisha Amani na Demokrasia wakati wa Uchaguzi; Azimio la Bunge la Kuzitaka Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kuchukua hatua za haraka katika kudhibiti Usafirishaji haramu wa binadamu; na Azimio la Bunge la kuwashukuru Wake wa Viongozi wa Nchi Waanzilishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.

176.         Mheshimiwa spika, Kamati ya Bunge la Afrika Mashariki ya Masuala ya Kikanda na Utatuzi wa Migogoro ilifanya ziara ya Uangalizi na tathmini ya changamoto za utekelezaji wa Itifaki ya Soko la Pamoja katika Kanda ya Kati mwezi Novemba 2015.  Kamati hiyo na Uongozi wa Wizara ilijadili hali halisi ya utekelezaji wa makubaliano ya Itifaki hiyo hususan katika kanda ya kati ambapo kati ya masuala yaliyoibuliwa ni kuhusu afya ya Wananchi katika kutumia uhuru wa watu wa Jumuiya kuingia na kutoka Nchi za Jumuiya ambapo walisisitiza kuhusu umuhimu wa Chanjo ya Homa ya Manjano ili kuzuia uambukizaji wa ugonjwa huo.

177.         Mheshimiwa Spika, Kamati mbalimbali za Bunge la Afrika Mashariki zilifanya mikutano ya kukusanya maoni ya wadau kuhusu utungwaji wa sheria mbalimbali za Jumuiya ambapo Kamati ya Mawasiliano, Biashara na Uwekezaji ilikusanya maoni  ya Muswada wa Sheria ya Sectional Properties Bill, 2016, Kamati ya Kilimo, Maliasili na Mazingira ilikusanya maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Usimamizi na Uhifadhi wa Misitu wa Afrika Mashariki wa mwaka 2015 na Kamati ya General Purpose ilikusanya maoni kuhusu Muswada wa Sheria ya Watu Wenye Ulemavu wa mwaka 2015.

178.         Mheshimiwa Spika, Wizara iliratibu Programu ya Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Jumuiya ya kutoa elimu kwa umma iliyohusisha Vyombo vya Habari, Taasisi za Elimu, Asasi za Kiraia, Wabunge na Maafisa wa Serikali mwezi Aprili, 2016. Lengo la programu hiyo pamoja na mambo mengine ni  kuhamasisha umma juu ya fursa zitokanazo na Jumuiya ili kunufaika nazo.

Ushirikiano katika Ulinzi

179.      Mheshimiwa Spika, ili kuimarisha uwezo wa vyombo vya ulinzi na usalama vya Nchi Wanachama katika urejeshaji amani wakati wa machafuko, kukabiliana na ugaidi, uharamia na majanga, Wizara iliratibu ushiriki wa Tanzania katika zoezi la kijeshi kwa vyombo vya ulinzi na usalama kutoka nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki la Vituo vya Kamandi lijulikanalo kama ‘Ushirikiano Imara 2016’. Zoezi hilo lilifanyika mwezi Machi 2016 nchini Kenya.

Ushirikiano katika Usalama

180.      Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kuwa amani na usalama ni nguzo kuu kwa maendeleo ya kijamii na uchumi katika Jumuiya, Wizara yangu iliratibu ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Wakuu wa Upelelezi toka Jeshi la Polisi, Wasajili wa Magari, Wakuu wa Kupambana na Madawa ya Kulevya na Wakuu wa Vitengo vya Kupambana na Biashara Haramu ya Watu uliofanyika mwezi Desemba 2015 Nairobi, Kenya. Mkutano huo ulitoa fursa kwa wakuu hao kubadilishana uzoefu na taarifa za mienendo ya uhalifu katika maeneo yao na kupanga mpango wa pamoja wa operesheni za kupambana na uhalifu. Aidha, Nchi Wanachama zinaendelea kutekeleza Mkakati wa Kikanda wa Amani na Usalama.

181.      Mheshimiwa Spika, napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kuwa Jamhuri ya Sudan Kusini imejiunga rasmi na Jumuiya na hivyo kuifanya idadi ya Nchi Wanachama kuongezeka kutoka tano hadi sita. Nchi ya Sudan Kusini, iliwasilisha rasmi maombi ya kujiunga na Jumuiya mwezi Novemba, 2011. Nchi Wanachama zilikamilisha mchakato wa uhakiki kuthibitisha iwapo nchi hiyo inakidhi vigezo kulingana na matakwa ya Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Nchi Wanachama uliofanyika mwezi Machi 2016 jijini Arusha uliridhia nchi hiyo kujiunga na Jumuiya.

182.      Mheshimiwa Spika, Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya walimpa heshima Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya kusaini Mkataba wa Jamhuri ya Sudan Kusini kujiunga na Jumuiya kwa niaba yao. Zoezi la utiaji saini Mkataba huo, lilifanyika Dar es Salaam tarehe 15 Aprili, 2016.

183.      Mheshimiwa Spika, kujiunga kwa Jamhuri ya Sudan Kusini kumeifanya Jumuiya kuwa na jumla ya watu zaidi ya milioni 160, hii ni fursa ya kipekee kwa sekta binafsi hapa nchini katika kuendeleza na kukuza biashara zao. Naomba kuchukua nafasi hii kuishauri sekta binafsi hapa nchini kuchangamkia fursa zitokanazo na kupanuka kwa soko la Jumuiya.



184.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kutekeleza Mkakati wake wa Mawasiliano kwa kutoa Elimu kwa Umma kuhusu fursa zilizopo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na jinsi ya kunufaika nazo. Wizara ilitumia maonesho mbalimbali kama vile ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Saba Saba, Nane Nane, Maonesho ya Biashara Zanzibar, maonesho ya Siku ya Mara, Maonesho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani na Juakali/Nguvu Kazi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutoa elimu kwa Umma. Jumla ya nakala za machapisho 11,046 yenye taarifa muhimu na fursa zipatikanazo kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki yalisambazwa na jumla ya wananchi 7,387 walitembelea Mabanda ya Wizara ili kupata taarifa na ufafanuzi wa masuala ya mtangamano. Taarifa za maonesho hayo zilisambazwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo Luninga, tovuti na blogu ya Wizara. Vilevile, makala ya Televisheni yenye ujumbe wa fursa mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki ilioneshwa katika Luninga za TBC1, Star TV, Channel 10 na Clouds TV.

185.      Mheshimiwa Spika, Wizara yangu iliweka mabango saba katika mipaka ya Namanga, Horohoro, Holili, Sirari, Mutukula, Rusumo na Kabanga yenye kuelezea taratibu za kufuatwa na wafanyabiashara wakati wa kuuza na kununua bidhaa ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

186.      Mheshimiwa Spika, Wizara iliendesha mikutano ya  elimu kwa umma katika Mikoa ya Mwanza, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, Mara, Kagera, Mtwara, Lindi na katika mipaka ya Mutukula, Rusumo, Kabanga, Holili na Namanga. Aidha, Wizara iliendesha warsha ya Waandishi wa Habari wa Zanzibar kwa lengo la kuwaelimisha juu ya fursa na masuala ya Mtangamano ili waweze kufikisha taarifa sahihi za Mtangamano kwa wananchi.



187.      Mheshimiwa Spika,  Wizara iliendelea kuimarisha uwezo wa kiutendaji kwa kupandisha vyeo watumishi 20 baada ya kukidhi Vigezo vya Kisheria kama vilivyoainishwa katika Miundo yao ya Utumishi pamoja na kutengewa fedha katika Makisio ya Ikama na Bajeti ya Mishahara ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2015/2016. Aidha, Wizara iliwabadilisha kada jumla ya watumishi watatu wa kada tofauti baada ya kujiendeleza kitaaluma wakiwa kazini na kupata sifa stahiki. Vilevile, watumishi 29 wamethibitishwa kazini na watumishi 15 wa kada mbalimbali walithibitishwa katika vyeo vyao vipya baada ya kukidhi vigezo.

188.      Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Wizara inawajengea uwezo wa kitaaluma watumishi wake ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi, Wizara iliandaa na kutekeleza mpango mdogo wa mafunzo kwa mwaka wa fedha 2015/2016 ambao hadi kufikia mwezi Februari 2016 watumishi wawili (2) walihudhuria mafunzo ya muda mrefu na watumishi tisa (9) walihudhuria mafunzo ya muda mfupi.  Mpango huu mdogo ni utekelezaji wa mpango wa mafunzo wa Wizara wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2015/2016 hadi 2017/2018.


USIMAMIZI WA MAPATO NA MATUMIZI


189.      Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kuimarisha usimamizi na uwajibikaji katika Mapato na Matumizi ya Fedha za Umma kwa kuzingatia sheria na kanuni za fedha za umma. Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Wizara imeendelea kupata Hati Safi ya Ukaguzi wa Hesabu. Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, Fungu 34 na 97 pamoja na balozi 34 zilizokuwepo kwa wakati huo zimepata Hati Safi. Naomba nichukue nafasi hii kuwapongeza watendaji wa Wizara na kuwahimiza waendelee kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya matumizi ya fedha za Serikali.

CHANGAMOTO ZILIZOJITOKEZA KATIKA UTEKELEZAJI WA BAJETI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016


190.      Mheshimiwa Spika, Changamoto  ambazo Wizara imekabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake ni kama ifuatavyo:

             i.        Kasi ndogo ya ubadilishaji wa Sheria za Nchi ili kuendana na matakwa ya Itifaki ya soko la pamoja la Afrika Mashariki;
           ii.        Kasi ndogo ya sekta binafsi kutumia fursa za biashara na uwekezaji zitokanazo na mtangamano wa Afrika Mashariki na masoko ya kimataifa; na uelewa mdogo wa Watanzania kuhusu masuala ya Mtangamano;
          iii.        Kasi ndogo ya Watanzania kuchangamkia fursa za ajira zilizopo kwenye taasisi za kikanda na kimataifa;
          iv.        Kuendelea kuibuka kwa vikwazo vipya visivyo vya kiforodha ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
            v.        Wigo mdogo wa uwakilishi nje. Hadi hivi sasa, Tanzania ina Balozi 35 na Konseli Kuu 3 duniani. Uwakilishi huu ni mdogo kuweza kukidhi mahitaji ya nchi hususan katika kipindi hiki ambacho fursa mbalimbali zinaibuka kila kona ya dunia.

191.      Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na changamoto zilizotajwa hapo juu Wizara yangu imejipanga kutekeleza yafuatayo:

             i.        Kuendelea kuzihimiza sekta husika kutoa kipaumbele na kuongeza kasi ya ubadilishaji wa sheria zilizoainishwa ili kuwawezesha Watanzania kunufaika ipasavyo na fursa za soko la pamoja;
           ii.        Kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na fursa zitokanazo na ushiriki wa nchi yetu katika Jumuya za kikanda na kimataifa, na kupitia makubaliano na mikataba mbalimbali kwa lengo la kuhamasisha Watanzania kuzitumia ipasavyo;
          iii.        Kuendelea kuhamasisha Watanzania kujitokeza pindi fursa za ajira zilizopo kwenye taasisi za kikanda na kimataifa zinapotangazwa;
          iv.        Kuendelea kuratibu uondoaji wa vikwazo visivyo vya kiforodha nchini ili kuwavutia wafanyabiashara kutoka ndani ya Jumuiya kununua bidhaa zinazozalishwa nchini na kutumia bandari zetu kikamilifu; na
            v.        Wizara itaendelea kuimarisha Balozi zetu na kufungua ofisi za uwakilishi kwenye maeneo yenye maslahi kwa taifa.

SHUKRANI


192.      Mheshimiwa Spika, Wizara imefanikiwa kutekeleza sehemu  ya majukumu yaliyotajwa hapo juu kwa ushirikiano na washirika wa maendeleo kutoka nchi na asasi mbalimbali za kitaifa, kikanda, kimataifa pamoja na sekta binafsi. Naomba nitumie fursa hii kuwashukuru washirika wetu wote wa maendeleo ikiwa ni pamoja na Australia, Brazil, Canada, China, Cuba, Denmark, Finland, India, Italia, Ireland, Japan, Korea Kusini, Kuwait, Malaysia, Marekani, Malta, Norway, Oman, Poland, Qatar,  Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uhispania, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Ureno, Urusi, Uswisi, Uturuki, Umoja wa Ulaya, AfDB, African Capacity Building Facility, FAO, IAEA, ILO, IMF, IOM, Investment Climate Facility for Africa,UNDP, UNEP, UN-HABITAT, UNWTO, UNHCR, UNICEF, UNFPA,  UNESCO, UNIDO, WHO, TradeMark East Africa, The Association of European Parliamentarians with Africa, World Bank na WWF kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha utekelezaji wa Diplomasia ya uchumi.

MALENGO YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017


193.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, pamoja na mambo mengine, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imepanga kutekeleza malengo makuu muhimu kulingana na majukumu yake kama ifuatavyo:-

             i.        Kuitangaza nchi yetu kama moja ya nchi duniani zenye mazingira mazuri kwa ajili ya uwekezaji kutokana na historia yake ya miaka mingi ya amani, umoja, utulivu na mshikamano wa kitaifa;
           ii.        Kuongeza uwakilishi wetu nje ya nchi kwa kufungua Balozi mpya, Ofisi za Kikonseli na kuimarisha rasilimali watu na fedha;
          iii.        Kuendelea kusimamia, kufuatilia na kuratibu utekelezaji wa mikataba mbalimbali iliyosainiwa kati ya nchi yetu na nchi nyingine na ile ya mashirika ya kikanda na kimataifa;
          iv.        Kukamilisha mchakato wa kuitambua jumuiya ya watanzania wanaoishi ughaibuni na kuweka utaratibu utakaowawezesha kuchangia maendeleo ya taifa;
            v.        Kuratibu majadiliano kuhusu maeneo ya ushirikiano katika uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi, kijamii na kuendeleza ushirikiano katika sekta za uzalishaji;
        vii.        Kuratibu majadiliano na kusimamia utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Jumuiya nyingine za Kikanda kuhusu kuanzisha Eneo Huru la Kibiashara na Kiuchumi;
       viii.        Kuratibu, kushiriki na kusimamia majadiliano na utekelezaji wa makubaliano katika maeneo ya siasa, ulinzi na usalama;
          ix.        Kuratibu, kushiriki na kusimamia majadiliano na utekelezaji wa hatua za Mtangamano wa Afrika Mashariki; na
           x.        Kutoa Elimu kwa Umma kuhusu Jumuiya ya Afrika Mashariki na fursa zinazopatikana katika Jumuiya hiyo.


MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA KWA MWAKA WA FEDHA 2016/2017


194.      Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Wizara imepangiwa bajeti ya kiasi cha shilingi 151,396,775,000.00 Kati ya fedha hizo shilingi 143,396,775,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na shilingi 8,000,000,000.00 ni kwa ajili ya bajeti ya Maendeleo.

195.      Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya Matumizi ya Kawaida ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2016/2017, shilingi 133,056,021,000.00 ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo na shilingi 10,340,754,000.00 ni kwa ajili ya Mishahara. Kati ya fedha za Matumizi Mengineyo shilingi 720,160,000.00 ni kwa ajili ya Mpango wa Kujitathmini Kiutawala Bora Tanzania, shilingi 3,154,721,000.00 ni kwa ajili ya fedha za Mishahara na Matumizi Mengineyo ya Chuo cha Diplomasia na shilingi 686,298,378.00 ni kwa ajili ya Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu.

196.      Mheshimiwa Spika, katika fedha za bajeti ya maendeleo za kiasi cha shillingi 8,000,000,000.00 zilizopangwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017, kiasi cha shilingi 2,375,250,000.00 zitatumika kufanikisha ujenzi wa jengo la ofisi ya Wizara ambalo ni sehemu ya Kituo cha Mikutano ya Kimataifa cha Julius Nyerere; shilingi 1,316,435,000.00 zitatatumika kukamilisha ukarabati jengo la ghorofa tisa (9), makazi ya Balozi na Mkuu wa Utawala Ubalozi wa Tanzania Maputo, Msumbiji; shilingi 2,172,880,000.00 zitatumika kukarabati makazi ya Balozi na watumishi yaliyopo Stockholm, Sweden; shilingi 1,813,871,000 zitatumika kukarabati majengo mawili yanayomilikiwa na Serikali yaliyopo Khartoum, Sudan  na shilingi 321,564,000.00 kwa ajili ya kuboresha mfumo wa mawasiliano kati ya Wizara na Balozi za Tanzania nje.

197.      Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara kupitia Balozi zake, inatarajia kukusanya kiasi cha shilingi 24,001,150,000.00 kama maduhuli ya Serikali.

HITIMISHO


198.    Mheshimiwa Spika, ili kuweza kutekeleza kikamilifu majukumu yaliyotajwa hapo juu, kwa mwaka wa fedha 2016/2017, naomba Bunge lako Tukufu liidhinishe jumla ya Shilingi 151,396,775,000.00. Kati ya fedha hizo Shilingi 143,396,775,000.00. ni kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi 8,000,000,000.00. ni kwa ajili ya Bajeti ya Maendeleo.

199.    Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua nafasi hii kukushukuru wewe binafsi, na Waheshimiwa Wabunge kwa kunisikiliza.

200.     Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.