Mkutano wa nganzi ya juu kuhusu UKIMWI jana ( alhamis) uliingia katika siku yake ya pili ambapo viongozi mbalimbali
wakiwamo Mawaziri na Manaibu waziri wanaohusika na masuala ya
afya wameendelea kuelezea nini ambacho nchi zao zinatekeleza katika kukabili na
kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vinavyosababisha UKIMWI pamoja na huduma wanazopatiwa
watu ambao wamekwisha kuathirika na kuugua.
Mmoja ya nchi ambayo iliwasilisha
mafanikio, changamoto na mwelekeo wa baadaye
katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa
UKIMWI, ambao jumuiya ya kimataifa umejiwekea
lengo la kuutokomeza ifikapo mwaka 2030
ilikuwa ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Juhudi za Tanzania dhidi ya
UKIMWI, zilielezwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.
Dkt. Hamis A. Kigwangalla (Mb). Ambaye katika maelelezo yake amesema, Tanzania
inaamini kuwa inawezekana kufikia hali ya kutokuwa na maambukizi mapya,
kumaliza ubaguzi na unyanyapaa, na kuwa na kiwango sifuri cha vifo vinavyohusiana na UKIMWI Ifikapo mwaka
2030.
Hata hivyo anasema, ilikufikia
hatua hiyo au mafanikio hayo, mambo kadhaa yanapashwa kufanyika, yakiwamo ya uimarishwaji
wa elimu ya kinga, vijana na jumuiya kwa
ujumla kufundishwa mbinu za kuepukana na tabia hatarishi ambazo zinachangia ongozeko
la waathirika na kuhakikisha upatikanaji
kirahisi wa dawa na ambazo zitakuwa za gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri ambaye anaongoza ujumbe wa Tanzania
katika mkutano huo, amekwenda mbali zaidi kwa kusema pia patahitajika kupunguza
vifo vitokanavyo na ugonjwa wa Kifua Kikuu kwa watu wanaoishi na virusi vya ukimwi, kujadili masuala ya jinsia pamoja na mila na tamaduni, kutenga raslimali za kutosha kwaajili ya watu
wenye mahitaji wakiwamo vijana, kuwa na viwanda vitakavyoweza kuzalisha dawa.
Akizungumza baadhi ya mafanikio
ambayo Tanzania imekwisha kuyafikia katika kukabili tatatizo la ugonjwa wa UKIMWI,
Naibu Waziri ameyataja baadhi ya mafanikio
hayo kuwa ni pamoja na kupunguza maambukizi mapya kutoka 140,000 mwaka 1990 hadi kufikia 63,000 mwaka
2014. Vilevile vifo vitokanavyo au vinavyo sababishwa na UKIMWI pia vimepungua kwa asilimi 40 katika kipindi hicho.
Akaeleza pia kwamba hata watu
wanaopatiwa huduma ya matibabu nayo imeongezeka kufikia asilimia 60 huku ongezeko
likiwa kwa watoto na hasa baada ya kupitisha mpango unaotambulika kama Option
B+ miaka sita iliyopita.
Kuhusu kupungua kwa raslimali
fedha hususani kutoka kwa wafadhili, Dkt. Kingwangalla, amesema katika kukabiliana
na changamoto hiyo, na kwa kuzingatia wito wa jumuiya ya kimataifa kupanua wigo
wa mapato ya ndani, serikali ya Tanzania
ilianzisha Mfuko wa UKIMWI, (AIDS Trust Fund) mfuko ambao alisema hadi
sasa serikali ndiyo imekuwa mchangiaji mkuu, ingawa pia kuna sekta binafsi nayo inatazamiwa kuchangia.
Akasema sehemu au nusu ya fedha hizo (55%) itakwenda kusaidia
upatikanaji wa huduma na kuongeza kuwa juhudi hizo za serikali pia zimesaidiwa na
ushirikiano baina ya Tanzania na nchi nyingine rafiki pamoja na mashirika ya kimataifa
na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wale
wote ambao wanachangia juhudi za serikali.
Kuhusu mipango mingine ambayo
serikali inaendelea nayo , Naibu waziri alikuwa
na haya ya kueleza “ baada ya kuwa tumeanza utaratibu wa kupima na kutibu kwa baadhi
ya wilaya chache nchini, tunakusudia kuisambaza huduma hiyo lakini itakuwa ni kwa
hatua ili kutoa nafasi ya kuwajengea uwezo watoaji wa huduma ya afya, kuhuisha mifumo
ya usambazaji wa vifaa ikiwa ni pamoja na ushiriki wa jamii iliiweze kupokea na
kuukubali mfumo huu mpya wa utoaji wa huduma” ameeleza Naibu Waziri.
Akasisitiza zaidi kwa kusema
ingawa ugonjwa wa UKIMWI umeendelea kuwa changamoto kubwa kwa maendeleo ya nchi
ambapo inakadiriwa watu milioni moja na nusu (1.5) wameathirika, huku mzigo mkubwa
ukiwaelemea wanawake na vijana hasa watoto wa kike, serikali ya Tanzania
itaendelea na jitihada zake za kuhakikisha inafikia lengo la kutokuwa na maambukizi mapya, kutokomeza unyanyapaa na ubaguzi, na vifo vitokanavyo
na UKIMWI.
Katika hatua nyingine amesema
ili kutorudisha nyuma mafanikio ambayo
Tanzania imeyafikia hadi sasa pamoja na nchi nyingine kusini mwa Jangwa
la Sahara Jumuiya ya Kimataifa inaombwa kusaidia jitihada zinazofanywa na serikali
za nchi hizo za kuwa na mapato yake yenyewe ya kugharamia huduma za afya kwa wagonjwa
wa UKIMWI pamoja na huduma nyinginezo badala ya kuziachia kabisa jukumu hilo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.