Thursday, June 30, 2016

Diaspora wahimizwa kutii Sheria bila Shuruti


TANGAZO KWA WATANZANIA WOTE NA WALE WANAOISHI NJE YA NCHI (DIASPORA)

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, inaendelea na jitihada zake za kuhamasisha Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) katika kuchangia maendeleo ya nchi yao.  Ili kufanikisha hilo, Wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo imekuwa ikizishawishi taasisi mbalimbali hapa nchini kutoa huduma na fursa za biashara na uwekezaji, ambazo zitasaidia Diaspora kuwekeza kiurahisi hapa nchini.  Juhudi hizi ambazo zilianza tokea Serikali ya Awamu ya Nne zimeanza kutoa matunda makubwa ambapo thamani ya uwekezaji kutoka kwa Diaspora inaongezeka kila kukicha.


Kutokana na umuhimu wa Diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi na huduma nyingine za kijamii; Serikali inapenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha Watanzania wote wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) umuhimu wa kuheshimu na kutii sheria na taratibu katika nchi wanazoishi. Aidha, Serikali pia inapenda kuwakumbusha tena Watanzania wote wenye nia ya kusafiri nje ya nchi kwa lengo la kupata ajira au kutafuta maisha bora (greenpastures), kuhakikisha kuwa mikataba ya ajira inatambulika na mamlaka za nchi husika. Sambamba na hilo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ofisi za Balozi za Tanzania nje ya nchi zitaendelea kuwa mstari wa mbele kusaidia kutatua matatizo ya namna hiyo kwa Watanzania; pamoja na Taasisi za Serikali kama vile Wakala wa Ajira Tanzania (TAESA).

Serikali pia inawakumbusha Watanzania wanaotaka kusafiri nje ya nchi kwa malengo mbalimbali kama vile masomo, biashara, makazi au masuala yoyote binafsi nao kuheshimu sheria na taratibu za nchi husika.  Taratibu hizo ni pamoja na:
1)          Kujitambulisha na kujiandikisha kwenye Ofisi za Balozi za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nchi wanazoishi au kama katika nchi hizo hakuna Ofisi ya Ubalozi wanashauriwa kuwasiliana na Ofisi za Ubalozi zilizo karibu na nchi yao.  Kufanya hivyo kutarahisisha maafisa wa Ubalozi kuweka kumbukumbu zao kwa ajili ya mawasiliano ili kama kuna taarifa muhimu ziwafikie kwa wakati; au endapo watapata majanga ya aina yoyote waweze kuhudumiwa mapema;
2)          Kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za nchi wanazoishi na kuwa raia wenye uzalendo na hekima;
3)          Kutojihusisha na tabia chafu zitakazohatarisha maisha yao kama vile kufanya biashara za magendo na madawa ya kulevya ambazo zinaweza kuwa na madhara kwao binafsi na pia kuiletea nchi yetu sifa mbaya;
4)          Kutunza Hati za Kusafiria (pasipoti) kwa kuwa ni utambulisho   muhimu kwao na pia ni nyaraka muhimu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
5)          Kutumia fursa zilizopo katika nchi wanazoishi kwa madhumuni ya kujiletea maendeleo yao na bila kusahau kutumia ujuzi, elimu, na maarifa waliyoyapata kwa ajili ya kuchangia kukuza uchumi wa nchi yao;
6)          Kuendelea kuitangaza Tanzania na kuwa mabalozi wazuri wenye uelewa na upendo wa nchi yao ili kuvutia watalii na wawekezaji wengi kuja hapa nchini;
7)          Kuendeleza matumuzi ya Lugha ya Taifa ya Kiswahili popote walipo ikiwa kama sehemu ya kukuza diplomasia ya utamaduni wetu;
8)          Kuwaelimisha na kuwahimiza ndugu zao na watoto wao popote walipo huko ughaibuni kutumia lugha ya Kiswahili na kueneza historia na tamaduni za Kitanzania ili wasisahau walikotoka.

Tunapenda pia kutumia nafasi hii kuwakumbusha kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inaendelea na jitihada zake thabiti za kutengeneza mazingira wezeshi ya kuwatambua, kuwahamasisha na kuwashirikisha Diaspora katika kuleta maendeleo yenye matumaini na tija kwa Tanzania.  Michango ya Diaspora katika maendeleo ya nchi kupitia sekta za kiuchumi, kibiashara, afya, elimu, miundombinu, na nyingine ni muhimu; na inazidi kukua na hatimaye itaipelekea Tanzania kuwa na uchumi wa kati katika miaka ya mbele.  Hivyo, Diaspora popote mlipo mnahimizwa kuzidi kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa letu bora la leo na la kesho.

IDARA YA DIASPORA

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA
USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI

DAR ES SALAAM.

30 Juni, 2016

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.