Askofu Francisco Montecillo Padilla akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Mabalozi waliohudhuria hafla hiyo
=========================================
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI.
WAZIRI MAHIGA ASHIRIKI HAFLA YA MAADHIMISHO YA MIAKA 3 YA UONGOZI WA BABA MTAKATIFU PAPA FRANCIS.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli katika hafla ya kuadhimisha miaka mitatu ya Uongozi wa Baba Mtakatifu Papa Francis pamoja na kumuaga Balozi wa Vatican na muwakilishi wa Papa hapa nchini Askofu Francisco Montecillo Padilla ambaye amemaliza muda wake wa kuhudumu hapa nchini.
Hafla hiyo ilifanyika jana jioni katika viwanja vya Parokia ya Mtakatifu Petro Osterbay Jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo Mhe. Mahiga alimpongeza Papa Francis pamoja na kumuelezea kuwa ni mtu wa Mataifa yote na mfano wa kiongozi bora duniani kwakuwa misingi yake ya uongozi imejikita katika kusimamia utu, kupinga Ubaguzi wa rangi pamoja na matabaka katika jamii. Pia amekuwa mpiganaji mkubwa katika masuala ya amani na mtetezi wa wakimbizi hivyo Tanzania na Dunia nzima inatambua mchango wake kwa ujumla na kuzidi kumwombea mafanikio katika utendaji wake.
Vilevile alimpongeza Askofu Francisco Montecillo Padilla ambaye amekuwa akihudumu nchini kwa muda wa miaka minne (4) na kueleza kuwa amekuwa mfano bora katika kazi za kichungaji kwa kuweza kutembelea nchi nzima katika Majimbo ya Kanisa Katoliki licha ya kazi yake kuwa na changamoto nyingi. Alikumbusha tukio la mlipuko lililotokea kanisani mjini Arusha wakati Askofu Padilla akiendesha Ibada, ni mfano dhahiri wa kazi alizokuwa akizifanya nchini na katika hilo amejiwekea historia katika huduma yake ya kichungaji.
Kwa upande wa ushirikiano baina ya Tanzania na Vatican, Mhe. Mahiga alieleza ni wa muda mrefu tangu 1960. Katika kuhakikisha uhusiano huo unaimalika mataifa hayo mawili yamekuwa yamekuwa yakifanya jitihada za makusudi katika kukuza uhusiano huo na alieleza hilo lilidhihirishwa na ujio wa Papa John Paul wa pili ambaye alifanya ziara nchini Tanzania mwaka 1990.
Pia alieleza Mhe. Rais Magufuli anapenda kutoa shukurani za dhati kwa huduma ambazo zimekuwa zikifanywa na Balozi wa Papa nchini pamoja na Kanisa Katoliki katika kuchangia shughuli za maendeleo hasa katika sekta ya Afya na Elimu ambapo wamefungua Shule za ufundi za Don Bosco katika Mikoa yote ."Ni imani yangu kuanzishwa kwa shule hizo hakutaishia katika ngazi ya mikoa tu, bali utaendelea katika ngazi ya wilaya na hata kata"
Aidha, alizungumzia sera ya viwanda ya Mhe. Rais John Pombe Magufuli katika kuondoa tatizo la kukosa ajira na kukuza uchumi wa Taifa, alimweleza Balozi huyo ni muda muafaka sasa mataifa hayo mawili yakajikita zaidi katika kuhakikisha yanaibua maeneo mapya ya ushirikiano ili kuhakikisha sera hiyo inafikiwa kwa kuvutia zaidi wawekezaji na kukuza biashara.
Watu wengine mashuhuri waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Benjamin W. Mkapa na mke wake Mama Anna Mkapa, Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, Kadinali Polycarp Pengo na Maaskofu wa Majimbo ya Kanisa Katoliki nchini, wengine ni Watawa na Walei.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.