Waziri Mahiga na Bi. Yeda wakibadilishana Mkataba mara baada ya kuusaini.
|
Waziri Mahiga asaini Mkataba wa uenyeji wa
Benki ya EADB
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb)
amesaini Mkataba wa uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za Benki ya Maendeleo ya
Afrika Mashariki (EADB) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bi. Vivienne Yeda. Mkataba
huo umesainiwa leo katika Ofisi za Wizara kwa lengo la kurasimisha kisheria Ofisi za
Benki hiyo zilizopo nchini.
Aidha, uwekaji
saini wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika tarehe 2 Machi, 2016 Mjini Arusha -Tanzania. Mkutano huo pamoja na
mambo mengine uliazimia kuanzishwa kwa Ofisi za Benki hiyo katika Makao Makuu
ya kila nchi Mwanachama ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa shughuli za
Benki hiyo.
Benki ya
Maendeleo ya Afrika Mashariki ni Taasisi ya Fedha iliyoanzishwa mwaka 1967
chini ya iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,
kwa lengo la kutoa misaada ya kifedha na misaada mingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
EADB
ilianzishwa wakati iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na wanachama
watatu ambao ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Rwanda ilijiunga na Benki hiyo mwaka
2007 na kufanya nchi wananchama waliojiunga kufikia wanne.
Kwa upande
wa Tanzania, EADB imeisaidia kutoa mikopo mbalimbali katika miradi ya maendeleo
kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB).
Pia, katika kulipa kipaumbele suala la Afya, Benki hiyo imeweka mpango wa kusaidia afya ya uzazi kwa akinamama
hususan, katika maeneo ya vijijini.
Miradi
mingine inayofadhiliwa na EADB hapa nchini ni pamoja na miradi ya Umeme hasa
kwa maeneo ya vijijini, na miradi ya maji na usafi wa mazingira.
Akiongea
katika hafla hiyo, Mhe. Waziri Mahiga aliahidi
kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika
kuhakikisha uendeshaji wa Benki hiyo unafanikiwa. “Karibuni sana na pale inapotokea mmekwama katika jambo lolote linalohitaji
usaidizi wa Serikali au ushauri tupo tayari kutoa ushirikiano” alisema Waziri
Mahiga.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.