Thursday, August 25, 2016

Mkutano wa TICAD kufanyika Afrika kwa mara ya kwanza

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya, Balozi Monica Juma (mwenye nguo ya kijani) akifuatiwa na Bw. Takeshi Osuga, Balozi wa TICAD kutoka Japan na  Mhe. Cherif Mhamat Zene, Balozi wa Chad, Ethiopia wakiongoza moja ya vika vya Maafisa Waandamizi ikiwa ni maandalizi ya Mkutano wa Sita wa TICAD.
=====================================================================================

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Mkutano wa  6 wa Kimataifa kuhusu Ushirikiano wa Maendeleo kati ya Japan na Afrika (Tokyo International Conference on African Development-TICAD VI) unatarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Agosti, 2016 Jijini Nairobi, Kenya. Hii ni mara ya kwanza kwa mkutano huu kufanyika nje ya Japan tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.

Mkutano huu wa Sita ambao umetanguliwa na kikao cha Maafisa Waandamizi wakiwemo Makatibu Wakuu na Mabalozi tarehe 24 na 25 Agosti, 2016 utafuatiwa na kikao cha Mawaziri tarehe 26 Agosti, 2016 unatarajiwa kupitisha Azimio la Nairobi ambalo litajikita katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazolikabili Bara la Afrika katika kufikia maendeleo na ustawi.

Changamoto hizo ni pamoja na kuporomoka kwa bei za bidhaa zinazotegemewa na nchi za Afrika katika ustawi wake kama vile mafuta, gesi na madini na hivyo kupelekea kuathirika kwa ukuaji wauchumi katika nchi nyingi za Afrika; kulipuka kwa magojwa kama Ebola na kusababisha vifo vilivyopelekea kusitishwa kwa shughuli za kiuchumi na kupotea kwa nguvu kazi; na Kuongezeka kwa vitendo vya ugaidi.

Agenda nyingine zitakazojadiliwa ni pamoja na: Kuhamasisha mageuzi ya kiuchumi kupitia uendelezaji wa viwanda; Kuboresha sekta ya Afya kwa maisha bora na Kusaidia jitihada za kudumisha amani na utulivu katika jamii.

Vile vile Mkutano huu umetoa kipaumbele kwa ushiriki wa sekta binafsi hususan wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka Japan na Afrika. Hivyo mkutano utatoa fursa kwa taasisi zenye dhamana ya kuvutia uwekezaji, biashara na utalii nchini kutangaza fursa zilizopo kwa kampuni za Japan.

Mkutano huu wa 6 wa TICAD ambao unashirikiana kwa karibu na Kamisheni ya Umoja wa Afrika unalenga kuiwezesha Afrika kujitegemea katika kukua na kufikia maendeleo yaliyokusudiwa ikiwemo utekelezaji wa Agenda 2063 ambayo viongozi wa Afrika walikubaliana wakati wakuadhimisha miaka 50  ya Umoja wa Afrika. Agenda 2063  inalenga kuliunganisha Bara la Afrika katika masuala ya kukuza uchumi; kuhamasisha utawala bora na utawala wa sheria; kuhakikisha maendeleo kwa mtu mmoja mmoja; kuhakikisha amani na usalama unaimarika na kuiweka Afrika kwenye nafasi ya mchangiaji mkuu wa uchumi duniani.

Mkutano wa kwanza wa TICAD uliofanyika Jijini Tokyo mwaka 1993 ulijikita zaidi katika agenda ya kuongeza misaada kwa nchi za Afrika. Kufuatia mkutano huo misaada ya Japan kwa nchi za Afrika iliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 0.6 mwaka 1993 na kufikia Dola bilioni 0.8 mwaka 1998. Hadi kufikia mwaka 2013 msaada wa Japan (ODA) kwa nchi za Afrika ulifikia Dola za Marekani bilioni 2.8.

Mkutano wa 6 wa TICAD ambao kwa mara ya kwanza katika historia unafanyika Afrika utawezesha majadiliano ya ana kwa ana kati ya Wakuu wa Nchi na Wawakilishi kutoka Sekta binafsi.

Kadhalika, mbali na mwenyeji wa Mkutano huu ambaye ni Rais wa Kenya, Mhe. Uhuru Kenyatta mkutano utahudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa Japan, Mhe. Shinzo Abe, Viongozi Wakuu kutoka nchi 54 za Afrika pamoja na wawakilishi kutoka mashirika ya kimataifa na makundi mbalimbali.

Ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huu utaongozwa na Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

-Mwisho-

 Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali
Wizara  ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
25 Agosti, 2016





No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.