Wednesday, December 21, 2016

Kikao cha Kwanza cha Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na UAE chafanyika Abu Dhabi





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Balozi Augustine Mahiga (kushoto) kwa pamoja na  Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakisaini  Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga. Mkataba huo ulisainiwa wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi, Falme za Kiarabu tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharika, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Uchumi na Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE wakiwekeana saini baadhi ya makubaliano yaliyoafikiwa.
Mhe. Dkt. Mahiga na ujumbe alioongozana nao wakiwa katika kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano na ujumbe wa UAE kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Mratibu wa Mkutano kwa upande wa Serikali ya Tanzania kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hangi Mgaka akifuatilia mkutano.


Picha ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania na UAE mara baada ya kukamilisha kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UMOJA WA FALME ZA KIARABU ZAFANYA MKUTANO WA KWANZA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU YA USHIRIKIANO HUKO ABU DHABI. 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimefanya kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano huko Abu Dhabi makao makuu ya Umoja wa Falme za Kiarabu.  Kikao hicho kilifanyika tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.

Mkutano huo ulioshirikisha sekta mbalimbali za Serikali zote mbili uliongozwa na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania na Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). 

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo Tanzania na UAE zimekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya Kidiplomasia; Uchumi; Utalii; Nishati; Kilimo; Sayansi na Teknolojia; Usafirishaji; Miundombinu; Ulinzi na Usalama; Elimu pamoja na Kazi na Ajira. 

Sambamba na mkutano huo, Tanzania na UAE zimesaini Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga (Bilateral Air Service Agreement-BASA) na Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utalii. Vilevile Serikali zote mbili zimekubaliana kukamilisha na kusaini Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi za Mapato; Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji; pamoja na ushirikiano katika sekta ya Elimu, Afya, Ulinzi na Usalama, Ushirikiano katika Usafiri wa Majini,  Kazi na Ajira pamoja ushirikiano katika masuala ya Zimamoto na Uokoaji. 

Mkutano huo umekuwa ni chachu katika mahusiano ya kihistoria ya nchi hizi mbili ambapo umeweka mazingira rasmi ya ushirikiano sio tu kwa Serikali bali pia kwa sekta binafsi. 

Mheshimiwa Waziri Mahiga katika hotuba yake ya ufungaji alitoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla za Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu kuchangamkia fursa zinazopatikana katika nchi hizi mbili kuafuatia mkutano huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Desemba, 2016.


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.