Friday, December 30, 2016

Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje akutana na Naibu Balozi wa China nchini

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima akizungumza na Naibu Balozi wa China nchini, Bw. Gou Haudong alipofika Wizarani kwa ajili ya kuzungumzia masuala mbalimbali ya ushirikiano kati ya Tanzania na China.
Sehemu ya ujumbe kutoka Ubalozi wa China nchini ukifuatilia mazungumzo kati ya Balozi Mlima na Bw. Gou (hawapo pichani)

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Luangisa (kushoto) akiwa na Bw. Humphrey Shangarai, Afisa Mambo ya Nje nao wakifuatilia mazungumzo
Bw. Gou akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Balozi Mlima.

Thursday, December 29, 2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI




Ufafanuzi kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Watanzania wanaodaiwa ni majasusi nchini Malawi

Baadhi ya Vyombo vya habari vya hapa nchini hivi karibuni vilitoa taarifa kuwa, Watanzania 8 wanaodaiwa kuwa ni majasusi wa Serikali ya Tanzania wamekamatwa nchini Malawi kwa tuhuma za kuingia kwenye mgodi wa urani wa Kayerekera uliopo nchini Malawi kinyume cha sheria. 
Taarifa hiyo kwa mara ya kwanza ilitolewa na chombo cha habari cha Malawi ambacho kilidai kuwa watu hao wametumwa na Serikali ya Tanzania ili kuchunguza kama Serikali ya Malawi inatengeneza silaha za nyuklia kwa kutumia madini ya urani ya kutoka mgodi huo.

Kufuatia taarifa hizo, Wizara kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi ulifuatilia ili kubaini ukweli wa tukio hilo. Baada ya kufuatilia ilibainika kuwa ni kweli Watanzania 8 kutoka taasisi ya CARITAS iliyo chini ya Kanisa Katoliki Songea mkoani Ruvuma walikamatwa na vyombo vya usalama katika Wilaya ya Karonga ambayo inapakana na Wilaya ya Kyela.  Watanzania hao mara moja walifunguliwa kesi kwa kutuhumiwa kufanya kosa la jinai la kuingia eneo la mgodi bila kibali (criminal trespass).

Ubalozi uliwasiliana na Taasisi ya CARITAS kutaka kufahamu madhumuni ya watu hao kufanya ziara nchini Malawi. Ubalozi ulielezwa kuwa ziara hiyo ilikuwa ni ya mafunzo ambapo walitaka kufahamu juu ya madhara yatokanayo na machimbo ya madini ya urani. Watanzania hao kwa sasa wapo katika gereza kuu la Mzuzu hadi kesi yao itakapotajwa tena tarehe 04 Januari 2017.

Ubalozi unaendelea kufanya mawasiliano na Kanisa Katoliki Songea ili kupata maelezo zaidi kuhusu ziara ya watu hao kwa madhumuni ya kuyawasilisha mamlaka husika ili watuhumiwa waweze kutolewa.
Aidha, Wizara kupitia Ubalozi umebaini kuwa CARITAS iliruhusu watu hao kufanya ziara nchini Malawi bila kupata kibali kutoka mamlaka husika na bila kutoa taarifa Ofisi ya Ubalozi kuhusu ziara hiyo. 

Aidha, kipindi cha kufanya ziara hiyo nchini Malawi hakikuwa muafaka kwa kuwa watumishi wa Serikali ya Malawi wanakuwa katika likizo ya mwaka kuanzia tarehe 22 Desemba hadi 03 Januari 2017. Hii inakwamisha juhudi za kuwafuatilia watu hao ikiwa ni pamoja na kukwama kwa maombi ya kibali cha kuwatembelea watu hao tarehe 28 Desemba 2016.

Wizara inatoa wito kwa mara nyingine kwa taasisi za dini, vyuo vya elimu na watu binafsi kuomba vibali na kufuata sheria za nchi nyingine wanapofanya ziara za mafunzo au ziara nyinginezo ikiwa ni pamoja na kuwasiliana na ofisi za Balozi zetu kwa madhumuni ya kufahamishwa taratibu zinazotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya ziara husika ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza. 

Wizara, kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi unaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa suala hilo linapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 29 Desemba  2016.


Tuesday, December 27, 2016

Wizara ya Mambo ya Nje yafanya kikao cha cha pamoja cha watumishi kujadili masuala ya kiutendaji

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga (katikati) akizungumza na watumishi wa Wizara hawapo pichani, kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika leo katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz P. Mlima na kushoto ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Bw. Hamid Mbegu.

Sehemu ya Wakurugenzi wakifuatilia kikao, kutoka kushoto Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Balozi Mbelwa Kairuki, Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, Balozi Samuel Shelukindo, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati, Balozi Abdallah Kilima na Mkurugenzi wa Kitengo cha Sheria, Balozi Baraka Luvanda.
Sehemu nyingine ya Wakurugenzi, katikati ni Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama Bw. Stephen Mbundi, Kulia ni Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara, Bi. Mindi Kasig.
Watumishi wakifuatilia kikao.

Sehemu ya watumishi wakifuatilia kikao.


Sehemu nyingine ya watumishi wakifuatilia kikao.

===============================================
Wakati huo huo uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umetumia fursa hiyo kutoa zawadi kwa Idara na vitengo vilivyofanya vizuri kwa kipindi cha mwaka 2016.

Balozi Mbelwa Kairuki akionyesha zawadi mara baada ya kukabidhiwa na Waziri Mahiga. 

Mkurugenzi wa Idara ya Siasa, Ulinzi na Usalama Bw. Mbundi akipokea zawadi ya Idara ya zilizofanya vizuri. Pamoja na Idara hizo Idara nyingine zilizoingia tano bora ni pamoja na Idara ya Amerika na Ulaya, Idara ya Afrika na Kitengo cha Fedha na Uhasibu.

Mfano wa Zawadi iliyokabidhiwa kwa Idara na vitengo vilivyoshinda na kuingia katika tano bora.

Kikao kikiendelea.


Waziri Mahiga apokea mchango wa maafa kutoka ubalozi wa Korea

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi, Dkt. Augustine Mahiga akihutubia katika hafla ya makabidhiano ya mchango uliotolewa na Ubalozi wa Korea kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Kagera mwezi Septemba, 2016 na kusababisha madhara makubwa, Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere.Kushoto ni Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini, Mhe.Song Geum Young

Waziri Mahiha akipokea mfano wa hundi yenye thamani ya Dola za Marekani elf 50 (shillingi millioni 108) kutoka kwa Balozi wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Song.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali na Msemaji wa Wizara ya Mambo y Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Mindi Kasiga akiratibu hafla hiyo.

Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia hafla ya makabidhiano, Kutoka kushoto ni Bw. Halmenshi Lunyumbu, Bw. Assah Mwambene, Bw. Ally Kondo na Bw. Freddy Maro.

Hafla ya makabidhiano ikiendelea.
Picha ya pamoja.

Wakiaga mara baada ya makabidhiano

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri Mahiga apokea Dola elf 50,000 kwa ajili ya Waathirika wa Kagera

Serikali ya Jamhuri ya Korea imetoa msaada wa Dola za Marekani elf 50,000 takribani milioni 108 kwa fedha za Tanzania kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lilitokea mkoani Kagera mwezi Septemba 2016.
Msaada huo ulikabidhiwa leo jijini Dar es Salaam na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Mhe. Song Geum Young na kupokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga (Mb) kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).
Baada ya kupokea msaada huo, Dkt. Mahiga aliishukuru Serikali ya Korea na kuahidi kuwa msaada huo ataukabidhi kwa Mhe. Waziri Mkuu ili uweze kutumika kama ulivyokusudiwa.
Mhe. Mahiga alisema kuwa Korea imekuwa mbia mkubwa wa Tanzania tokea nchi hiyo ilipoanzisha mahusiano ya kidiplomasia na Tanznaia miaka 25 iliyopita. Alieleza kuwa katika kipindi hicho Tanzania imekuwa ikipokea misaada mbalimbali ya kiuchumi, kijamii na ya kibinadamu  ukiwemo huu wa leo ulioelekezwa kwa waathirika wa tetemeko la ardhi la mkoani Kagera.
Mhe. Waziri alitaja misaada ambayo Korea imeipatia Tanzania ni pamoja na ujenzi wa daraja la Malagarasi mkoani Kigoma, ujenzi wa hospitali ya kisasa ya Mloganzila na ujenzi wa hospitali ya uchunguzi wa afya ya Mama iliyopo Chanika. Aidha, Korea hivi karibuni itaanza ujenzi wa daraja la Selander ambalo linatarajiwa kuanzia ufukwe wa Coco, Oysterbay hadi maeneo ya hospitali ya Aga Khan, Upanga jijini Dar es Salaam.
Waziri Mahiga alibainisha pia kuwa  Jamhuri ya Korea itatoa msaada mkubwa zaidi wa maendeleo kwa Tanzania kuliko nchi yeyote ya Afrika. Taarifa hiyo ilitolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Yun Byung-se alipofanya naye mazungumzo kando ya Mkutano wa nchi za Afrika na Korea  uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia tarehe 06 na 07 Desemba 2016.
Kwa upande wake, Balozi wa Korea nchini aliahidi kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania hususan kutoa misaada ya maendeleo ili iweze kutimiza azima ya Serikali ya awamu ya tano ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.

  Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 27 Desemba  2016.



Wednesday, December 21, 2016

Kikao cha Kwanza cha Tume ya Ushirikiano kati ya Tanzania na UAE chafanyika Abu Dhabi





Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Balozi Augustine Mahiga (kushoto) kwa pamoja na  Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wakisaini  Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga. Mkataba huo ulisainiwa wakati wa kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi, Falme za Kiarabu tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Masharika, Balozi Ramadhan Muombwa Mwinyi (kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Uchumi na Biashara wa Wizara ya Mambo ya Nje ya UAE wakiwekeana saini baadhi ya makubaliano yaliyoafikiwa.
Mhe. Dkt. Mahiga na ujumbe alioongozana nao wakiwa katika kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano na ujumbe wa UAE kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.


Mratibu wa Mkutano kwa upande wa Serikali ya Tanzania kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Hangi Mgaka akifuatilia mkutano.


Picha ya pamoja ya ujumbe wa Tanzania na UAE mara baada ya kukamilisha kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kilichofanyika Abu Dhabi tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.




TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TANZANIA NA UMOJA WA FALME ZA KIARABU ZAFANYA MKUTANO WA KWANZA TUME YA PAMOJA YA KUDUMU YA USHIRIKIANO HUKO ABU DHABI. 

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) zimefanya kikao cha kwanza cha Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano huko Abu Dhabi makao makuu ya Umoja wa Falme za Kiarabu.  Kikao hicho kilifanyika tarehe 19 na 20, Desemba, 2016.

Mkutano huo ulioshirikisha sekta mbalimbali za Serikali zote mbili uliongozwa na Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (MP), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania na Mhe. Reem Ebrahim Al Hashimy, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Ushirikiano wa Kimataifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). 

Pamoja na mambo mengine, katika mkutano huo Tanzania na UAE zimekubaliana kushirikiana kwenye masuala ya Kidiplomasia; Uchumi; Utalii; Nishati; Kilimo; Sayansi na Teknolojia; Usafirishaji; Miundombinu; Ulinzi na Usalama; Elimu pamoja na Kazi na Ajira. 

Sambamba na mkutano huo, Tanzania na UAE zimesaini Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Anga (Bilateral Air Service Agreement-BASA) na Mkataba wa Ushirikiano katika Sekta ya Utalii. Vilevile Serikali zote mbili zimekubaliana kukamilisha na kusaini Mkataba wa Kutotoza Kodi Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji wa Kodi za Mapato; Mkataba wa Kuhamasisha na Kulinda Uwekezaji; pamoja na ushirikiano katika sekta ya Elimu, Afya, Ulinzi na Usalama, Ushirikiano katika Usafiri wa Majini,  Kazi na Ajira pamoja ushirikiano katika masuala ya Zimamoto na Uokoaji. 

Mkutano huo umekuwa ni chachu katika mahusiano ya kihistoria ya nchi hizi mbili ambapo umeweka mazingira rasmi ya ushirikiano sio tu kwa Serikali bali pia kwa sekta binafsi. 

Mheshimiwa Waziri Mahiga katika hotuba yake ya ufungaji alitoa wito kwa Jumuiya za Wafanyabiashara na sekta binafsi kwa ujumla za Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu kuchangamkia fursa zinazopatikana katika nchi hizi mbili kuafuatia mkutano huo.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 21 Desemba, 2016.