TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Ziara
ya Rais wa Uturuki nchini Tanzania
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amemshukuru Rais wa Jamhuri
ya Uturuki, Mhe. Recep Tayip Erdogan kwa kuichagua Tanzania kuwa nchi ya kwanza
kuitembelea katika mpango wake wa kuzitembelea nchi za Afrika. Kauli hiyo imetolewa
leo na Mhe. Rais Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa anaongea na
waandishi wa habari pamoja na mgeni wake huyo.
Rais Magufuli
alimuhakikishia, Rais Erdogan kuwa Tanzania ipo tayari kushirikiana na Uturuki
na ana matumaini kuwa kufunguliwa kwa Ubalozi wa Tanzania nchini humo kutakuza
mahusiano zaidi ya kibiashara ambapo kwa takwimu zilizopo zinaonesha kuwa
biashara kati ya nchi hizi mbili imekua kutoka Dola za Marekani milioni 66
mwaka 2011 na kufikia Dola milioni 190 mwaka 2016.
Aidha, Rais alielezea matumaini
yake kuwa ziara ya Rais Erdogan nchini, itaongeza uwekezaji kutoka Uturuki
ambapo kwa sasa takribani makampuni 30 yenye thamani ya Dola za Marekani
milioni 305 ambayo yameajiri watu 2,959 yapo nchini.
Rais Magufuli na Mgeni
wake walishuhudia uwekaji saini wa Mikataba 9 ya ushirikiano kati ya nchi hizo
mbili katika maeneo mbalimbali kama vile, viwanda, utalii, usafiri wa anga,
utangazaji, elimu, utafiti, ulinzi na afya. Uwekaji saini wa mikataba hiyo
utaimarisha ushirikiano na utasaidia pia kufikia azma ya Serikali ya kuifanya
kuwa nchi ya viwanda kutokana na teknolojia kubwa iliyofikiwa na Uturuki.
Rais Magufuli alieleza
kuwa mojawapo ya kampuni zilizoomba zabuni ya kujenga reli ya kati ni kampuni
kutoka Uturuki hivyo, amemuomba Rais Erdogan kuwa endapo kampuni hiyo itashinda
zabuni, Benki ya Exim ya Uturuki itoe
mkopo kwa ajili ya ujenzi wa sehemu ya reli hiyo ambayo ina urefu wa zaidi ya
kilomita 400.
Kwa upande wake, Rais wa
Uturuki aliahidi kushirikiana na Tanzania kukuza uwekezaji na biashara ambapo
alisisitiza umuhimu wa kukuza kiwango cha biashara angalau kifikie Dola milioni
500 kwa mwaka.
Aidha, Rais Erdogan
alielezea tukio la jaribio la mapinduzi dhidi ya Serikali yake lililofanywa na
kikundi cha Fethulla tarehe 15 Julai 2016 ambalo lilisababisha vifo vya watu
240 na maelfu ya majeruhi nchini humo. Alisema wafuasi wa kikundi hicho
kilichopanga jaribio hilo wamesambaa hadi katika nchi za Afrika, hivyo, aliomba
viongozi wa nchi za Afrika kushirikiana naye katika kukabiliana nao ili kujihakikishia amani kwa ajili ya
maendeleo ya kiuchumi.
Rais wa Uturuki
alihitimisha mazungumzo yake kwa kumuomba Rais Magufuli azuru nchini Uturuki
wakati wa ufunguzi wa Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania nchini humo ambapo Mhe.
Prof. Elizabeth Kiondo ameteuliwa kuwa Balozi wa kwanza.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
23 Januari 2017.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.