TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Watanzania
waliokuwa wanashikiliwa nchini Malawi waachiwa huru
Mahakama Kuu ya Mzuzu
nchini Malawi jana tarehe 12 Aprili 2017 iliwaachia huru Watanzania wanane waliokuwa
wanashikiliwa nchini humo kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi
wa urani wa Kayerekera.
Hakimu Mkazi Mkuu wa
Mahakama ya Mzuzu, Bw. Texious Masoamphambe alitoa hukumu ya kifungo cha mwezi
mmoja kwa kosa la kuingia kinyume cha sheria kwenye mgodi wa urani wa
Kayerekera (trespass) na kifungo cha miezi mitatu kwa kosa la kufanya ujasusi (reconnaissance).
Makosa hayo mawili, kifungo chake kinakwenda
pamoja na kwa mujibu wa Hakimu huyo watuhumiwa tayari wameshatumikia kifungo
hicho na kuamuru waachiliwe huru. Aidha, Hakimu aliamuru Wizara ya Mambo ya
Ndani na Usalama wa Ndani kuhakikisha kuwa Watanzania hao wanasafirishwa na
kurejeshwa makwao haraka iwezekanavyo.
Kwa mujibu wa taarifa
kutoka Ubalozi wa Tanzania nchini Malawi, Watanzania hao wamesafirishwa leo
tarehe 13 Aprili 2017, kutoka Mzuzu hadi Mpaka wa Songwe/Kasumulu kati ya Tanzania
na Malawi.
Watanzania hao ambao ni Walasa
Mwasangu, 30, Binto Materinus, 32, Ashura Yasiri, 63, Christian Msoli, 38,
Layinali Kumba, 47, Maliyu Mkobe, Gilbert Mahumdi, 32, na Martin Jodomusole, 25
walikuwa wamekamatwa na kushikiliwa na vyombo vya usalama vya Malawi tokea
tarehe 20 Desemba 2016.
Imetolewa na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar
es Salaam,
13 Aprili 2017.