TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Tanzania na Afrika Kusini za dhamiria kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi.
Wataalamu wa Tanzania na Afrika Kusini wapo katika mkutano wa siku nne wa kuandaa mpango bora wa kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi hizo.
Mkutano huo unaojulikana kama Tume ya Ushirikiano ya Marais (Bi-National Commission-BNC) umefunguliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Aziz Mlima jijini Dar Es Salaam leo.
“Mkutano huu ni muhimu sana kwa kuwa licha ya nchi zetu kuwa na uhusiano na ushirikiano mzuri tokea enzi za ubaguzi wa rangi, lakini bado utakuwa chachu ya kuimarisha na kuharakisha ushirikiano wa kiuchumi na kijamii katika maeneo tutakayokubaliana na wenzetu” Balozi Mlima alisema.
Balozi Mlima alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini zilikubaliana kuanzisha Tume ya Marais ya Uchumi (Presidential Economic Commission-PEC) mwaka 2005 na mwaka 2011 nchi hizo zilisaini BNC ambayo ilichukuwa nafasi ya PEC. Tokea uwekaji saini wa makubaliano hayo, chombo hicho hakikuweza kukutana licha ya kuwa, makubaliano hayo ndiyo yatakuwa mwongozo katika majadiliano yatakayoendelea hadi tarehe 11 Mei 2017.
Kwa mujibu wa Balozi Mlima, uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaendelea kuimarika kadri siku zinavyokwenda. Kwa takwimu zilizopo takribani makampuni 226 ya Afrika Kusini yamewekeza nchini mtaji wa jumla ya Dola za Marekani milioni 803.15 na kuajiri zaidi ya watu 20,917. Alisema idadi ya makampuni inaweza kuongezeka kwani kuna makampuni mengi mapya kutoka Afrika Kusini yameshaonesha dhamira ya kuwekeza nchini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Afrika Kusini, Bw. Edward Makaya alieleza kuwa Tanzania na Afrika Kusini hazijafanya vya kutosha kwenye ushirikiano wa kiuchumi na kijamii. Alisema hadi wakati huu nchi hizo zimesaini makubaliano na mikataba takribani 14 ambayo ni michache ukilinganisha na urafiki na udugu uliopo baina ya nchi hizo.
Hivyo, alisistiza umuhimu wa kikao hicho kufanya majadiliano yatakayowezesha uwekaji saini wa mikataba mingi zaidi. Alisisitiza umuhimu wa mikataba hiyo kuzingatia maslahi ya pande zote.
-Mwisho-
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 08 Mei, 2017
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.