Taarifa ya
Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya kuhusu utekelezaji wa maamuzi ya
Wakuu wa Nchi Mhe. Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania na Mhe. Rais Uhuru
Kenyatta wa Jamhuri Kenya
Itakumbukwa kuwa tarehe 28 Juni, 2017
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitoa taarifa kwa umma kuhusu
vikwazo vya kibiashara ambavyo nchi ya Kenya iliweka katika baadhi ya bidhaa
kwa kipindi cha hivi karibuni. Katika taarifa ile, Serikali ya Tanzania
ilibainisha dhamira yake ya kufanya mazungumzo na Serikali ya Kenya kwa lengo
la kumaliza tofauti hizo za kibiashara baina ya nchi hizi mbili kwa kuzingatia
taratibu za kibiashara tulizokubaliana katika Jumuiya yetu ya Afrika ya
Mashariki.
Bidhaa za Tanzania
ambazo ziliwekewa vikwazo na nchi ya Kenya ni unga wa ngano pamoja na gesi ya
kupikia (LPG). Aidha, juhudi za awali za Serikali ya Tanzania kuona vikwazo hivyo
vinaondelewa na Serikali ya Kenya kwa wakati hazikuzaa matunda. Hali hiyo
ilipelekea Serikali ya Tanzania nayo kuchukua hatua.
Kwa kuzingatia
mahusiano mazuri ya kindugu yaliyopo kati ya nchi zetu mbili na kwa kujali
manufaa mapana ya Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, Viongozi Wakuu wa nchi hizi
mbili Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Jamhuri ya Kenya walizungumza
na kukubaliana kuondoleana vikwazo hivyo maramoja, Vikwazo hivyo ni;
1. Serikali ya
Kenya kuondoa vikwazo kwa bidhaa za unga wa ngano na gesi ya kupikia (LPG)
kutoka Tanzania.
2. Serikali ya
Tanzania kuondoa vikwazo kwa bidhaa za maziwa zinazozalishwa nchini Kenya.
3. Serikali za
Kenya na Tanzania kuondeleana vikwazo vyovyote vile ambavyo vinaweza kuathiri
biashara ya bidhaa na huduma kati ya nchi zetu mbili.
4. Sigara ni kati
ya mambo yaliyojadiliwa. Hata hiyo utekelezaji wake utafuata taratibu za ndani
Hivyo, Viongozi Wakuu
wa nchi zetu mbili waliwaelekeza Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi wa Tanzania na
Kenya, Mhe. Dkt. Augustine Philip Mahiga (Mb) na Dkt. Amina Mohammed, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Kenya kuutarifu umma
kwamba pande zote mbili zimekubaliana kumaliza tofauti hizo za kibiashara
zilizojitokeza hapo awali.
Katika
kutekeleza hilo, Mhe. Waziri Dkt. Amina Mohamed alimwalika Mhe.Waziri Dkt.
Mahiga nchini Kenya tarehe 23 Julai, 2017 ambapo walifanya Mkutano wa Pamoja na
waandishi wa habari kuutangaza uamuzi wa Viongozi Wakuu wa Kenya na Tanzania
kuondoleana vikwazo hivyo maramoja.
Kufuatia makubaliano
haya ya pamoja kati ya nchi hizi majirani ambazo ni waasisi wa Jumuiya ya
Afrika Mashariki, pia, tunapenda kutaarifu kwamba Mataifa haya mawili
yamekubaliana kuunda Tume ya Pamoja ambayo itakuwa na jukumu la kuepusha
tofauti za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya pamoja na kutolea ufumbuzi
changamoto za kibiashara kati ya nchi hizi mbili pindi zinapojitokeza. Tume hii
itaongozwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Kenya na kujumuisha
Mawaziri wanaohusika na masuala yaJumuiya ya Afrika Mashariki, Biashara, Fedha,
Mambo ya Ndani ya Nchi, Kilimo, Uchukuzi na Utalii wa nchi zote mbili.
Vilevile, Mawaziri
hawa wataunda mfumo wa kupeana taarifa mara kwa mara kuhusu masuala yenye
changamoto za kibiashara kwa lengo la kuepusha kujirudia kwa tofauti kama hizi.
Ni matarajio yetu kuwa uamuzi huu wa pamoja utakuza zaidi mahusiano ya
kibiashara baina ya nchi hizi mbili. Aidha, tunapenda kuwashukuru
wafanyabiashara wa nchi zetu mbili kwa uvumulivu.
Imetolewa
na:
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es
Salaam, 24 Julai, 2017
MASWALI NA MAJIBU BAADA YA TAARIFA YA MSINGI
SWALI: Je ni kwa nini Kenya waliweka vikwazo hivyo
hapo awali?
JIBU:
Sababu za awali zilizotolewa na Serikali ya Kenya zilidai kwamba bidhaa hizo
hazikidhi viwango vya ubora wa kimataifa. Hata hivyo, Wataalamu wa Tanzania wameihakikishia
Kenya kuwa bidhaa za unga wa ngano kutoka Tanzania zina ubora unaokubalika Kimataifa na huuzwa nchi nyingine
za Jumuiya ya afrika Mashariki na Afrika ya Kati. Halikadhalika bidhaa ya gesi
ya kupikia (LPG) inakidhi viwango vya ubora vya Kimataifa
.
SWALI: Nini msimamo wa Serikali ya
Tanzania kuhusu tuhuma za baadhi ya wanasiasa wa Kenya na baadhi ya vyombo vya
habari kuhusu Tanzania kuingilia uchaguzi wa Kenya.
JIBU: Tuhuma
hizi hazina ukweli wowote, na hata nilipokuwa nchini Kenya juzi niliona zimeripotiwa tena na
vyombo vya habari vya Kenya. Naomba nikanushe tena kwa mara nyingine, kwa niaba
ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, haijawahi, na wala haifikirii
kuingilia maswala ya ndani ya nchi nyingine tunazoshirikiana nazo ikiwemo
maswala ya uchaguzi. Hatujawahi kuingilia uchanguzi wa Kenya na hututegemei
kufanya hivyo kwenye uchaguzi huu na chaguzi nyingine zozote. Naomba waandishi
wa habari, kabla ya kuandika taarifa hizi, wazihakiki mara mbili, na watutafute
kutoa ufafanuzi kabla ya kuwapelekea wananchi taarifa hizi za kupotosha. Natoa
rai, tuwe waangalifu na walaghai wa nje wanaotaka kutugombanisha. Nichukue pia fursa
hii kuwatakia wananchi wa Kenya uchaguzi mwema wa amani na huru.
SWALI: Je ni kwanini Tanzania inaonekana kuweka
vizingiti vingi vya kibiashara ikilinganishwa na nchi nyingine kwenye ukanda wa
Afrika Mashariki na Afrika ya kati kwenye siku za hivi karibuni? Je hii
haitakwaza ukuaji wetu wa uchumi kama nchi?
JIBU: Hapana,
hata kidogo. Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira wezeshi ya
biashara ili kuwezesha uchumi wa nchi kukua na kuendelea, kutokana na biashara
ndani ya bara la Afrika na hususan ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati.
Tanzania kwa siku za hivi karibuni chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya Tano,
Mhe. John Joseph Pombe Magufuli, imefanya mageuzi makubwa kwenye taasisi zetu
za bandari na ushuru yaani TRA. Hatua hizi zinalenga kwenye kuziba mianya
iliyokuwepo huko nyuma ambayo ilisababisha ukusanywaji hafifu wa mapato. Ni
wazi sasa mambo yanaenda kwa uwazi zaidi na ushuru unatozwa na kukusanywa kwa
wakati. Tuna hakika sasa changamoto hizi zimepungua na nchi jirani zitaendelea kufanya
biashara na sisi bila vikwazo.
SWALI: Kabla ya kuunda hii kamati ya
kutatua changamoto zilizojitokeza hivi karibuni, Jumuiya ya Afrika Mashariki
imekua ikitatua vipi changamoto kama hizi za kibiashara hususan kwenye nchi
zenye ushindani mkubwa kama Kenya na Tanzania?
JIBU: Jumuiya
ya Afrika Mashariki imejiwekea misingi imara na muhimu ya kutatua changamoto
pindi zinapojitokeza. Hivyo ukiacha jopo la wataalam wa Serikalini kuna Baraza
la Mawaziri wa Biashara wa Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki ambao pia huweza kupendekeza ufumbuzi wa
changamoto mbalimbali kwa wakuu wa nchi ili kutatua changamoto hizi. Lakini
kutokana na ukaribu uliopo baina ya Tanzania na Kenya, hili la sasa tumelitatua
kwa haraka na kwenda mbele zaidi kuunda tume ya mawaziri wa nchi zetu mbili ili
huko baadae tuweze kutatua masuala kama haya mapema sana kabla ya kuathiri
biashara kati ya nchi zetu mbili.
Ni dhahiri kwamba nchi zetu mbili ni jirani na tunalindwa na
Itifaki za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki, lakini pia tuna ushindani kati
yetu. Na ili tupate maendeleo ni lazima kuweka ushindani wenye tija kwa manufaa
ya ukanda wetu na wananchi wetu. Japo kuwa Kenya ipo kwenye kundi la nchi zenye
kipato cha kati, uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi kubwa na ni hali ya kawaida
kwa changamoto kama hizi kujitokeza pindi nchi zinapokuwa katika ushindani wa
kiuchumi.Kwa namna ya pekee naomba kusifu tena hekima za Viongozi wetu wa Juu
kwa kutatua changamoto hizi kwa wakati.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.