WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA COMORO
Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro,
Mhe. Sylvester M. Mabumba alipokea ujumbe wa Clouds Media Group uliowasili
visiwani humo tarehe tarehe 20 Januari
2017 kwa ziara maalumu ya siku tatu ikiwa na lengo la kushirikiana na Ubalozi
kuzitangaza fursa mbalimbali zinazopatikana Visiwani humo kwa Watanzania.
Ujumbe huo wa Clouds Media Group ukiongozwa na Mkurugenzi wa
vipindi na uzalishaji, Bw. Ruge Mutahaba uliwasili Comoro kufuatia mualiko wa
Ubalozi wa Tanzania hapa Comoro ambapo lengo lake lilikuwa ni kuja kufanya
tathamini ya kuzindua Jukwa la Fursa (FURSA EXPO) Visiwani Comoro kama sehemu
ya kuendeleza kampeni za kuwapatia vijana wa Kitanzania taarifa muhimu kuhusiana
na fursa za uwekezaji na biashara.
Ubalozi wa Tanzania Visiwani Comoro kwa kushirikiana na Ujumbe
wa Clouds Media Group umelenga ifikapo mwezi Aprili 2018 kupanua mianya ya
uwekezaji nchini Comoro pamoja na kuhakikisha kwamba masoko ya uhakika
yanapatikana kwa ajili ya bidhaa za Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo
Uchumi wa Tanzania unaelekea kuwa ni uchumi wa Viwanda.
Aidha, Mhe. Balozi akiwa ameambatana na ujumbe wa Clouds
Media Group alipata fursa ya kuonana na kufanya mazungumzo na wadau kutoka
sekta mbalimbali za Serikali ya Comoro, Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi. “Serikali
ya Tanzania itaendelea kufungua maeneo mapya ya ushirikiano sambamba na kuhakikisha
vijana wananufaika na ushirikiano baina ya nchi na nchi ulioanzishwa na mataifa
yao” alisema Mhe. Balozi
Aidha, Mhe. Balozi alielezea anataraji ziara hiyo italeta
matokeo chanya na kwamba kuzinduliwa kwa jukwaa la FURSA EXPO ni sehemu mojawapo
ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo inalenga kwenye Diplomasia ya
Uchumi na kwamba kupitia jukwaa hilo bidhaa za Tanzania zinauhakika wa kuingia
kwenye Soko la Comoro kwani nchi ya Comoro inaitegemea Tanzania kwa kiasi
kikubwa katika mahitaji yake mbalimbali.
Pia ujumbe wa Clouds Media Group ulitumia nafasi hiyo
kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji Visiwani Comoro, Ndg. Said Mohamed Omar, Mkurugenzi Mkuu Ofisi
ya Kitaifa ya Utalii, Ndg. Mouzamildine
Youssouf pamoja na Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Vijana. Katika mazungumzo
hayo, wajumbe walionesha nia ya kutaka kushirikiana kwa pamoja katika kuendesha
kampeni itakayoibua maeneo muhimu ya kimkakati ambayo Vijana wa Kitanzania na
wale wa KiComoro wanaweza kushirikiana.
Naye Bw. Ruge Mutahaba kwa upande wake alieleza kufurahishwa
na fursa mbalimbali zinazopatikana Comoro na kuahidi kuendelea kushirikiana na
Ubalozi wa Tanzania Visiwani hapa kuhakikisha kwamba FURSA EXPO Comoro
inafanikiwa na kuleta matokeo chanya kwa lengo la kuinua uchumi wa vijana wa
Kitanzania na wa KiComoro.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.