Monday, March 26, 2018

Taarifa kwa Vyombo vya Habari

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

TAARIFA YA UFAFANUZI KUHUSU RAIA WA TANZANIA NCHINI OMAN


Kuna kipande cha video kinasambaa mitandaoni kikiwa na maelezo kuwa raia wa Tanzania wanaoishi nchini Oman wamekusanyika ofisi ya Ubalozi kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso na adhabu kali wanazopata kutoka kwa mabosi wao.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, baada ya kutazama kipande hicho cha video iliwasiliana na Ubalozi wa Tanzania nchini Oman kwa madhumuni ya kujua usahihi wa jambo hilo.

Ubalozi ulitoa ufafanuzi kuwa uliandaa mkutano wa Watanzania wote wanaoishi Oman na ulipangwa kufanyika katika hoteli ya Golden Tulip jijini Muscat tarehe 23 Machi 2018. Matangazo ya mkutano huo yalitaka Watanzania watakaopenda kushiriki wajisajili kabla ya siku ya mkutano. Watanzania takriban 200 walijisajili na ubalozi ulifanya maandalizi ya ukumbi, vyakula na vinywaji kwa ajili ya watu 300 kwenye hoteli ya Golden Tulip.

Siku ya mkutano ilipowadia, Watanzania zaidi ya elfu moja walijitokeza na kusababisha ugumu wa kuendelea na mkutano kutokana na maandalizi yaliyofanywa yalilenga watu 300.

Kamati ya maandalizi ilipoona ukumbi umejaa na watu walio nje ni weng mara mbili zaidi ya watu waliokuwemo ndani ya ukumbi iliamua kufunga milango na kuwaomba waliochelewa warejee nyumbani.

Uamuzi huo haukuwafurahisha watu waliochelewa, hivyo walishinikiza waingizwe kwenye ukumbi wa mkutano, kitendo ambacho kiliashiria uwezekano wa kutokea vurugu kubwa.

Kutokana na uhalisia huo, Kamati ya maandalizi ambayo ilijumuisha pia viongozi wa Watanzania wanaoishi nchini humo ilishauriana na kuamua kuwa mkutano huo uahirishwe na maandalizi yaanze upya kwa madhumuni ya kupata ukumbi na huduma nyingine zitakazokidhi idadi kubwa ya watu.

Kutokana na ufafanuzi huo, Wizara inapenda kuufahamisha umma wa Watanzania kuwa kipande hicho cha video kimechukuliwa wakati Watanzania wanashinikiza kuingia kwenye ukumbi wa mkutano na sio kwamba wamekusanyika kwenye ofisi ya ubalozi wa Tanzania kushinikiza kurejeshwa nyumbani kutokana na mateso wanayoyapata.


-Mwisho-

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 26 Machi, 2018

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.