TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa kuhusu ziara ya Waziri wa Sheria wa Israel nchini
Waziri wa Sheria wa Israel, Mhe.
Ayelet Shaked atafanya ziara ya kikazi ya siku tatu nchini kuanzia tarehe 22
hadi 24 Aprili, 2018.
Akiwa nchini, Mhe. Waziri Shaked
ambaye anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara na wawakilishi wa makampuni kutoka Israel
atashiriki Kongamano la Tano la Biashara kati ya Tanzania na Israel
litakalofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
Jijini Dar es Salaam tarehe 23 na 24 Aprili, 2018.
Kongamano hilo ambalo linalenga
kuwakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Israel, litahusisha Sekta muhimu
katika ukuaji wa uchumi wa Tanzania ambazo ni pamoja na Kilimo, Viwanda, Afya,
Nishati na Utalii. Aidha, kupitia Kongamano hilo wafanyabiashara katika sekta
hizo watabadilishana mawazo baina yao pamoja na watendaji wa Serikali ili
kufikia malengo waliyopanga.
Kongamano hilo linaratibiwa na
Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) na
Kingdom Leadership Network Tanzania
(KLNT).
Pamoja na kushiriki katika
Kongamano hilo, Mhe. Waziri Shaked ameomba miadi ya kukutana na Viongozi
mbalimbali Serikalini akiwemo Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Prof. Palamagamba
Kabudi, Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Mhe. Dkt. Aderladus Kilangi.
Kabla ya kuhitimisha ziara hiyo, Mhe.
Shaked atakutana na vyombo vya habari tarehe 24 Aprili, 2018 kwa ajili kueleza mafanikio
ya ziara yake nchini. Mhe. Shaked na ujumbe wake wataondoka nchini siku
hiyohiyo kurejea Israel.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Aprili, 2018
-Mwisho-
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.