Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf Mkenda akiongea na wawakilishi kutoka kampuni ya Agricom Afrika Ltd walioshiriki maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya yanayoendelea katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta Jijini Nairobi, Kenya tarehe 27 Aprili 2018.
=======================================
Tanzania yajikita
kutumia fursa za soko la Afrika Mashariki.
Serikali ya Tanzania kupitia
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesisitiza kuendelea
kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali za Tanzania na Kenya ili
kuhakikisha bidhaa na mazao ya kilimo yanayozalishwa na wananchi yanapata soko
la kuaminika katika ukanda wa Afrika Mashariki hususan Kenya.
Hayo yamesemwa leo na Katibu
Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Adolf
Mkenda alipotembelea maonesho ya bidhaa za viwanda vya Tanzania nchini Kenya,
yaliyofunguliwa rasmi na Waziri wa Kilimo na Umwagiliaji, Mhe. Mwangi Kiunjuri
tarehe 25 April, 2018 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Kenyatta
(KICC) Jijini Nairobi, Kenya.
Maonesho hayo ni sehemu ya
maadhimisho ya Wiki ya Tanzania nchini Kenya ambayo imeambatana na maadhimisho
ya miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Kongamano la biashara kati
ya Tanzania na Kenya ambapo lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wafanyabiashara
wa mataifa hayo ili waweza kufanya makubaliano ya kibiashara, kupeana uzoefu na
kuwezesha bidhaa za viwanda vya Tanzania kupenyeza katika soko la Kenya kama
ambavyo bidhaa na huduma za wakenya zilivyoingia katika soko la Tanzania na
Afrika Mashariki kwa ujumla.
Aidha, aliongeza ushirikiano
huo utasaidia kukuza biashara na uwekezaji na hivyo kuongeza ajira, kuinua pato
la taifa na kipato cha mtu mmoja mmoja kwa lengo la kuboresha maisha ya
wananchi kwa ujumla. ‘’ Tanzania itaendelea kushirikiana na mataifa yote na
itaendelea kufata taratibu na kanuni za biashara zilizokubaliwa kimataifa”
alisema Prof. Mkenda
Vilevile Katibu Mkuu Wizara
ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji alipata fursa ya kutembelea maonesho hayo ya
bidhaa ambapo alisisitiza umuhimu wa
kuthamini bidhaa zetu na kwamba Serikali ya Tanzania na Kenya zitaendelea
kuimarisha undugu na mshikamano uliopo kama ilivyokubaliwa na marais wa
Tanzania na Kenya walipokutana Kampala, Uganda katika Mkutano wa 19 wa kawaida
wa Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo waliwataka
viongozi katika nchi zao kumaliza vikwazo vya kibiashara. “ Serikali itaendelea kuweka mazingira wezesha
kwa wafanyabiashara hivyo natoa rai kwa wafanyabiashara wote kufuata taratibu
na masharti katika kufanya biashara zao” alisema Prof. Ole Gabriel
Wiki ya Tanzania nchini
Kenya imeandaliwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kupitia ubalozi wake wa Nairobi, Kenya kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda,
Biashara na Uwekezaji (Bara), Wizara ya Viwanda na Biashara (Serikari ya
Mapinduzi Zanzibar), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade),
Taasisi ya Sekta Binafsi, Wafanyabiashara na wadau mbalimbali wa Tanzania ambao
walijitoa kwa hali mali katika kudhamini ili kufanikisha Wiki ya Tanzania
nchini Kenya.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.