TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MAHIGA AHITIMISHA ZIARA YAKE NCHINI NORWAY
ASISITIZA UWEKEZAJI WENYE TIJA
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga
amehitimisha ziara yake ya kikazi nchini Norway kwa mazungumzo na wafanyabiashara
huku akiwapa ujumbe mkuu wa kuwekeza Tanzania ambapo tayari kuna mazingira
mazuri ya uwekezaji.
Kwenye hotuba
yake kwa wanachama wa Umoja wa Wafanyabiashara wa Norway na Afrika (NABA), Mhe.
Mahiga ameelezea ushirikiano uliopo kati ya Serikali za Norway na Afrika kwa
ujumla hususan Tanzania, ambapo Norway inasaidiana na nchi nyingi za
kiafrika ikiwemo Tanzania katika
kutekeleza miradi ya maendeleo. Hii ni ishara nzuri kwa ukuaji wa biashara na
mahusiano.
Akitolea mfano
wa Tanzania, Mhe. Mahiga alisema kuwa miaka ya hivi karibuni Serikali ya Norway
imebadilisha ushirikiano wake na Tanzania kutoka kwenye kutoa misaada kwenda
kwenye udhamini wa pamoja wa miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kuinua
uchumi.
“Ushiriki wa
Serikali ya Norway nchini kwetu ni wa kipekee, kwani unazingatia vipaumbele na
sera za Tanzania na pale wanaongeza nguvu kwa kudhamini mafunzo na hatimaye
ujenzi wa mifumo sahihi ya utekelezaji wa sera hizo” Waziri Mahiga alisema.
Waziri Mahiga
aliongeza kuwa, kwenye awamu ya tano ya uongozi nchini Tanzania, Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na mambo
mengine, amejenga mifumo bora ya ukusanyaji kodi, usimamizi wa rasilimali za
umma pamoja na uendelezwaji wa rasilimali ya mafuta kwa maendeleo. “Serikali ya
Norway inadhamini maeneo yote hayo na mengine mengi, kama mdau wa maendeleo ya
Watanzania. Hivyo ni vyema na nyie wafanyabiashara muwekeze pale ambapo Serikali
yenu ipo. Kwa sababu hapo ndio mahali salama kwa uwekezaji wenye tija”
alihimiza Mhe. Mahiga.
Mkutano huo
uliojumuisha taasisi takriban 25, ulifanyika chini ya mwamvuli wa Norfund,
Taasisi inayojenga uwezo kwa wafanyabiashara kuendesha biashara kwenye nchi
zinazoendelea.
Akielezea
mikakati ya taasisi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wake, Bw. Kjell Roland alisema
Norfund inajikita zaidi kwenye nchi ambazo upatikanaji wa mitaji ni mgumu
kutokana na uchanga wa sekta binafsi.
Kwa upande
wake, Mratibu wa umoja huo wa Wafanyabiashara wa NABA, amesema kuwa wapo kwenye
maandalizi ya ziara ya biashara Tanzania kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Waziri Mahiga
alitumia fursa ya mkutano huo kumtambulisha Balozi wa Tanzania nchini Norway
mwenye makazi yake nchini Sweden, Mhe. Dkt. Wilbroad Slaa ambaye anatarajiwa
kukabidhi hati zake za utambulisho tarehe
21 Juni, 2018.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya
Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam, 21 Juni, 2018
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.