TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC)
zimejipanga kuzuia na kudhibiti madhara yanayosababishwa na machafuko ya
kisiasa katika jumuiya hiyo na Bara la Afrika kwa ujumla. Wawakilishi wa nchi
hizo wamekusanyika nchini Malawi kuanzia tarehe 1 Oktoba hadi 17 Oktoba 2018
kwa ajili ya kufanya mazoezi ya namna ya kutuliza ghasia pamoja na kutoa
misaada ya kibinadamu kwa waathirika katika kipindi cha machafuko
Wawakilishi wa Tanzania kutoka Jeshi la Wananchi, Magereza na
taasisi za kiraia ikiwemo Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki ni miongoni mwa watu 600 wanaoshiriki zoezi hilo lililopewa jina la
EX UMODZI CPX 2018 na kaulimbiu ya Afrika ni Amani na Maendeleo (Africa for
peace and prosperity).
Katika hafla ya ufunguzi wa mazoezi hayo iliyofanyika leo tarehe 08 Oktoba, 2018 katika
Chuo cha Kijeshi cha Malawi kilichopo mji wa Salima takriban kilomita 120
kutoka Lilongwe, Naibu Waziri wa Ulinzi wa Malawi, Mhe. Evaton Chemulirenji
alisema mazoezi hayo ni utekelezaji wa maazimio ya SADC na Umoja wa Afrika (AU)
wa kuandaa kikosi cha kukabiliana na machafuko barani Afrika (Standby Force-SF)
ambacho kinatakiwa kiwe kimekamilika ifikapo Januari 2019.
Alisema madhumuni ya mazoezi hayo ni kuhakikisha kuwa kikosi cha
SF kinapewa mafunzo ya vitendo ya kutosha ili kiwe na ujuzi na mbinu za
kushiriki operesheni za kulinda amani na/au kuingilia kati na kuzuia machafuko
(peace keeping and enforcement) pale yanapotokea barani Afrika. Aidha, alisema
mazoezi hayo ni muhimu kwa kuwa yatasaidia kuimarisha ushirikiano na kuaminiana
baina ya nchi wanachama wa SADC.
Mazoezi hayo yanajumuisha makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na
majeshi ya ulinzi, askari polisi, askari magereza na raia wa
fani tofauti kama vile za Utawala wa Sheria, siasa, mawasiliano, Utawala, haki
za binadamu na jinsia ambao wana mchango mkubwa katila masuala ya operesheni za
kulinda amani.
Wanajeshi watafanya zoezi la namna ya kutuliza machafuko na raia
watajifunza namna ya kusaidia jamii punde tu machafuko yanapodhibitiwa na
vikosi vya usalama.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki,
Salima,
Malawi
08 Oktoba 2018
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.