TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Dkt. Mahiga amwakilisha Rais katika Jukwaa
la Uchumi Duniani
Tanzania imesisitiza
umuhimu wa kukabili uhaba wa chakula kwa kuzalisha mazao kwa kutumia utalaamu
wa kisasa kwa kuwpatia wakulima pembejeo na masoko ya uhakika ya chakula cha
ziada.
Kauli hiyo ilitolewa
na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt.
Augustine Mahiga (Mb) wakati wa kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula
na changamoto za uhaba wa chakula duniani katika mkutano wa Jukwaa la Uchumi
Duniani (World Economic Forum-WEF) unaofanyika Davos, Uswisi kuanzia tarehe 22
hadi 25 Januari 2019.
Mhe. Mahiga
alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Joseph Magufuli katika jukwaa hilo ambalo kaulimbiu ya mwaka huu ni Kutengeneza Mazingira ya Utandawazi wa
Dunia kwa ajili ya Mapinduzi ya Kisasa ya Nne ya Viwanda “Shaping a Global Architecture in the Age of
the Fourth Industrial Revolution”.
Katika mkutano huo,
ajenda kuu zilizojadiliwa ni pamoja na Mapinduzi ya Nne ya Viwanda, Agenda ya
Afrika ya Maendeleo, Hali ya Ulinzi na Usalama Pembe ya Afrika, changamoto za biashara
ya kimataifa, ushirikiano wa Bara la Ulaya na Afrika katika ajenda mpya ya
maendeleo.
Tanzania ilialikwa
kuchangia mjadala unaohusu uhakika wa chakula na changamoto za uhaba wa chakula
duniani pamoja na ajenda ya uwezeshaji wa mawasiliano ya simu za mkononi. Katika
ajenda hiyo, Tanzania ilitoa wito wa umuhimu wa teknolojia katika kuboresha
utaalamu katika sekta ya kilimo kwa ajili ya kuwawezesha wakulima wadogo
waliopo vijijini.
Hili ni Jukwaa la
pekee ambalo linakutanisha kwa pamoja Viongozi wa Serikali kutoka mabara yote
duniani, Taasisi na Mashirika ya Kimataifa, Viongozi wa Makampuni Makubwa ya Kibiashara
kwa ajili ya kujadili maendeleo na mwelekeo wa uchumi duniani.
Kando ya Mkutano huo,
Mhe. Dkt. Mahiga alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa mashirika na
makampuni ambayo yapo Tanzania na yanayohitaji kupanua wigo kama vile Tigo na
General Electric na makampuni yanayotafuta fursa za kuwekeza Tanzania. Aidha,
alikutana na Rais wa WEF, Mhe. Borge Brende ambapo aliahidi kushawishi
wawekezaji kuwekeza Tanzania na kuandaa Jukwaa la wawekezaji wa kimataifa la
Tanzania ili waweze kuwekeza Tanzania.
Viongozi wengine
waliokutana na Waziri Mahiga ni pamoja na; Bw. Scott Strazik, Rais na
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Gesi yenye Makao makuu yake Atlanta, Georgia-
Marekani; Bw. Richard Hatchett, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kupambana na
magonjwa ya Mlipuko (Coalition for
Epidermic Preparedness Innovations); Bi. Rachel Samren, Makamu wa Rais wa
Kampuni ya Kimataifa ya Millicom ambayo TIGO ni Tawi la Kampuni hiyo, na Bw. Mohamed
Al-Beity, Mtanzania aliyetambuliwa na Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mradi wa
kutangaza Utalii wa Tanzania kwa njia ya Mtandao (Tanzania Digital Tourism).
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dodoma
26 Januari 2019
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.