Saturday, June 29, 2019

Sekta Binafsi zaaswa kuchangamkie Fursa katika Mkutano wa SADC

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt, Faraji Kasidi Mnyepe amekutana na kufanya mazungumzo na wawakilishi wa benki mbalimbali, wawakilishi wa kampuni za utalii, viongozi wa vyama vya wamiliki wa vyombo vya usafiri na wafanyabiashara mbalimbali jijini Dar Es Salaam. Katika Mkutano huo, Dkt. Mnyepe aliwasihi wawakilishi hao kujipanga vizuri ili waweze kuchangamkia fursa za Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika nchini Mwezi Agosti 2019. Aliwasihi kujipanga vizuri katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya usafiri, utalii, burdani na vyakula. Dkt. Mnyepe alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuendeleza utamaduni wa ukarimu na kuwa waaminifu na uadilifu katika kuhudumia ugeni huo mkubwa ambapo inakadiriwa zaidi ya watu elf moja watakuja nchini.
Sehemu ya washiriki wa mkutano huo. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya maandalizi ya Habari, Machapisho na Matangazo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bi. Zamaradi Kawawa. 

Ujumbe ulioshiriki kikao hicho ukisikiliza kwa makini maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Katibu Mkuu.
Mkutano ukiendelea.





Wednesday, June 26, 2019

Prof. Kabudi Ahudhuria Mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC)

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Nchi za Kiafrika zimeiomba China kuhakikisha kuwa ufadhili ama mikopo inayotoa kwa Nchi za Kiafrika inalenga katika miradi ya kikanda itakayoziunganisha na kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi huku Tanzania ikiitaka China kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo inayowekeza nchini iwe ya manufaa kwa pande zote mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ,Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) ameyasema hayo Beijing Nchini China katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) alipopata fursa ya kuzungumza katika mkutano huo na kuongeza kuwa endapo China itazisaidia kwa ufadhili ama kwa mikopo nafuu kuwekeza katika miradi hasa ya miundombinu itakayoziunganisha Nchi za kiafrika kwa kiasi kikubwa itazisaidia Nchi hizo kufanya biashara zenyewe kwa zenyewe  itaziwezesha kupiga hatua za kimaendeleo na kiuchumi na hivyo kujitegemea.

Ameongeza kuwa Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) umekuwa ni wa manufaa kwa kuwa Nchi zenyewe za kiafrika zimepata fursa ya kutaja baadhi ya miradi ya kipaumbele kutokana na uhitaji wa Nchi husika  huku akiitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji kwa kuwa Nchi nyingi za Kiafrika bado zina vyanzo vingi vya maji vinavyoweza kuzalisha umeme ambao utakuwa ni wa bei nafuu na kusaidia katika ujenzi wa viwanda.

Aidha, katika mkutano huo wa siku mbili uliozikutanisha Nchi zipatazo 53 za Kiafrika na China zimeitaka China pia kuhakikisha inasaidia ama kufadhili katika kuinua uwezo wa kitaaluma utakaowawezesha vijana kwa Kiafrika kujiajiri na kupata wataalam wabobezi katika masuala mbalimbali kutokana na uwekezaji hasa wa viwanda na miundombinu utakaofanywa kwa pamoja na China na Nchi za Kiafrika.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi (Mb) amesema katika mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Tanzania imesisitiza kuwa katika miradi ya uwekezaji ya misaada ama ile ya mikopo nafuu inayoelekezwa Tanzania iwe ni ile yenye manufaa kwa pande zote mbili yaani win-win situation kama anavyosisitiza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Rais wa China Mhe. Xi Jimping, Waziri wa Mambo ya Nje wa China Mhe. Wang Yi amesema kuwa China haitatoa misaada yenye masharti magumu kwa Nchi za Afrika, badala yake itaendeleza ushirikiano wake na Afrika katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo, Serikali ya China imeahidi kuongeza umoja na ushirikiano kati yake na Afrika katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na usalama  ili kuleta maendeleo endelevu kwa watu na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.

Mkutano huo wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika limeazimia kwa pamoja kutekeleza miradi ya kipaumbele kulingana na uhitaji wa kila nchi kwa kufuata hatua nane zilizotangazwa katika mkutano wa wakuu wa nchi wa FOCAC uliofanyika mwezi September 2018 jijini Beijing.

Hatua hizo ni pamoja na program ya kuendeleza viwanda kupitia ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda, ujenzi wa miundombinu ikiwemo nishati, reli, barabara na bandari, sambamba na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vitakavyosaidia kuzalisha nguvu kazi ya viwandani.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
BEIJING - CHINA.
25 Juni 2019



Meza kuu watatu kushoto ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ambaye ni mgeni wa heshima na Mkuu wa Nchi pekee kutoka Bara la Afrika akiwa katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika. Wa pili kushoto ni Waziri wa Mambo ya Nje China na Mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi. Mkutano huo umefanyika Beijing,China na Kuhudhuriwa na Mawaziri wa mambo ya Nje wa Nchi za Afrika 53. Juni 25, 2019.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof Palamagamba John Kabudi (Mb) (katikati) akifuatilia mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC),Beijing -  China. Juni 25,2019 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi(Mb.) (watano kutoka kushoto) akiwa katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaohudhuriwa na Mawaziri wa Mambo ya Nje 53 kutoka Nchi za Afrika. Mkutano huo unafanyika Beijing – China. Juni 25, 2019.




Sehemu ya Mawaziri wa mambo ya Nje kutoka Nchi 53 za Afrika wanaohudhuria mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).Mkutano huo unafanyika Beijing – China. Juni 25, 2019.


Monday, June 24, 2019

Prof. Kabudi akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China


 Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) na ujumbe wake akiwa kwenye mkutano pamoja na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa mambo ya nje wa China na na Mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi na ujumbe wake. Mkutano huo umefanyika Beijing,China. June 24, 2019.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiteta na mwenyeji wake ambaye ni Waziri wa mambo ya nje wa China na na Mjumbe wa Baraza la Taifa Mhe. Wang Yi na ujumbe wake mara baada ya kumaliza mkutano baina yao. Mkutano huo umefanyika Beijing,China. June 24, 2019.
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi  (Mb) akisaini mkataba wa msaada wa shilingi bilioni sitini bila ya masharti yeyote pembeni yake ni Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Bw. Zhou Liujun,akisaini kwa niaba ya serikali ya China. Zoezi hilo limefanyika Beijing,China. June 24, 2019.

Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi  (Mb) akibadilishana nyaraka na Makamu Mwenyekiti wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo la China Bw. Zhou Liujun, mara baada ya kusaini nyaraka hizo. Zoezi hilo limefanyika Beijing, China. June 24, 2019.


Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi  (Mb) akiwa katika mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 53 za Afrika na taasisi za fedha za China.
 Sehemu ya mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na wajumbe wao waliohudhuria katika wamkutano wa mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi 53 za Afrika na taasisi za fedha za China. Beijing,China. June 24, 2019.
  




Dkt. Migiro apokea vifaa vya mafunzo ya utabibu vyenye thamani ya Tsh. milioni 130



Dodoma, 24 Juni 2019

Dkt. Migiro apokea vifaa vya mafunzo ya utabibu vyenye thamani ya Tsh. milioni 130

Ubalozi wa Tanzania nchini Uingereza ulipokea kifaa muhimu cha kufundishia madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wa sekta ya afya, pamoja na vitabu vya kitabibu kutoka katika Jumuiya ya Watanzania waishio Uingereza wanaofanya kazi katika sekta ya afya (Tanzania United Kingdom Health Diaspora Association - TUHEDA). Makabidhiano hayo yalifanyika jijini London tarehe 22 Juni 2019. 

Kifaa hicho ni sanamu ya binadamu ambayo inaendeshwa na programu maalumu za kompyuta zinazowezesha wataalamu mbalimbali wa afya kupata uhalisia wa hali ya magonjwa kama ambavyo wangeupata kutoka kwa mgonjwa aliye hai. 

Sanamu hiyo iliyopewa jina la ‘Msafiri’ na Ubalozi, ina uwezo wa kupumua, kutoa sauti ya mapafu kama mtu mwenye pumu, homa ya mapafu, au mapigo ya moyo yanayoweza kuashiria shinikizo la juu au la chini la damu, sawa na mgonjwa halisi. Upatikanaji wa sanamu hiyo umefanikishwa na mwanachama wa TUHEDA, Dkt. Nasibu Mwande, mtaalamu wa masuala ya ajali na magonjwa ya dharura (Accidents and Emergency), anayefanya kazi ya udaktari hapa Uingereza. 

‘Msafiri’ ana thamani ya pauni za Uingereza zisizopungua 30,000 (sawa na shilingi za Tanzania zipatazo milioni mia moja), ana umbo la kawaida la binadamu na uzito wa kilo 60. Ubalozi umetaarifiwa kuwa sanamu hiyo ni ya kwanza nchini Tanzania katika ufundishaji wa kitabibu.

Kupatikana kwa ‘Msafiri’ kutasaidia sana kupunguza makosa ya kibinadamu yanayoweza kufanywa na madaktari, wauguzi na wataalamu wengine kwani ‘Msafiri’ anaweza kutumika kutoa mafunzo ya kitabibu kwa mfano halisi wa magonjwa mbalimbali bila ya madhara ambayo yangetokea kama wataalamu wa utabibu wangetegemea kujifunza kupitia mgonjwa aliye hai. 

TUHEDA pia wamekabidhi vitabu muhimu mia tatu vinavyotumika kama rejea kwa madaktari wakati wa kuamua mgonjwa apewe dawa gani, dawa zipi zinaweza kutumika kwa pamoja bila madhara, na zitolewe kwa kiwango gani. Vitabu hivyo vina thamani inayokaribia pauni 9,000 sawa na shilingi za Tanzania zipatazo milioni 30.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,

Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Dkt. Asha-Rose Migiro akisikiliza mkoromo wa kifua cha ‘Msafiri’ kama mgonjwa halisi mwenye maambukizi kwenye mapafu. ‘Msafiri’ na vitabu hivi ni mchango mkubwa katika kazi za kitabibu nchini Tanzania.
Watanzania waishio Uingereza waliohudhuria mapokezi ya Msafiri na vitabu vya utabibu vilivyokabidhiwa na TUHEDA.

Sunday, June 23, 2019

PROF. KABUDI ZIARANI NCHINI CHINA

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwasili katika Ubalozi wa Tanzania Nchini China na kupokelewa na Balozi wa Tanzania Nchini China Balozi Mbelwa Brighton Kairuki. June 23,2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akisaini kitabu cha wageni katika ubalozi wa Tanzania Nchini China. June 23,2019.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akisaini kitabu cha wageni katika ubalozi wa Tanzania Nchini China. Mbele yake anayeshuhudia ni Balozi wa Tanzania Nchini China Balozi Mbelwa Brighton Kairuki. June 23,2019.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiwa katika kikao cha pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Nchini China. June 23,2019.




Friday, June 21, 2019

TANZANIA YANG’ARA KATIKA MAONESHO YA UTALII SEOUL, KOREA

Ubalozi wa Tanzania Seoul, kwa kushirikiana na wadau wa Utalii kutoka sekta binafsi wameshiriki katika maonyesho makubwa ya Kimataifa ya “Seoul International Tourism Industry Fair” yaliyofanyika jijini Seoul, Jamhuri ya Korea kuanzia tarehe 6 hadi 9 Juni 2019. Maonesho hayo yaliandaliwa na Korea World Travel Fair (KOTFA) kwa kushirikiana na Seoul International Travel Mart (Seoul Metropolitan City) ambapo wadau (kampuni za utalii, usafirishaji, wamiliki wa hoteli, migahawa, vyombo vya habari) kutoka nchi mbalimbali za Asia, Ulaya, Amerika, Afrika na Mashariki ya Kati walishiriki.

Kampuni za Utalii kutoka Tanzania zilizoshiriki maonesho hayo ni Eastenders, Zara Tours, Travel Booking Guide kwa kupitia Mwakilishi wake aliye Korea, Ms. Han Bitnarae, na SAFANTA Tours & Travel ya Zanzibar.

Kupitia maonesho hayo, Tanzania iliweza kutangaza vivutio vya utalii kwa jamii ya Wakorea na mataifa mengine kwa ujumla. Aidha, kampuni zilizoshiriki ziliweza kupata wenzao wa kushirikiana nao kibiashara kupitia B2B na kuingia makubaliano ya kibiashara.

Balozi wa Tanzania Korea Kusini, Mhe. Matilda Swilla Masuka akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Tanzania katika maonesho hayo, pamoja na wageni waliotembelea banda la Tanzania.
Picha ya pamoja kati ya washiriki wa Maonesho hayo ya Utalii, Wafanyakazi wa Ubalozi wa Tanzania Seoul, na Watanzania waishio Korea Kusini (Diaspora) ambao walikuja kuunga mkono juhudi hizo za kuitangaza Tanzania
Mwakilishi wa kampuni ya Zara Tours, Bi Leila Ansell akiongea na wateja kuhusu huduma mbalimbali zitolewazo na kampuni hiyo ambayo imeingia mkataba pia na kampuni ya kikorea ya Hyecho Trekking ambayo hupeleka watu kupanda mlima Kilimanjaro. Mazungumzo pia bado yanaendelea na makampuni mengine.   




Thursday, June 20, 2019

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe akimsikiliza Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani hapa Nchini Bi Janine S. Young  alipomwita Wizarani kutoa ufafanuzi kuhusu angalizo la kiusalama lilitolewa na ubalozi huo kupitia tovuti ya Ubalozi wa Marekani hapa Nchini. June 20,2019. 


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA YA MASHARIKI WAMWITA KAIMU BALOZI WA MAREKANI WIZARANI

Tarehe 19 June, 2019, Ubalozi wa Marekani Nchini Tanzania ulitoa taarifa katika mitandao ya kijamii “Twitter” kuhusu angalizo la kiusalama “security alert”. Angalizo hilo la kiusalama lilitokana na uvumi unaodaiwa na ubalozi huo kusambaa kuhusu uwezekano wa kutokea kwa shambulio katika baadhi ya maeneo ya jiji la Dar es Salaam.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki ulimwita katika ofisi ndogo za Wizara zilizopo Jijini Dar es Salaam, Kaimu Balozi wa Marekani Bi Janine S. Young ili kutoa ufafanuzi wa “twitter” yao. 

Ubalozi wa Marekani ulimtuma Mwakilishi wa Kaimu Balozi wa Marekani Bi. Janine S. Young kuonana na uongozi wa Wizara ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe.  

Bi Janine S. Young ameutambua ujumbe huo na kukiri kuwa  umetumwa na ubalozi wa Marekani hapa nchini.

Katika ufafanuzi wake amekiri kuwa Ubalozi umefanya makosa ya kutoa tetesi ambazo hazikuwalenga raia wa Marekani pekee bali raia wote wakitambua kuwa Ubalozi hauna mamlaka ya kufanya hivyo jambo lililosababisha taharuki kwa wananchi na wageni wanaotarajia kuitembelea Tanzania. 

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeukumbusha Ubalozi wa Marekani umuhimu wa kuzingatia sheria za nchi na taratibu za kidiplomasia zinazokubalika duniani kote katika utoaji wa taarifa za aina hii.

 Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dkt. Faraji Kasidi Mnyepe amewataka wananchi na Jumuiya za Kimataifa pamoja na wageni mbalimbali waliopo  nchini na wanaotarajia kuitembelea Tanzania kuendelea na shughuli zao kama kawaida kwani mpaka sasa hakuna taarifa yeyote iliyothibitishwa ya kuwepo kwa tishio la aina hiyo hapa nchini na kwamba Vyombo vya Ulinzi na Usalama vimejizatiti kukabiliana na matishio yeyote.


Imetolewa na:

Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar Es Salaam.
20 Juni, 2019



Wednesday, June 19, 2019

Wizara inaendelea kuhudumia wananchi Wiki ya Utumishi wa Umma

Bw. Hassan Mnondwa,  Mtumishi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akitoa ufafanuzi kwa Bw. Abdullatif kuhusu majukumu ya Wizara  alipofika kwenye Dawati la Wizara wakati wa kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma. Mwingine katika picha ni Mtumishi wa Wizara, Bi. Roxana Kagero. Katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ipo kwa mujibu wa Kalenda ya Umoja wa Afrika, Wizara imefungua madawati maalum kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi ikiwemo kusikiliza na kujibu hoja zao kuhusu Wizara pamoja na kueleza majukumu yanayotekelezwa na Wizara.
Mtumishi wa Wizara akimhudumia mgeni, Bi.Eunice Mmari kutoka Ofisi ya Kamishna wa Kazi aliyefika kwenye Dawati la Wizara katika Ofisi za Wizara zilizopo Chuo Kikuu cha Dodoma ikiwa ni maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyoanza tarehe 16 hadi 23 Juni 2019.
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Macha na Deogratius wakiwa tayari kuwapokea na kuwahudumia wadau mbalimbali wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma
Mtumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Jenipher akiwa kwenye dawati lililopo Ofisi za Wizara za Mtumba tayari kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika kuanzia tarehe 16 hadi 23 Juni 2019
Mtumishi wa Wizara akiwa tayari kwenye dawati lilopo Ofisi ya Mambo ya Nje Zanzibar kwa ajili ya kuwahudumia wananchi katika kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma

Tuesday, June 18, 2019

Waziri Kabudi akutana na Balozi Al - Mashaan

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) amekutana na kufanya mazungumzo na Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait anayeshughulikia masuala ya Afrika, Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan.

Pamoja na mambo mengine walizungumzia kuhusu jinsi ya kuboresha mahusiano yaliyopo katika kati ya Tanzania na Kuwait, nchi ya Kuwait imekuwa ni kati ya wadau muhimu wa Maendeleo hapa nchini kupitia mradi wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait(Kuwait Fund). 


Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi ndogo za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zilizopo jijini Dar es Salaam tarehe 18 Juni, 2019
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) akimwelezea jambo Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan
Balozi Mubarak Mohamed Al -Sehaijan pamoja na maafisa Ubalozi wa Kuwait nchini wakisikiliza kwa makini mazungumzo hayo kati ya Prof. Palamagamba John Kabudi na Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan (hawapo pichani)
Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan naye akimweleza jambo  Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.)
Sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wakifuatilia kwa makini mazungumzo hayo kati ya Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) na Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan (hawapo pichani)
Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) na Balozi Hamad Suliman Al - Mashaan, Balozi wa Kuwait nchini Mhe. Mubarak Mohamed AlSehaijan (wa pili kutoka kulia) pamoja na maafisa Ubalozi wa Kuwaiti na Afisa Mambo ya Nje Bw. Odilo Fidelis (wa pili kutoka kushoto)