Mhe. Balozi Luvanda akifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika hafla ya kutoa tuzo za utalii zilizotolewa na Jarida la "Outlook Traveller Magazine" na kufanyika katika Hoteli ya Rossette jijini New Delhi, India tarehe 22 Februari 2020. Tanzania iliibuka mshindi kwa kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani nchini India kwa mwaka 2020. ===============================================================
TANZANIA YASHINDA TUZO YA UTALII NCHINI INDIA
Tanzania imeshinda tuzo ya utalii kwa
kuonekana ni eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori duniani nchini India kwa
mwaka 2020 (The Best International
Wildlife Destination).
Balozi wa Tanzania nchini India Mhe.
Baraka H. Luvanda amepokea Tuzo hiyo kutoka Jarida la kihindi la “Outlook Traveller Magazine” katika hafla
maalum iliyofanyika katika Hoteli ya Roseate jijini New Delhi kwa niaba ya Tanzania. Hafla
hiyo ilihudhuriwa na takriban washiriki 200.
Tanzania imepata ushindi huo kutokana
na kura zilizopigwa kwenye mtandao wa jarida hilo la “Outlook Traveller” lililoshirikisha
wapiga kura 1,200,000 kwa njia ya mtandao.
Hii ni mara ya kwanza kwa Tanzania
kushinda tuzo hiyo ambayo hutolewa kila mwaka nchini India, washiriki kupitia
jarida hilo wameichagua Tanzania kama eneo bora zaidi la utalii wa wanyamapori
duniani.
Aidha, Shelisheli na Indonesia kwa
pamoja zilishinda tuzo kama maeneo bora zaidi duniani kwenye utalii wa fukwe.
The Outlook Traveller Award ni tuzo ya kifahari zaidi katika
sekta ya utalii nchini India na hutolewa na Jarida la Utalii la “Outlook Traveller Magazine” ambalo ni
jarida namba moja nchini India linalojishughulisha kutangaza utalii, ndani na
nje ya India.
Wakati akipokea tuzo hiyo, pamoja na
mambo mengine Balozi Luvanda aliushukuru uongozi wa Jarida hilo kwa kuandaa
tuzo hizo muhimu ambazo zinasaidia kutanganza utalii wa nchi mbalimbali nchini
India na akaeleza kuwa kupitia tuzo hiyo, watu wengi zaidi wataijua Tanzania na
vivutio vingi vya utalii vilivyopo nchini na kuwavutia kutembelea Tanzania.
Mafanikio hayo yanatokana na jitihada
zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kupitia Ubalozi wa Tanzania nchini India,
Wizara za Utalii za Tanzania Bara na Zanzibar, na Taasisi zote zinazosimamia
masuala ya utalii za ndani na nje ya nchi katika kutangaza vivutio vya utalii
kwa nchi mbalimbali duniani ikiwemo India.
Kupitia juhudi hizi, idadi ya watalii
wanaokuja Tanzania kutoka India imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa
mfano, idadi hiyo iliongezeka kutoka watalii 39,115 mwaka 2016 hadi watalii
69,876 mwaka 2017.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kupitia Balozi zake ukiwemo Ubalozi wa Tanzania nchini India na wadau wengine
itaendelea kuongeza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania ili
kuhakikisha idadi ya watalii kutoka India na nchi zingine duniani inaongezeka.
Hii ni pamoja na kutumia Shirika la Ndege la Tanzania ambalo limeanza safari za
moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai kuanzia mwezi Julai 2019 kwa
upande wa India.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.