Mkutano wa
Dharura wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC)
utafanyika tarehe 23 Juni, 2020 kwa njia ya Mtandao (Video Conferencing) katika
Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa
taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali, Wizara
ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Emmanuel Buhohela, mkutano
huo utatanguliwa na kikao cha Kamati ya Kudumu ya Maafisa Waandamizi/ Makatibu
Wakuu chini ya uenyekiti wa Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge, Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kufuatiwa na
Mkutano wa Baraza la Mawaziri.
Mkutano wa
Baraza la Mawaziri utajadili utekelezaji wa maazimio ya Baraza la Mawaziri
dhidi ya mapambano ya ugonjwa wa COVID 19, kupokea taarifa ya Mkutano wa Kamati
ya Wataalamu ya SADC ya kusimamia utekelezaji wa Itifaki ya Afya ya SADC
uliofanyika tarehe 05 Juni 2020 na upendeleo utakaotolewa na India kwa nchi za
SADC zitakaponunua dawa, vifaa kinga na vifaa tiba kwa ajili ya COVID 19.
Mkutano pia
utapitia na kujadili Mwongozo wa Kikanda wa Urazinishaji {harmonization) na uwezeshaji wa
shughuli za usafirishaji ndani ya SADC pamoja na masuala ya uratibu, usimamizi
na uangalizi wa usafirishaji kwa njia ya barabara katika vituo vya kuingilia,
ukaguzi dhidi ya Virusi vya Corona vinavyotambuliwa na SADC na namna ya
kuendeleza shughuli za biashara wakati huu wa janga la CORONA ili kunusuru
uchumi na kupunguza umasikini ndani ya jumuiya.
Mkutano huo utakuwa chini ya Uenyekiti wa Prof. Palamagamba
John Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
utakutanisha Mawaziri wenye dhamana ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa, Fedha na Mipango, Viwanda na Biashara, Uchukuzi, Utalii na Afya
kutoka nchi 16 wanachamawa SADC ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Botswana,
Comoro, DRC, Eswatini, Lesotho, Malawi, Mauritius, Msumbiji, Madagascar,
Namibia, Visiwa vya Shelisheli, Zambia, Zimbabwe na Mwenyekiti Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.