Serikali
imekiagiza Chuo cha Diplomasia kujikita kuongeza tafiti pamoja na machapisho
mbalimbali kwa lengo la kuwawezesha wahitimu wa chuo hicho kutoa mchango wao katika
Taifa hususani wakati huu wa utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.
Maagizo
hayo yametolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (Mb) wakati alipotembelea
chuo hicho na kuongea na wahadhiri, wafanyakazi pamoja na wanafunzi.
Dkt.
Ndumbaro amesema ili chuo cha diplomasia kiendelee kuheshimika zaidi duniani lazima
kihakikishe kuwa kinazalisha tafiti na machapisho ya kutosha.
"Utafiti
na machapisho siyo suala la wahadhiri peke yao…..siyo suala la wanafunzi peke
yao ni suala la wanachuo…… mawazo yenu lazima yafanyiwe utafiti kwa kushirikiana
na wahadiri wenu na ni lazima tuwe na machapisho zaidi," Amesema DKt.
Ndumbaro
Naibu
Waziri ameongeza kuwa moja kati ya changamoto inayoikumba diplomasia hivi sasa ni
mabadiliko ya mifumo mbalimbali duniani ambapo wanadiplomasia wanapaswa kujua
kuwa dunia ipo katika mlengo upi, hivyo vyema mkajikita katika tafiti zenu ili
kuweza kusaidia kufafanua masuala ya kidiplomasia na uhusiano wa kimataifa
yanayotokea duniani.
"Lakini
pia niliagiza muongeze lugha zaidi kwa sababu pia diplomasia pia ni mawasiliano
na unawasiliana na watu wa lugha tofauti tofauti, kwa hiyo tuongeze lugha
mbalimbali ili diplomasia iweze kufanya kazi yake," Amesema DKt. Ndumbaro.
Aida,
Naibu Waziri ameagiza pia chuo hicho kuanzisha semina za kila mwezi ambapo
zitajumuisha Wahadiri na wanafunzi pamoja na mabalozi wastaafu kwa lengo la
kujadili mambo yanayohusu diplomasia na kuwapa uzoefu wa masuala ya
kidiplomasia.
Wanafunzi
kwa upande wao wamepata fursa ya kumuelezea Naibu Waziri changamoto mbalimbali zinazo
wakabili zikiwemo za kupata asilimia ndogo za mkopo wa elimu ya juu, ukosefu wa
mafunzo kwa vitendo, ukosefu wa mabweni pamoja na mazingira ambayo siyo wezeshi
kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
"Mkopo
tunaopewa ni mdogo sana na hautoshi hivyo tunaomba serikali itusaidie kutuongezea
fedha za mkopo ili tuweze kukidhi mahitaji yetu wakati tunapokuwa chuoni,"Amesema
Isack Sadock
Pia,
Dkt. Ndumbaro baada ya kusikiliza changamoto zinazowakabili wanafunzi chuoni hapo,
ameuagiza uongozi wa chuo kuandaa na kuratibu mafunzo kwa vitendo badala ya kufuatiliwa
na wanafunzi, kutoa huduma stahiki kwa wanafunzi wenye ulemavu/maitaji maalumu
ili waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Nae
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera amemhakikishia Naibu
Waziri kuwa chuo kitayafanyia kazi na kuyatekeleza maagizo yote aliyoyatoa.
"Mhe.
Naibu Waziri naomba nikuhakikishie kuwa maagizo yako tumeyapokea……….mimi kwa
kushirikiana na menejimenti, wahadhiri na wafanyakazi tayafanyia kazi kwa
wakati," Amesema Dkt. Ponera
Aidha,
Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro amekagua mradi wa ujenzi wa jengo jipya la chuo cha
Diplomasia.
Katika
hatua nyingine, ametoa msimamo wa Serikali kuhusu changamoto zinazojitokeza
mipakani hasa katika mpaka wa Tanzania na Kenya na kusema kuwa Serikali ipo
kwenye mazungumzo na Kenya ili kuweza kubaini tatizo ni kitu gani.
"Kwa
sasa tupo kwenye majadiliano na wenzetu wa Kenya na kuona tatizo ni kitu gani
je ni corona tu au ni zaidi ya corona? Msimamo wa serikali yetu ni kuwa kila nchi
ipime watu wake…..na tunaamini huo ndiyo msimamo sahihi wa diplomasia ya uchumi,"
Amesema Dkt. Ndumbaro.
Chuo
cha Diplomasia kilianzishwa rasmi tarehe 13 Januari 1978 kwa kusainiwa
Makubaliano yaliyofanywa na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wa wakati huo,
Mhe. Benjamini William Mkapa wa Tanzania na Mhe. Joaquim Chissano wa Msumbiji.
Baadhi ya wanafunzi wakimsikiliza Mhe. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro (hayupo pichani) |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro akiongea na wanafunzi (hawapo pichani) |
Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro akioneshwa mchoro wa jengo jipya la chuo cha Diplomasia na meneja mradi Abdalla Khama |
Meneja mradi wa jengo jipya Abdalla Khama akimuelezea jambo Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro wakati alipotembelea eneo la mradi |
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Diplomasia, Dkt. Jeremia Ponera (aliyesimama) akimkaribisha Naibu Waziri, Dkt. Ndumbaro (aliyekaa wa kwanza kushoto) kwenye kikao cha menejimenti ya chuo |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.