Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuziomba taasisi za fedha za
kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya madola kufikiria kufuta kabisa madeni
yaliyokopeshwa kwa nchi zinazoendelea ili fedha hizo ziweze kutumika kupambana
na athari zilizotokana na Covid 19.
Ombi hilo
limetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi alipokuwa akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe. John Pombe Joseph Magufuli katika mkutano wa Marais, Mawaziri Wakuu pamoja
na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi na Serikali za Jumuiya ya Madola
uliofanyika kwa njia ya mtandao (video conference) leo katika ofisi ndogo za
Wizara jijini Dar es Salaam.
Prof.
Kabudi amesema kuwa Tanzania imesisitiza
tena umuhimu wa mashirika ya fedha ya Kimataifa pamoja na nchi za Jumuiya ya Madola
zilizoikopesha Tanzania mbali na kutoa msamaha wa madeni waweze kufikiria
kufuta kabisa madeni hayo ili kuziwezesha nchi zinazoendelea kuwa na fedha za
kuboresha mifumo ya afya, pamoja na kupambana na athari zilizotokana na janga
la covid 19.
Katika
mkutano huo, Tanzania imesisitiza umuhimu wa kuendeleza ushirikiano kati ya nchi
za Jumuiya ya Madola na nchi zinazoendelea ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na
umoja na mshikamano katika kupambana na janga la Covid
19.
"Mkutano
huu umekuwa ni mkutano muhimu sana katika jumuiya yetu ya madola na
tumesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kushirikiana na kuwa na misaada na mipango
madhubuti ya mashirika ya kimataifa kuzisaidia nchi zinazoendelea katika
jitihada zake za kuboresha na kujenga viwanda vyake hasa vya kutengeneza dawa
na vifaa tiba ili inapotokea majanga kama haya ya covid 19 ziweze kuwa na dawa
na vifaa tiba kwa wananchi wake," Amesema Prof. Kabudi
Ameongeza
kuwa, nchi nyingi mara baada ya janga la covid 19 zilizuia utoaji wa dawa na
vifaa tiba kwenda nje ya nchi kwa sababu dawa hizo walizihitaji kwa ajili ya
matumizi yao wenyewe ndani ya nchi, na ndiyo maana nchi za Jumuiya ya Maendeleo
ya Nchi Kusini mwa Afrika (Sadc) tumeiomba India kwa upendeleo kutupatia dawa
na vifaa tiba vya kukabiliana na janga la Corona.
Aidha, mkutano
umejadili pia umuhimu wa teknolojia katika kupambana na Covid 19 na kuboresha
mifumo ya afya na kwamba wakati umefika sasa teknolojia hiyo mahali popote
ilipo ndani ya Jumiya ya Madola iweze kutolewa kwa nchi zote kwa gharama nafuu ili
kuziwezesha nchi mbalimbali kutumia mifumo mipya ya kiteknolojia katika mifumo
yake ya afya na kuziwezesha pia kupambana na Covid 19.
"Ni
vizuri tuwe na mipango madhubuti na mikakati ya kupambana na aina hii ya
majanga ambayo yanaweza kujitokeza siku za usoni na kufanya hivyo ni kuanza
kujiandaa sasa kwa kuimaraisha huduma za afya katika nchi zetu," Amesema
Prof. Kabudi.
Waziri
Kabudi ameongeza kuwa Tanzania imeanza jitihada hizo kwa kujenga hospitali
nyingi za wilaya, mikoa pamoja na vituo mbalimbali vya afya na zahanati.
Mkutano
umejadili, masuala mbalimbali ikiwemo, covid19, biashara, uchumi, viwanda,
uwekezaji pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.
Mwezi April,
2020 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Joseph Magufuli
aliiomba Benki ya Dunia pamoja na mashirika ya fedha ya kimataifa kuzisamehe
madeni nchi zinazoendelea ili nchi hizo ziweze kutumia fedha hizo katika
mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID 19).
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.