Thursday, July 2, 2020

PROF. KABUDI ATETA NA MJUMBE MAALUM WA MAZIWA MAKUU



TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Prof. Kabudi ateta na Mjumbe Maalum wa Maziwa Makuu

Dodoma, 2 Julai 2020
Tanzania inaamini katika umoja wa jumuiya ya kimataifa kwenye kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili dunia ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa Corona.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb.) alipofanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye eneo la Maziwa Makuu, Balozi Huang Xia.

Viongozi hao walitumia fursa hiyo kubadilishana mawazo katika masuala mbalimbali yanayotokea duniani, ikiwa ni pamoja na mikakati na mbinu bora za kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona na athari zake katika uchumi kwenye eneo la Maziwa Makuu.   

Balozi Huang alielezea hatua mbalimbali anazozichukua zikiwemo kuongea na taasisi za kimataifa za fedha na wadau wengine kwa ajili ya kuzihimiza kutoa misaada kwa nchi za Maziwa Makuu ili ziweze kukabiliana na janga la ugonjwa wa Corona na athari zake za kiuchumi na kijamii. Licha ya kukutana na taasisi hizo, Balozi Huang pia amefanya mashauriano na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Maziwa Makuu kuhusu janga la Corona. Kwenye mashauriano hayo Mawaziri wamesisitiza umuhimu wa kuandaa mkutano wa Mawaziri kwa njia ya mtandao ili kujadili, pamoja na mambo mengine mikakati ya kukabiliana na ugonjwa wa Corona na hali ya usalama katika eneo la Maziwa Makuu.

Kwa upande wake, Prof. Kabudi aliunga mkono wazo la kuwa na mkutano wa Mawaziri wa nchi za Maziwa Makuu na kuelezea matumaini yake kuwa, mkutano huo utatoa mawazo mazuri yatakayosaidia ufumbuzi katika changamoto zinazoikabili dunia ukiwemo ugonjwa wa Corona.

Aidha, Prof. Kabudi alitoa maelezo kuhusu mikakati iliyochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kudhibiti ugonjwa wa Corona. Alisema moja ya mikakati hiyo ni tangazo la maombi ya siku tatu kwa nchi nzima lililotolewa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, maombi ambayo yaliyohusisha imani zote.  Tangazo hilo  lilionekana ni jambo geni kwa watu wengi duniani lakini kwa Tanzania, nchi yenye waislamu na wakristo takribani nusu kwa nusu, lilikuwa ni muhimu na uamuzi huo haukuifanya Tanzania kupuuza maelekezo mengine yanayotolewa na wataalam wa afya.   

Mazungumzo hayo yalihitimishwa kwa Mhe. Waziri kuahidi kuwa, Tanzania itashirikiana kwa karibu na ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika uamuzi wake wa kuandaa mkakati maalum wa kuzuia migogoro na kuimarisha amani na utulivu kwenye eneo la nchi za maziwa makuu.


Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi akizungumza kwa njia ya mtandao na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwenye Ukanda wa Maziwa Makuu, Mhe. Balozi Huang Xia kuhusu ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona na masuala ya amani na usalama katika ukanda huo. Mazungumzo hayo yalifanyika Prof. Kabudi akiwa jijini Dodoma huku Balozi Huang Xia akiwa jijini Nairobi, Kenya.
Sehemu ya ujumbe ulioambatana na Mhe. Prof. Kabudi ukifuatilia mazungumzo kati ya Prof. Kabudi na Balozi Huang Xia (hawapo pichani). Kulia ni Bw. Magabilo Murobi, Katibu wa Waziri na Bw. Ali Ubwa, Afisa Mambo ya Nje.




No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.