TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
TANZANIA YACHAGULIWA KUWA RAIS WA BARAZA LA MAWAZIRI WA JUMUIYA YA NCHI ZA AFRIKA, CARRIBEAN NA PACIFIC
Dodoma, 6 Agosti 2020
Serikali ya Tanzania imechaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Mawaziri wa
Jumuiya ya Nchi za Afrika, Carribean na Pacific (Organisation of African,
Carribean and Pacific States-OACPS) kwa
kipindi cha miezi sita kuanzia tarehe 1 Agosti 2020 hadi tarehe 31 Januari
2021.
Mhe. Prof. Palamagamba John Kabudi, Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki alikabidhiwa rasmi nafasi hiyo
iliyopokelewa kwa niaba yake na Mhe. Dkt. Damas Daniel Ndumbaro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki wakati wa Mkutano wa Dharura wa Baraza la Mawaziri wa
Jumuiya hiyo uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 28 Julai 2020.
Tanzania inakuwa Rais wa Baraza hilo kutokana na Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Mhe. Jestas
Abuok Nyamanga kuchaguliwa kwa kauli moja kuwa Mwenyekiti wa Mabalozi wa Nchi
za OACPS waliopo Brussels. Kwa mujibu wa Jumuiya ya OACPS, nchi inayotoa Mwenyekiti wa Mabalozi wa
Jumuiya hiyo, Waziri wake anayesimamia masuala ya OACPS ambaye ni Waziri wa
Mambo ya Nje moja kwa moja anakuwa Rais wa Baraza la Mawaziri. Uamuzi wa
kuichagua Tanzania ulifanywa na Mabalozi kutoka nchi 15 za Ukanda wa Mashariki
mwa Afrika kwenye kikao kilichofanyika tarehe 2 Julai 2020 na kuthibitishwa kwa
kauli moja na mabalozi wote wa nchi 79 wa OACPS kupitia kikao chao kilichofanyika
Brussels tarehe 14 Julai 2020.
Tanzania ambayo inachukua nafasi hiyo kutoka kwa Gambia, imejipanga
kutekeleza masuala mbalimbali yenye maslahi kwa Nchi za OACPS ikiwa ni pamoja
na kusimamia ukamilishwaji wa majadiliano kuhusu Mkataba mpya wa ushirikiano wa
Nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya (EU) unaotarajiwa kuanza kutumika mwezi Januari
2021 baada ya mkataba wa sasa wa Cotonou (Cotonou Partnership Agreement)
kufikia ukomo mwezi Desemba 2020, pamoja na kuhakikisha maslahi ya nchi za OACPS yanaingizwa kwenye
mkataba huo mpya. Aidha, Tanzania imejipanga kusimamia utekelezaji wa mikakati
mbalimbali ya Jumuiya ya OACPS katika kukabiliana na janga la ugonjwa wa COVID-19
na madhara yake kiuchumi kwa nchi wanachama.
Kadhalika, maeneo mengine ya kipaumbele yatakayosimamiwa na Tanzania
katika kipindi cha Urais wa Baraza hilo ni kusimamia mikakati ya kuongeza mtangamano na ushirikiano
miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya; kusimamia mabadiliko ya kiutendaji na
mifumo ili kuendana na wakati pamoja na kudumisha mshikamano na umoja miongoni
mwa nchi wanachama wa Jumuiya.
Vilevile miongoni mwa manufaa ya Tanzania kuwa Rais wa Baraza hilo ni pamoja na kuongeza ushawishi wa nchi yetu
katika kupanga na kutekeleza mikakati, miradi na programu mbalimbali za Jumuiya
ya OACPS ambazo ni pamoja na zile zinazotekelezwa kwa kushirikiana na Umoja wa
Ulaya na wabia wengine wa maendeleo kama vile kilimo, uwekezaji, biashara na
ujasiriamali, mazingira, miundombinu, vijana na utamaduni.
Hii ni mara ya tatu kwa Tanzania kuwa Rais wa
Baraza la Mawaziri na Mwenyekiti wa Mabalozi wa nchi za OACPS tangu ilipojiunga mwaka 1975. Miongoni mwa sababu zilizopelekea Tanzania kuchaguliwa
kwenye nafasi hiyo ni kutokana na kuongozeka kwa ushawishi wake kwenye Jumuiya
ya OACPS, Sera na hatua thabiti zinazochukuliwa na Mhe. Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kusimamia masuala
mbalimbali ya kitaifa na kimataifa pamoja na utendaji madhubuti wa Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kusimamia Sera ya Mambo
ya Nje ikiwemo ushiriki mahiri wa
Tanzania katika masuala yanayogusa maslahi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya
OACPS.
Imetolewa
na;
Kitengo
cha Mawasiliano ya Serikali.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.