Thursday, October 8, 2020

Matukio katika Ubalozi wa Tanzania, Abu Dhabi

KUTAFUTA SOLO LA KOROSHO

Mhe. Balozi Mohamed Mtonga alifanya mazungumzo na wafanyabiashara, Bw. Abdo Shamakh Al-Shibani wa kampuni ya SHAFA iliyopo Dubai na Bw. Dzhuraev Khairullo ambaye ni Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya FoodArt LLC yenye Makao Makuu yake mjini Moscow nchini Urusi. Kampuni ya FoodArt LLC imekuwa ikinunua korosho sehemu mbalimbali duniani na kuziuza katika nchi mbalimbali za Ulaya ikiwamo Urusi.

Mhe. Balozi Mtonga aliwaonesha fursa ya kuweza kununua zao la korosho kutoka Tanzania na kuwapa mwongozo wa ununuzi kama ulivyotolewa na Wizara ya Kilimo na Ushirika na Bodi ya Korosho Tanzania.

Kwa ujumla wafanyabiashara hao walionesha dhamira ya kununua zao la korosho kutoka Tanzania katika msimu huu wa mwaka 2020/2021.

KUKABIDHI UENYEKITI WA SADC

Mhe. Balozi Mohamed Mtonga alikabidhi Uwenyekiti wa SADC Group of Ambassadors hapa Abu Dhabi kwa Balozi wa Nchi ya Msumbiji. Mhe. Balozi Tiago Recibo Castigo. Balozi Tiago, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alikuwa Mwenyekiti wa SADC aliyemaliza muda wake kwa mafanikio makubwa katika kipindi chake cha uenyekiti licha ya changamoto ya ugonjwa wa COVID-19.


KUTANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI

Mhe. Mohamed Abdallah Mtonga, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu alifanya mazungumzo na Wakurugenzi wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi (ADNOC), Bw. Khaled Salmeen, Bw. Iman Al Hosani, Bw. Mohamed Al Suwaidi na Bw. Abdulla Al Qubaisi kwa njia ya mtandao (Virtual Meeting).

Balozi alitumia fursa hiyo kuwajulisha fursa kadhaa zilizopo katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzaia katika eneo hili la Mafuta na Gesi. Maeneo aliyowajulisha kwa uwekezaji ni yale yaliyohusu uwekaji wa miundombinu katika biashara ya Gesi na Mafuta. Aidha, Balozi aliwajulisha fursa za kibiashara katika biashara ya mbolea aina ya Urea kwa utaratibu wa Bulk Procurement System unaoratibiwa na Tanzania Fertilizers Regulatory Authority na uletaji wa Mafuta kwa pamoja unaoratibiwa na Bulk Procurement System for Petroleum Products. Bidhaa zote hizi huzalishwa na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Abu Dhabi (Abu Dhabi National Oil Company (ADNOC).

Vilevile, Balozi aliwasilisha kwa ADNOC miradi ambayo ipo tayari kwa uwekezaji iliyopo katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (Tanzania Investment Centre) ambayo inatafuta wawekezaji au wabia.

Miradi hiyo ni kama ifuatavyo:

·       Establishment of Strategic Petroleum Reserve Infrastructures (Farm Tanks).

Kwa mujibu wa andiko Mradi utajikita katika ujenzi wa Matanki ya kuhifadhia mafuta katika miji ya Dar Es Salaam, Morogoro, Isaka(Kahama),Makambako, Mbeya, Songwe na Tanga. Watekelezaji wa Mradi huu ni Mwekezaji Mshirika (Strategic Partner) na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development Corporation). 

·       LPG Bulk Distribution Project

Kwa mujibu wa andiko Mradi huu ni kuweka miundombinu ya Kupokea,kuhifadhi na kuweka miundombinu ya kujaza Gesi aina ya LPG. Mradi huu utatekelezwa kwa awamu katika miji ya Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Watekelezaji wa Mradi huu ni Mwekezaji Mshirika (Strategic Partner) na Shirika la Maendeleo la Petroli Tanzania (Tanzania Petroleum Development Corporation).

Kwa upande wao, Wakurugenzi wa ADNOC wamehitaji taarifa mbalimbali ambazo Mhe. Balozi Mohamed Mtonga ameziwasilisha katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwa kufanyiwa kazi.







 

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.