Friday, October 23, 2020

NCHI ZA AFRIKA ZAHIMIZWA KUSHIKAMANA ILI KUONDOKANA NA UTEGEMEZI

Nchi za Afrika zimehimizwa kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi jambo litakaloliwezesha Bara hilo kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje kwa kisingizio cha demokrasia na haki za binadamu.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar es Salaam na Kiongozi wa Mabalozi wa nchi za Afrika hapa Tanzania Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed wakati Mabalozi hao walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ikiwa ni utaratibu wa kukutana na Mabalozi mbalimbali wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kwa lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo na Tanzania.

Kiongozi huyo wa Mabalozi hapa nchini ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro amesema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara hilo linaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara hilo kujitegemea.

"Njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa sisi kama waafrika tunaweka mikakati madhubuti itakayowezesha bara letu kujitegemea kwa umoja, mshikamano wetu wenyewe," Amesema Dkt. Mohamed

Nae Balozi wa Kenya hapa Nchini Mhe. Dan Kazungu amesema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.

"MKutano wa leo umetuwezesha sisi mabalozi wa Afrika tunaowakilisha nchi zetu hapa Tanzania kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo," Amesema Balozi Kazungu.   

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi ameitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika,kulinda demokrasia na haki za binadamu lakini pia kutumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.  

"Waheshimiwa Mabaalozi napenda kuwahakikishia kuwa Tanzania inaheshimu na imedhamiria kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za binadamu pamoja na kuhakikisha kuwa inatumia fedha zake za ndani katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa," Amesema Prof. Kabudi.  

Mkutano huo uliohudhuriwa Mabalozi 15 na wawakilishi wa Balozi 8 walitumia fursa hiyo kumuombea Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere kama Baba wa demokrasia Barani Afrika pamoja na kuuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Mabalozi waliohudhuria katika mkutano huo ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Ahamada El Badaoui Mohamed, Balozi wa Msumbiji, Mhe. Patricio Clemente, Balozi wa Namibia, Mhe. Theresia Samaria, Balozi wa Somalia, Mhe. Mohammed Abdi, Balozi wa Morocco, Mhe. Abdelilah Benryane, Balozi wa Zambia, Mhe. Benson Chali.

Wengine ni Balozi wa Burundi, Mhe. Gervais Abayeho, Balozi wa Kenya, Mhe. Dan Kazungu, Balozi wa Ethiopia, Mhe. Yonas Yosef Sanbe, Balozi wa Misri, Mhe. Mohamed Gaber Mohamed Abdulwafa, Balozi wa Angola, Mhe. Sandro De Oliveira, Balozi wa Malawi, Mhe. Chembe Mnthali, Balozi wa Saharawi, Mhe. Mahayub Buyema, Balozi wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali, Charles Karamba pamoja na Balozi wa Algeria, Mhe. Ahmed Djelal.

Wawakilishi waliowakilisha Balozi nane ni Bw. Jaafar Nasir Abdalla kutoka Ubalozi wa Sudan, Mr. Sizwe Ernest Mayoli kutoka Ubalozi wa Afrika Kusini, Balozi William Wani Ruben kutoka Ubalozi wa Sudani Kusini, Bibi. Bintu Bwala Ekikor kutoka Ubalozi wa Nigeria, Bw. Kamal Krista kutoka ubalozi wa Libya, Bw. Adjanga Bissa Benjamin kutoka ubalozi wa DRC, Bibi. Musekura Esezakutoka ubalozi wa Uganda pamoja na Bw. Chrispen Chibuwe kutoka Ubalozi wa Zimbabwe.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi akiongea na Mabalozi mbalimbali wa nchi za Afrika hapa nchini Tanzania leo jijini Dar es Salaam

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwaonesha Mabalozi (hawapo pichani)  ilani ya Chama Cha Mapinduzi wakati mkutano ukiendelea



Mkutano baina ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na Mabalozi ukiendelea  


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi mara baada ya kumaliza mkutano



No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.