Thursday, November 26, 2020

MAWAZIRI SADC - TROIKA WAKUTANA KWA DHARURA BOTSWANA

 Baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama wakutana katika mkutano wa dharura na kujadili masuala ya siasa, ulinzi na usalama.

Mkutano huo umefanyika leo mjini Gaborone, Botswana ambapo ulitanguliwa na mkutano wa Makatibu Wakuu wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama ulioanza asubuhi na kumalizika mchana.

Kupitia mkutano huo, mawaziri wameweza kujadili masuala ya hali ya siasa, ulinzi na usalama katika kanda ya SADC na kupendekeza njia mbalimbali za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza kwenye siasa, ulinzi na usalama ndani ya ukanda wa SADC.

Pamoja na mambo mengine, Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama  inawajibika kukuza amani na usalama katika eneo la SADC na pia ina wajibu wa kuongoza na kuzipatia nchi Wanachama mwongozo kuhusu mambo ambayo yanatishia amani, ulinzi na usalama.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) (mwenye tai nyekundu) akifuatilia mkutano wa dharura wa baraza la Mawaziri wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama uliofanyika Mjini Gaborone. Kulia mwa Waziri ni Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe akifuatiwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge

Ujumbe wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) ukiwa ukiimba wimbo wa SADC kabla ya kuanza kwa mkutano wa dharura wa baraza la Mawaziri


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Botswana Dkt. Lemogang Kwape akifungua mkutano wa Dharura wa baraza la mawaziri, kushoto kwake ni Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Taxi

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Asasi ya SADC ya Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Mtendaji wa SADC, Dkt. Stegomena Taxi mara baada ya kumaliza mkutano wao     


No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.