Katibu Mkuu
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge
amekutana na Wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na kuwahimiza
kutanguliza maslahi ya Tanzania katika
kutekeleza majukumu yao.
Mhe. Ibuge
amesema hayo jijini Dodoma alipokutana na Wabunge hao na kusisitiza kuwa maslahi ya Tanzania ni lazima yawe kipaumbele chao katika kutekeleza majukumu yao ili
kufanikisha ushiriki wa Tanzania kikamilifu katika mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Endeleeni kushikilia msimamo wa kutanguliza maslahi ya Tanzania siku zote, muendelee kufanya kazi hiyo nzuri kwenye masuala mengine yote yanayogusa maslahi ya nchi yetu,” amesema Balozi Ibuge na kuongeza kuwa nafasi yao kama wabunge wa Afrika Mashariki inatokana na uwepo wa jimbo lao ambalo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mtangamano huo.
Balozi Ibuge
pia amewataka Wabunge hao kuwasiliana mara kwa mara na Serikali ili kupata maoni,
ushauri na msimamo wa Serikali katika kujadili na kupitisha masuala mbalimbali
ndani ya bunge hilo.
Balozi Ibuge
amewataka wabunge hao kujiepusha na migogoro ndani ya Bunge na Jumuiya kwani
kufanya hivyo kutaiwezesha Tanzania kujiweka sawa katika nyanja za siasa na
diplomasia na kuwapongeza kwa utendaji kazi wao na hasa jinsi
walivyoshughulikia suala la Muswada binafsi wa Marekebisho ya Sheria ya Usimamizi
wa Forodha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Akizungumza
katika kikao hicho Mwenyekiti wa Wabunge hao Mhe. Adam Kimbisa aliishukuru Wizara
kwa kukutana nao kuwapa muongozo wa namna ya kushughulikia mambo mbalimbali
yanayoendelea ndani ya Bunge na Jumuiya kwa ujumla.
Mhe. Kimbisa
alimuahakikishia Katibu Mkuu kuwa Wabunge hao
wataendelea kuhakikisha maslahi ya Tanzania yanazingatiwa katika hatua
zote za mtangamano kupitia ushiriki wao katika Bunge la Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.