Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki umepangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021 kwa njia ya mtandao (video conference).
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amewaeleza waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam kuwa mkutano huo ni muhimu kwa sababu ya maamuzi ya msingi
ya kuiwezesha jumuiya hiyo iweze kuendelea kufanya kazi zake.
“………Jambo la kwanza ni uteuzi wa Katibu Mkuu mpya wa
Jumuiya ya Afrika mashariki, kwa hiyo Wakuu wa nchi watamchagua Katibu Mkuu
mpya siku hiyo,” Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mkutano huo pia utafanya
uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (The East African
Court of Justice) kutokana na baadhi ya majaji kufikia umri wa kustaafu wa
miaka 70, ambapo Tanzania imempendekeza jaji Yohane Masara kuwa jaji wa jopo la
kwanza la mahakama ya Afrika Mashariki.
“Pamoja na kuteuliwa kwa majaji hao, pia Wakuu wa nchi
watamteua Rais wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki (Judge President) pamoja
na kumchagua Makamu wa Rais (Vice President) kwa ngazi ya Rufaa ya Mahakama
hiyo, lakini katika ngazi ya awali Mkutano huo utamchagua Principla Judge wa
Mahakama hiyo, kwa hiyo mtaona hizo ni baadhi ya shughuli zilizopelekea Wakuu wa
nchi wakutane ili kuweza kufanya teuzi hizo muhimu ili shughuli za Jumuiya ya
Afrika Mashariki ziweze kuendelea” Ameongeza Prof. Kabudi
Prof. Kabudi ameongeza kuwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki pia utajadili Muswaada ulipitishwa na Bunge la
Afrika Mashariki kwa ajili ya kupata bajeti.
Mkutano huo utatanguliwa na mkutano wa 40 wa Kawaida
wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki utakaofanyika Alhamisi tarehe 25
Februari 2021 kwa ajili ya kuandaa mkutano wa wakuu wa nchi. Aidha, mkutano wa
Baraza la Mawaziri umetanguliwa na mkutano Wataalam ulifanyika tarehe 22-23
Februari na mkutano wa Makatibu Wakuu ulifanyika tarehe 24 Februari.
Tarehe 1 Januari 2019, Rais wa Rwanda Mhe. Paul
Kagame alikabidhiwa Uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki katika Mkutano wa
wakuu wa jumuiya hiyo jijini Arusha Tanzania.
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi ameelezea kuhusu
ziara ya kikazi aliyoifanya nchini Ufaransa kuanzia tarehe 16 mpaka 21 Februari
2021, kufuatia mwaliko wa Mhe. Jean-Yves Le Drian, Waziri anayeshughulikia
Masuala ya Ulaya na Mambo ya Nje wa Ufaransa na kuelezea mafanikio makubwa ya
ziara hiyo.
“Pamoja na mambo mengine niliweza kukutana na
kufanya mazungumzo na viongozi wa Serikali ya Ufaransa, Umoja wa
Wafanyabiashara wa Ufaransa (MEDEF), Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa
Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Uongozi wa
Kampuni ya Total, Kundi la Maseneta wa Bunge la Ufaransa ambao ni Marafiki wa
Tanzania, Uongozi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Wadau wa Utalii
pamoja na kuzungumza na Watanzania wanaoishi nchini Ufaransa,” Amesema Prof.
Kabudi.
Aidha, kupitia ziara hiyo, Ufaransa imeeleza kuwa itaendelea kuhamasisha Makampuni yake kuja kuwekeza Tanzania pamoja na kuhamasisha watalii kuja kuwekeza Tanzania, kuiunga mkono Tanzania katika masuala mbalimbali kwenye ngazi ya Umoja wa Mataifa.
Mengine
ni kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itaendelea kufadhili
miradi mbalimbali ya maendeleao hapa nchini hususan kwenye sekta ya maji,
elimu, nishati, miundombinu, utalii, ulinzi na usalama;na Ufaransa kuwa tayari
kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali yanayohusu ulinzi na
Usalama.
Mafanikio
mengine ni pamoja na kukubaliana kuanza mara moja mchakato wa kuifanya lugha ya
Kiswahili kuwa miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika kwenye Umoja wa Mataifa.
Nilimweleza mafanikio yaliyopatikana kwenye lugha ya Kiswahili ikiwa ni pamoja
na kuwa miongoni mwa lugha 10 zinazozungumzwa zaidi barani Afrika pamoja na
kutumika kama lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika (AU) na SADC;
“Tulikubaliana
kuanza mchakato ili kuwa na siku rasmi ya kuadhimisha lugha ya Kiswahili
duniani kila mwaka. Nilipendekeza tarehe 7 Julai kila mwaka kwa kuzingatia kuwa
tarehe hiyo ndio kilizaliwa Chama cha TANU. TANU ilikifanya Kiswahili kuwa
lugha rasmi ya kupigania uhuru wa Tanganyika wakati huo. Tumeona ni jambo jema
kuienzi tarehe hiyo muhimu kwenye historia ya nchi yetu,” Amesema Prof. Kabudi
Kupitia ziara hiyo, Prof. Kabudi aliweza kuyakaribisha
Makampuni ya Ufaransa kuja kuwekeza nchini hususan kwenye sekta ya viwanda,
kilimo, nishati, maji, elimu, miundombinu, uvuvi na utalii. Makampuni hayo
yalionesha kuridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika
kuboresha mazingira ya uwekezaji na ushiriki wa sekta binafsi katika uchumi wa
Tanzania.
“Baadhi ya Makampuni makubwa yaliyoshiriki
majadiliano hayo ni pamoja na Bureau Veritas; Mitsubishi II; Biolore Transport
and Logistics; Eutelsat Company; Artelia Company; Catering International
Services-CIS; Systra Company; Transder
Group; Credit Agricole Corporate and Investment Bank; Air Bus; na Bouyegues
Construction. Mengi ya makampuni haya tayari yamefanya uwekezaji mkubwa nchini
katika maeneo mbalimbali,” Amesema Prof. Kabudi.
Aidha, makampuni hayo yameonesha utayari wa
kutekeleza miradi hapa nchini kwa kutumia fedha kutoka Serikali ya Ufaransa
zitakazotolewa kama mkopo wenye masharti nafuu. Tumeyakaribisha Makampuni hayo
kuja nchini ili kukutana na wataalam wetu kwa ajili ya majadiliano.
Prof. Kabudi ameelea kuwa Shirika la Maendeleo la
Ufaransa (AFD) kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania ipo katika hatua za
mwisho za kukamilisha majadiliano ya miradi ya kimkakati kwa Tanzania katika
sekta ya maji safi na usafi wa mazingira, nishati na miundombinu ambapo tayari
jumla ya fedha Euro milioni 791.70 tayari zimeshatengwa kwa ajili ya miradi
hiyo. Fedha hizo zitaelekezwa katika baadhi ya miradi ambayo ni mradi wa ujenzi
wa awamu ya tano ya mwendokasi BRT Phase 5 (Euro milioni 150), mradi wa Maji
safi na Usafi wa Mazingira mkoani Shinyanga (Euro milioni 70), ujenzi wa bwawa
la kuzalisha umeme la Kakono (Euro milioni 100), mradi wa kuzalisha umeme kwa
kutumia jua chini ya TANESCO (Euro milioni 130) na mradi wa kuunganisha umeme
Tanzania na Uganda (Euro milioni 100).
Katika hatua nyingine, Prof. Kabudi amewasihi
watanzania kuheshimu katiba na kuacha mara moja tabia ya kusambaza taarifa za
uongo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwasomea waandishi wa habari (hawapo
pichani) moja ya kifungu cha katiba kuhusu mipaka ya haki na Uhuru na hifadhi
kwa haki na wajibu jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika
Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akiwaonesha waandishi wa habari (hawapo
pichani) aina za cocoa zinazozalishwa Tanzania na kuuzwa nchini Ufaransa jijini
Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.