Na Mwandishi wetu, Dar es
Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana
na kupokea nakala za hati za utambulisho za mabalozi wateule hapa nchini pamoja
na hati ya utambulisho ya Konseli Mkuu wa China Zanzibar.
Mabalozi
waliowasilisha nakala za hati za utambulisho kwa Prof. Kaabudi katika Ofisi
Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius
Tangeni Tobias na Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil, pamoja na Konseli
Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.
Awali akiongea mara
baada ya kupokea nakala ya hati ya utambulisho wa Balozi mteule wa Namibia, Prof.
Kabudi amesema kuwa Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza kuimarisha
sekta ya biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi katika bahari kuu pamoja madini
kwa maslahi ya mataifa yote mawili.
“Tanzania na Namibia
tuna historia inayofanana iliyoanza tangu vita vya ukombozi wa uhuru wa
Namibia….wote tulikuwa makoloni ya Wajerumani, hivyo tumekubaliana kuimarisha
sekta za biashara na uwekezaji, na katika maeneo ya mazao ya mifugo, uvuvi,
kilimo, na madini, ambapo katika maeneo hayo Tanzania tunayo mengi ya kujifunza
kutoka Namibia hasa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika bahari kuu,hivyo
tukiimarisha maeneo hayo uchumi wan chi zetu mbili utazidi kukua na kuimarika”
Amesema Prof. Kabudi
Kwa upande wake Balozi
Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias ameahidi kuendeleza
ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Namibia.
“Mimi kama mwakilishi
wa Serikali ya Namibia nitajitahidi wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania kuhakikisha
kuwa uhusiano wetu sisi Namibia na Tanzania unazidi kuimarika kwa maslahi
mapana ya wananchi wetu wote,” Amesema Mhe. Tobias
Kadhalika, Prof.
Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho wa Balozi mteule wa Ireland hapa
nchini, Mhe. Mary O’Neil ambapo mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho
Balozi Mteule ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na
Ireland.
“Ni furaha kwangu
kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini
Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa
uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa
yetu,” Amesema Balozi O’Neil
Kwa upande wake Prof.
Kabudi amesema kuwa mahusiano ya kibalozi kati ya Tanzania na Ireland yalianza
tangu mwaka 1979 ambapo Ireland ilianzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa
masomo katika vyuo vikuu vya Ireland kwa watanzania katika taaluma mbalimbali.
“Mbali na kutoe
ufadhili wa elimu kwa Watanzania, tumeongelea masuala ya kuimarisha ufadhili wa
masomo, biashara na uwekezaji hasa kwa kutumia teknolojia ya habari pamoja na
kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na katika kipindi chake cha uwakilishi hapa
nchini tutaangalia maeneo mapya ya ushirikiano ili tuweze kuendele kuimarisha
ushirikiano baina yetu na Ireland,” Amesema Prof. Kabudi.
Katika tukio jingine,
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba
John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea hati ya utambulisho wa Konseli Mkuu wa
China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.
Prof. Kabudi amesema
kuwa China imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar tangu mapinduzi ya mwaka 1964,
katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ukarabati
wa uwanja wa ndege, hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na Abdallah Mzee………na “tumekubaliana
kuwa tutaendelea kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania – Zanzibar
ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Amesema Prof. Kabudi
Nae Konseli Mkuu wa
China Zanzibar amesema kuwa China kama taifa lililoendelea wataendelea
kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha
mahusiano ya China na Tanzania yanaimarika kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“China inaunga mkono
umoja, amani na mshikamano wa Tanzania, sisi tumekuwa marafiki wa muda mrefu na
tutaendelea kusaidiana ili kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya China na Tanzania
yanazidi kuimarika hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli na
Rais Mwinyi,” Amesema Mhe. Zhisheng
Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea
nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias leo katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati za utambulisho kutoka Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.