Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokelewa na Waziri wa
Mambo ya Nje wa Kenya Mhe. Raychelle Omamo alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo
Kenyatta jijini Nairobi kuanza ziara rasmi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa
mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akitia
saini kitabu maalum mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa
wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini Kenya. |
Baadhi ya Watanzania wakisubiri kumkaribisha Rais wa Jamhuri ya Muungano
Mhe. Rais Samia Suluhu Hasssan alipowasili jijini Nairobi kwa ziara rasmi ya
siku mbili nchini Kenya. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan akiwasalimia
baadhi ya Wafanyabiashara wa Tanzania waliopo Kenya alipowasili jijini
Nairobi kwa ziara rasmi ya siku mbili nchini Kenya. |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewasili
katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi nchini
Kenya kuanza ziara rasmi ya siku mbili kufuatia mwaliko wa mwenyeji wake Rais
wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Kenyatta.
Alipowasili jijini Nairobi Mhe. Rais Samia alilakiwa na Waziri wa Mambo
ya Nje wa Kenya Mhe. Raychelle Omamo na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi Mhe. Amina
Mohammed.
Baada ya kuwasili Mhe. Rais Samia aliekea hotelini kwa ajili ya mapumziko
kidogo na baadaye alielekea Ikulu ya Nairobi kwa ajili ya kupokelewa rasmi na
Mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta ambapo alikagua gwaride na kupigiwa mizinga
21 kwa heshima yake.
Akiwa Ikulu jijini Nairobi Mhe. Rais alifanya mazungumzo ya faragha na
mwenyeji wake Mhe. Rais Kenyatta na baadaye walifanya mazungumzo rasmi ambayo
yalihudhuriwa na wajumbe wa pande zote mbili.
Baada ya kumaliza mazungumzo yao viongoazi hao walizungumza na waandishi
wa habari na baadaye Mhe. Rais Samia alikwenda kuweka shada la maua katika
Kaburi la Baba wa Taifa la Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta.
Jioni Mhe. Rais atahudhuria dhifa ya Kitaifa ambayo imeandaliwa kwa
heshima yake na mwenyeji wake Rais Uhuru Kenyatta.
Kesho tarehe 05/05/2021 Mhe. Rais akiwa na mwenyeji wake Rais Uhuru
Kenyatta atahutubia Mabunge ya Kenya na baadaye atafungua Kongamano la wafanyabiashara
wa Kenya na Tanzania linalofanyika jijini Nairobi.
Mhe. Rais anatarajiwa kurejea nyumbani siku hiyohiyo ya tarehe
05/-05/2021
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.