Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) amekutana na kuzungumza na mabalozi wanne wanaowakilisha nchi zao hapa
nchini na kupokea nakala ya hati ya utambulisho ya balozi mteule wa Msumbiji hapa
nchini.
Mabalozi
waliokutana na Waziri katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi
wa Rwanda, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba, Balozi wa Indonesia Mhe. Ratlan
Pardede, Balozi wa Sweden Mhe. Anders Sjöberg na Balozi wa Norway Mhe. Elisabeth
Jacobsen.
Pamoja
na mambo mengine, Mhe. Waziri Mulamula na mabalozi hao wamejadili juu ya kuimarisha
na kuongeza ushirikiano baina ya mataifa wanayoyawakilisha hapa nchini na
Tanzania.
“Leo nimekutana na mabalozi kadhaa
wanaowakilisha nchi zao hapa nchini, akiwemo Balozi wa Rwanda, Sweden, Norway
na pia nimepokea nakala ya hati ya utambulisho ya balozi mteule wa Msumbiji na
kuwahakikishia ushirikiano wetu kama wizara, kama nchi katika kuboresha na kukuza
mahusiano yetu,” amesema Balozi Mulamula
Nae
Balozi wa Rwanda hapa nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles Karamba amesema kuwa
ushirikiano baina ya Tanzania na Rwanda ni mzuri hivyo wataendelea kuudumisha uhusiano
huo kwa maslahi ya pande zote mbili.
“Nchi
zetu mbili zimekuwa zikishirikiana vizuri hivyo tumekubaliana kuendelea
kudumisha ushirikiano huu kwani Watanzania na Wanyarwanda ndugu na marafiki,” amesema
Balozi Karamba
Kwa
upande wake Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Ratlan Pardede amesema
Indonesia na Tanzania zitaendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali ikiwemo
uchumi, utalii na kijamii na kuhakikisha kuwa ushirikiano huo unazidi
kuimarika.
“Tumejaribu
kuwahamasisha wawekezaji kutoka Indonesia kuja kuwekeza hapa Tanzania na hadi
sasa kampuni kumi (10) zimewekeza katika sekta za biashara na uwekezaji, madini,
uvuvi, ujenzi na viwanda,” amesema Balozi Pardede
Nae
Balozi wa Sweden Mhe. Anders Sjöberg amesema kuwa Sweden itaendelea kuimarisha
mahusiano na ushirikiano katika sekta za biashara na uwekezaji, utunzaji wa mazingira
na masuala ya kijamii kama vile usawa wa kijinsia, uhuru wa vyombo vya habari
pamoja na haki za binadamu.
“Tumejadiliana
kuhusu kuimarisha mahusiano, biashara na uwekezaji, utunzaji wa mazingira
pamoja na masuala ya kijamii kama vile usawa wa kijinsia, uhuru wa vyombo vya
habari na haki za binadamu,” amesema Balozi Sjöberg.
Kwa
upande wake Balozi wa Norway hapa nchini, Mhe. Elisabeth Jacobsen amesema
Norway na Tanzania zimekuwa na uhusiano mzuri ambapo kwa sasa Norway inaangalia
fursa za uwekezaji na biashara hapa nchini ili kuimarisha mahusiano na kukuza
uchumi.
“Norway
itaendelea kutumia fursa za uwekezaji na biashara zilizopo Tanzania ili
kuimarisha mahusiano yetu na kukuza uchumi wa pande zote mbili,” amesema Balozi
Jacobsen
Katika
tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe.
Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea nakala ya hati ya utambulisho kutoka kwa
Balozi Mteule wa Msumbiji hapa nchini Mhe. Ricardo Ambrosio Sampaio Mtumbuida.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akizungumza na Balozi wa Rwanda hapa nchini, Mhe. Meja Jenerali Charles
Karamba katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam. Kulia ni baadhi ya
Wakurugenzi na Afisa kutoka Wizarani
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akiteta jambo na Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Ratlan Pardede katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mazungumzo
kati ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi
Liberata Mulamula (Mb) na Balozi wa Indonesia hapa nchini Mhe. Ratlan Pardede yakiendelea
Balozi
wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg akimsikiliza Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati balozi huyo
alipomtembelea Mhe. Waziri ofisini kwake Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.