Thursday, June 3, 2021

BALOZI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA CHINA NCHINI NA NAIBU KATIBU MKUU WA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb) Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki leo tarehe 3 Juni 2021 kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. WANG Ke Balozi wa China nchini Tanzania na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. 

Balozi WANG amemtembelea Balozi Mulamula kwa lengo la kumuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi hapa nchini. Balozi WANG ameeleza furaha na kuridhishwa kwake na namna Wizara na Serikali kwa ujumla ilivyompa ushirikiano kwa kipindi chote alichokuwa nchini akitekeleza majukumu yake. Aidha, ameonyesha furaha yake juu ya namna mahusiano kati ya Tanzania na China yanavyoendelea kushamiri na hivyo kuchagiza maendeleo kwa Nchi zote mbili. 

Balozi Mulamula kwa upande wake amempongeza na kumshukuru Balozi WANG kwa utumishi na mchango wake alioutoa katika kudumisha na kukuza mahusiano kati ya Tanzania na China. Sambamba na pongezi hizo Balozi Mulamula amemtakia kheri Balozi WANG katika maisha yake na utumishi. Vilevile Balozi Mulamula amemwakikishia Balozi WANG kuwa Tanzania itaendelea kudumisha na kukuza mahusiano mazuri yaliyopo kati ya Tanzania na China yaliyodumu kwa nyakati zote. 

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Balozi Mulamula na Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa pamoja wamekutana na kufanya mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala. Mhandisi Mlote amefika Wizarani kwa lengo la kujitambulisha kwa Waziri Mulamula na Naibu Waziri Mbarouk na kuwapongeza kwa kuteuliwa kushika nyadhifa hizo. 

Balozi Mulamula na Balozi Mbarouk wamemweleza Mhandisi Mlote kuwa Wizara na Serikali kwa ujumla itaendelea kutoa ushirikiano kwa Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika shughuli zao za kuiletea maendeleo Jumuiya. Aidha, wameipongeza Sekretariet kwa kazi nzuri ya kutekeleza miradi ya kimkakati kama vile ujenzi barabara, miradi ya umeme na maji ambayo inaleta mchango mkubwa katika kukuza uchumi kwa Nchi wanachama. 
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo na Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma
Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akimsikiliza Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

Mazungumzo yakiendelea


Mheshimiwa Balazo Liberata Rutageruka Mulamula (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb), Naibu Waziri (kulia) na Mhandisi Steven Mlote,Naibu Katibu Mkuu Sekretariet ya Jumuiya ya Afrika Mashariki wakiwa katika picha pamoja baada ya mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi za Wizara jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.