Na Mwandishi wetu, Dar
Nchi ya Finland imeipongeza
Tanzania kwa hatua mpya za kimaendeleo katika nyanja za ushirikishwaji wa sekta
binafsi, uhuru wa vyombo vya habari,utawala bora na haki za binadamu pamoja na
mapambano dhidi ya UVIKO 19.
Balozi wa Finland hapa nchini Mhe.
Riitta Swan ametoa pongezi hizo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb)
katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Balozi Swan amesema uamuzi wa Serikali
ya Tanzania wa kukuza sekta binafsi, uhuru wa vyombo vya habari, kutoa
kipaumbele kwa masuala ya utawala bora na haki za binadamu ikiwemo suala la
kujiunga na mpango wa chanjo dhidi ya UVIKO 19 ni hatua inayopaswa kupongezwa.
“……….pamoja na masuala mengine
suala la Tanzania kukubali chanjo dhidi ya ugonjwa wa UVIKO 19 ni maendeleo
mazuri sana kwa Taifa hili,” amesema Balozi Swan
Balozi Swan pamoja na mambo
mengine, amejadiliana na Balozi Mulamula masuala mbalimbali ya kuimarisha na
kukuza ushirikiano baina ya Finland na Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula amesema Tanzania na
Finland zimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu Tanzania ilipopata Uhuru
ambapo Finland imekuwa ikisaidia kukuza na kuendeleza sekta za kimaendeleo
hususan Elimu, Afya, Utalii, Mazingira pamoja na Maliasili.
“Katika jitihada za kuendeleza
ushirikiano wetu na Finland,imeandaa mpango mkakati wa maendeleo katika nyanja
mbalimbali kama vile masuala ya misitu, utawala bora, haki za binadamu na
masuala ya kuendeleza wanawake ambapo nimepokea rasimu ya mpango huo leo na
nitaufanyia kazi ili tuweze kuendeleza ushirikiano wetu kwa maslahi ya mataifa
yetu,” Amesema Balozi Mulamula
Balozi huyo wa Finland amekutana na
Balozi Mulamula kwa lengo la kuwasilisha mpango mkakati wa miaka minne wa
Finland katika nyanja za mashirikiano na Mataifa mengine ikiwemo kukuza na
kuendeleza diplomasia ya uchumi kupitia biashara na uwekezaji.
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akimkaribisha Balozi wa Finland hapa nchini Mhe. Riitta Swan wakati walipokutana
kwa mazungumzo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula
(Mb) akiteta jambo jambo na Balozi wa Finland nchini Mhe. Riitta Swan wakati wa
mazungumzo yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi
wa Finland nchini Mhe. Riitta Swan akimuelezea jambo Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) wakati wa
mazungumzo baina yao yaliyofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es
Salaam
Maongezi
baina ya Balozi wa Finland Mhe. Riitta Swan na Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula yakiendelea katika
Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.