Wednesday, August 25, 2021

WAZIRI MULAMULA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA WATANZANIA WAISHIO KENYA


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula amewahimiza Watanzania waishio ughaibuni (Diaspora) kwenye maeneo mbalimbali duniani kuwa na utaratibu wa kujitambulisha na kujiandikisha kwenye Balozi za Tanzania zilizo karibu yao ili kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa zao na kuwashirikisha kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

Waziri Mulamula ametoa rai hiyo alipokutana kwa mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Kenya katika mkutano uliofanyika kwenye Makazi ya Balozi jijini Nairobi hivi karibuni.

Mhe. Balozi Mulamula ambaye alifuatana na Mawaziri kadhaa kwenye mkutano huo, alisema kwamba kwa sasa Wizara ya Mambo ya Nje ina mpango mahsusi wa kuwatambua Diaspora wote kwa kukusanya taarifa zao na kuzihifadhi katika Kanzidata (Database) kwa lengo la kuiwezesha Serikali kuwa na taarifa muhimu za Watanzania hao hususan elimu, kazi, ujuzi na mitaji ili iwe rahisi kuwashirikisha kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ya taifa.

Kadhalika aliongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa na imejipanga kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuwawezesha kuchangia kikamilifu maendeleo ya nchi. “Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua mchango wa Diaspora kwenye maendeleo ya Taifa. Na haya si maneno yangu kwani tayari yameainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 184, sura ya 7 kipengele D pamoja na Sera mpya ya Mambo ya Nje ambayo imejumuisha masuala ya Diaspora” alisisitiza Balozi Mulamula.

Pia Mhe Balozi Mulamula alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania Kote ulimwenguni kuheshimu sheria za nchi walizopo na kupeperusha bendera ya Tanzania ya maadili mema ambayo inajulikana duniani kote. “Wapo Watanzania wachache wamefungwa magerezani kwenye nchi mbalimbali kwa makosa ya uvunjifu wa sheria. Tafadhali nawaomba mfuate sheria kwenye nchi mlizopo na mbebe bendera ya Tanzania ya tabia njema ambayo inajulikana duaniani” alisema Balozi Mulamula.

Kuhusu Lugha ya Kiswahili, Mhe Waziri Mulamula alitumia nafasi hiyo kuwahamasisha Diaspora hao kuchangamkia fursa ya kuanzisha vituo vya Kiswahili kwenye nchi walizopo ili kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa inayouzika. Pia aliwaomba kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutangaza biashara, uwekezaji, utalii na bidhaa za Tanzania ili kuchangia maendeleo ya nchi.

Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi ambaye amefuatana na Mhe. Waziri Mulamula nchini Kenya aliwahimiza Diaspora wanaohitaji ardhi kuja nchini na kufika Wizarani kwake ili kupata ufafanuzi wa kina wa masuala ya ardhi badala ya kutafuta taarifa nje ya utaratibu na kujikuta wanatapeliwa fedha zao.

Awali akimkaribisha Mhe. Waziri Mulamula, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Dkt. John Simbachawene alisema kuwa hali ya ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni nzuri na kwamba Watanzania wanaoishi nchini hapo wakiwemo wafanyabiashara, wafanyakazi na wanafunzi wanaendelea vizuri na shughuli zao bila kubughudhiwa. Aliongeza kuwa, hali hii ya utulivu imechangiwa kwa kiasi kikubwa na ziara ya Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika nchini Kenya mwezi Mei 2021.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watanzania waishio Kenya, Padri Cleophas Tesha alimshukuru Mhe. Balozi Mulamula kwa kutenga muda wa kuzungumza na Jumuiya hiyo na kumwomba kuendelea kuwashirikisha Diaspora kwenye mipango mbalimbali ya maendeleo ya nchi pamoja na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili Diaspora hao.

Mhe. Waziri Mulamula alikuwa nchini Kenya kwa ajili ya ziara ya kikazi pamoja na kushiriki Mkutano wa Nne wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano ambao ulifanyika nchini humo kuanzia tarehe 19 hadi 24 Agosti, 2021. Wakati wa Mkutano huo Mhe. Balozi Mulamula alifuatana na Mhe. Lukuvi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Joyce Ndalichako, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Khamis Chilo na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Exaud Kigahe.

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akisalimiana na baadhi ya Wanafunzi wanaosoma Vyuo mbalimbali nchini Kenya wakati alipokutana na Watanzania waishio nchini humo.

Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene akitoa hutuba ya kuwakaribisha wageni mbalimbali waliohudhuria hafla iliyowakutanisha baadhi ya Waheshimiwa Mawaziri wa Tanzania na Watanzania wanaoishi nchini humo iliyofanyika jijini Nairobi.

 Kutoka kushoto; Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi (Mb), Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene, Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (Mb) na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) wakiwa wamesimama wakati Wimbo wa Taifa ukiimbwa walipokuna kwa mazungumzo na Watanzania waishio nchini Kenya.

Waziri Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) Balozi wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. John Simbachawene na Prof. Prof. Patrick Loch Otieno Lumumba wakifurahia jambo walipokutana kwenye hafla iliyowakutanisha viongozi hao na Watanzania waishio nchini Kenya.
Mawaziri, Balozi wa Tanzania nchini Kenya na Watumishi wa Ofisi za Ubalozi wa Tanzania nchini humo wakiwa katika picha ya pamoja.


Mawaziri, Balozi wa Tanzania nchini Kenya na baadhi ya Watendaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wakiwa katika picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.