Waziri wa Nchi , Katiba, Sheria Utumishi wa Umma na Utawala Bora Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman akifungua Mkutano wa Kimataaifa wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi jijini Dar es Salaam |
Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo |
Washiriki wa Mkutano wa Kimataifa wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu wakifuatilia ufunguzi wa mkutano huo |
Mmoja wa viongozi wanaoshiriki katika mkutano huo akizungumza kitu na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu Mhe. Jaji Iman Abood baada y aufunguzi wa mkutano huo jijini Dar es Salaam |
Na mwandishi wetu, Dsm
Mkutano wa Kimataaifa kujadili utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama ya Afrika ya Watu na Haki za Binadamu, changamoto na matarajio yake umeanza jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku tatu umefunguliwa na Waziri wa Nchi Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora wa Zanzibar Mhe. Haroun Ali Suleiman kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussien Ali Mwinyi.
Akifungua mkutano huo Mhe. Suleiman amezitaka nchi za Afrika kuhakikisha Mahakama hiyo inakamilisha malengo ya kuanzishwa kwake.
"Mahakama ya Afrika ni taasisi yetu sote, tumeiunda sisi wenyewe na kwa maana hiyo naamini kuwa ni kwa maslahi yetu sote Waafrika tunajukumu la kuhakikisha taasisi hii haishindwi kufikia malengo yake" alisema Mhe. Suleiman na kuongeza kuwa hakuna mtu atakayenufaika iwapo Mahakama hiyo itafeli au kuwa taasisi isiyotekeleza kazi ya kulinda na kukuza haki za binadamu barani Afrika.
Amesema malengo ya Mahakama hiyo yataweza kufikiwa iwapo tu Serikali zote za bara la Afrika zitatelekeza kikamilifu maamuzi ya Mahakama hiyo.
" Niwaambie kuwa namna moja kuu ambayo Serikali zitawezesha Mahakama hii kufikia malengo yake ni kwa kutekeleza kikamilifu maamuzi yanayotolewa" alisema na kuongeza kuwa kufanya hivyo kutaionesha dunia kuwa nchi za Afrika zinachukua hatua kulinda na kukuza haki za binadamu kwa nguvu zote.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Mahakama ya Afrika Mhe. Jaji Iman Abood alisema mkutano huo umelenga kuangalia namna bora ya kuboresha utendaji kazi wa mahakama hiyo na changamoto zinazopitia nchi katika kutekeleza maamuzi yanayotolewa na Mahakama hiyo na hivyo kuja na suluhisho la pamoja ili kuziwezesha nchi zote kutekeleza maamuzi hayo.
Mkutano huo unashirikisha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na unahudhuriwa wanasheria waandamizi kutoka katika Serikali za nchi za Afrika kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa maamuzi yanayotolewa na Mahakama hiyo kwa nchi wanachama pamoja na changamoto zinazopitia nchi hizo na kutafuta namna ya kukabiliana nazo na matarajio yaliyopo kutokana na kuwepo kwa mahakama Mahakama hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.