Na Waandishi wetu, Dar
Tanzania na Uganda zimekubaliana kuimarisha
ushirikiano katika sekta mbalimbali za kimkakati zikiwemo nishati, utalii,
usafirishaji, viwanda, kilimo na uvuvi kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati wa mazungumzo
rasmi kati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
na Rais wa jamhuri ya Uganda, Mhe. Yoweri Kaguta Museveni yaliyofanyika leo
tarehe 27 Novemba 2021, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa ya mazungumzo baina yao kwa waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema
Tanzania na Uganda zimeendelea kushirikiana kwenye maeneo mbalimbali ya uwekezaji
na biashara kwa miaka mingi ambapo hadi sasa Uganda ni nchi ya pili kwa
uwekezaji nchini Tanzania kwa ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumezungumza masuala mengi na Mhe. Rais Museveni
na tumekubaliana kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kindugu uliopo kati yetu
hususan kwenye sekta za manufaa kwetu sote. Pia tumekubaliana kuimarisha
biashara na uwekezaji baina yetu na ninafurahi kuwajulisha kuwa hadi sasa Uganda
ni nchi ya pili kwa uwekezaji nchini Tanzania
kwa ukanda wa Afrika Mashariki ambapo ipo miradi 45 yenye thamani ya Dola
milioni 114 na imewezesha kutoa ajira kwa watanzania 2150”, amesema Mhe. Samia.
Kuhusu masuala ya biashara, Mhe. Rais Samia amesema
mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Uganda ni mzuri ambapo hadi kufikia
mwaka 2020 ujazo wa baishara kati ya nchi hizo umeongezeka hadi kufikia
Shilingi bilioni 607 kutoka shilingi bilioni 200 mwaka 20214.
Kadhalika, viongozii hao wamewaagiza Mawaziri
wanaoshughulikia masuala ya biashara wa Tanzania na Uganda kukutana mara kwa
mara ili kutatua changamoto mbalimbali za ufanyaji biashara na kuwataka
kukutana katika kipindi cha miezi miwili ijayo kujadili namna ya kuondoa
vikwazo visivyo vya kiforodha vilivyopo baina ya nchi hizo kwa lengo la
kurahisisha ufanyaji biashara.
Rais Samia ameongeza kuwa pia wamekubaliana kufungua
Ofisi ya Bandari nchini Uganda ili kurahisisha na kukuza biashara kati ya
Tanzania na Uganda.
Akizungumzia kuhusu Ugonjwa wa UVIKO 19, Mhe. Rais Samia
amesema wamekubaliana kuanzisha kiwanda cha pamoja cha kuzalisha dawa na chanjo
kwa ajili ya binadamu na wanyama kwa ajili ya kukabiliana na magonjwa ya
mlipuko ikiwemo UVIKO 19.
Aidha, Rais Samia ametumia fursa hiyo kumpongeza
Mhe. Rais Museveni kwa kufadhili ujenzi wa Shule ya Msingi huko Wilayani Chato,
Mkoani Geita na kusema kitendo hicho ni cha kuigwa kwani Mhe. Rais Museveni
anatambua umuhimu wa elimu kwa watoto wa Tanzania.
Rais Samia amesema pia katika mazungumzo yao
wamewaagiza Mawaziri wa Mambo ya Nje kufanya mkutano wa Tume ya Pamoja ya
Ushirikiano kati ya Tanzania na Uganda mwezi Disemba ili kuweka mikakati ya
kutekeleza makubaliano mbalimbali yaliyofikiwa kwa nyakati tofauti na nchini
hizi mbili.
Kwa upande wake, Rais Museveni amemshukuru mwenyeji
wake kwa mwaliko na kusisitiza kwamba ushirikiano huo wa kindugu kati ya Tanzania na Uganda utaimarishwa na kuenziwa kwa maslahi mapana ya pande zote
mbili.
Akizungumzia mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la
Afrika Mashariki, Rais Museveni amesema kuwa matayarisho ya msingi kuhusu kuanza
kwa ujenzi wa mradi wa bomba hilo yamekamilika.
Mhe. Rais Museveni yupo nchini kwa ziara ya kitaifa
ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine, atashiriki Kongamano la Biashara
kati ya Tanzania na Uganda, atatembelea Bandari ya Dar es Salaam na mradi wa Ujenzi
wa Reli ya Kisasa (SGR) pamoja na kukabidhi shule ya msingi iliyojengwa
Wilayani Chato kwa ufadhili wake.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimtambulisha
mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni kwa wakuu wa vyombo
vya Ulinzi na Usalama mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akisalimiana na viongozi mbalimbali
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makala. Wengine ni
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata
Mulamula (Mb), Balozi wa Tanzania Nchini Uganda, Dkt. Aziz Mlima pamoja na
Mkurugenzi Idara ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Naimi Aziz
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na mgeni
wake Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiteta jambo na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na
waandishi wa habari (hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam
Rais
wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Museveni akiongea na waandishi wa habari
(hawapo pichani) Ikulu Jijini Dar es Salaam
Baadhi ya Mawaziri, Wakuu wa vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na viongozi waandamizi serikalini wakifuatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula akisoma tamko la pamoja kati ya Tanzania na Uganda, Ikulu Jijini Dar es Salaam |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.